NA SHARON SAUWA
6th December 2012
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (Chadema), amegwaya baada ya kusema kuwa hatataja orodha ya vigogo walioficha fedha nje ya nchi kwa shinikizo kama ilivyokuwa kwa watuhumiwa 11 wa ufisadi, lengo likiwa ni kuwezesha uchunguzi wa kina kufanyika.
Akizungumza jana katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Star TV, Zitto, alisema badala ya kutaja majina hayo kwa lengo la kupata umaarufu wa siku chache, atalisaidia taifa kufanya uchunguzi utakaosaidia kuondokana na kitendo hicho cha kuhujumu uchumi wa nchi.
“Hili si jambo dogo hata kidogo, nashangaa limepunguzwa uzito kwa watu kutaka nitaje majina ya watu waliohifadhi fedha nje ya nchi, mwaka 2007 tulitaja orodha ya mafisadi 11 ni hatua gani zimechukuliwa?” alihoji Zitto na kuongeza: “Safari hii hatutataja majina ya watu hawa kwa mashinikizo.”Akizungumza jana katika kipindi cha Tuongee Asubuhi kinachorushwa moja kwa moja na kituo cha Televisheni cha Star TV, Zitto, alisema badala ya kutaja majina hayo kwa lengo la kupata umaarufu wa siku chache, atalisaidia taifa kufanya uchunguzi utakaosaidia kuondokana na kitendo hicho cha kuhujumu uchumi wa nchi.
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam mwaka 2007, alitaja majina ya watu 11 ambao chama hicho kilidai kuwa ni mafisadi.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), alisema kwa bahati nzuri Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, ameshaunda kikosi kazi cha kuchunguza tuhuma hizo.
Alisema yeye yuko tayari kushirikiana na kikosi kazi hicho katika kubaini ukweli wa tuhuma hilo.
Aliwataka Watanzania kusubiri taarifa ya uchunguzi huo ambayo serikali iliahidi kwamba itaiwasilisha bungeni katika Mkutano wa 11 utakaofanyika Aprili mwakani.
Zitto alisema kuwa anamshangaa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika, kusema kuwa Uswisi ambayo ni miongoni mwa nchi ambazo benki zake zinadaiwa kuhifadhi fedha hizo, imetoa masharti mazito ikiwamo ya kupelekwa kwa majina ya watu wanaodaiwa kuhifadhi fedha hizo.
“Mimi namheshimu sana Mkuchika, najua kuwa ni komredi na ni mjamaa anayefahamu jinsi baadhi ya mabepari wanavyoziibia serikali za Afrika,” alisema.
Alisema maneno hayo yaliyotolewa na serikali ya Uswisi ni ya kawaida na yamekuwa yakitolewa kila mahali na kutolea mfano kwa aliyekuwa Rais wa iliyokuwa Zaire (sasa DRC), Mobutu Seseseko, ambaye alificha mamilioni ya Dola za Manchini nchini Uswisi.
Zitto alisema kuwa serikali ya Uswisi iliwataka waliokuwa wakimlalamikia Mobutu watoe ushahidi kuhusiana na tuhuma hizo wakati ilikuwa wazi kabisa kwamba kwa mshahara aliokuwa akilipwa na serikali asingeweza kuwa na kiasi hicho cha fedha.
Alipoulizwa kuwa haogopi watu hao wenye fedha ambao wanajua wazi kuwa anawafahamu, Zitto alisema kuwa haogopi kwa kuwa wajibu wa mbunge ni kulisaidia taifa.
Alisema yeye amekuwa na rekodi ya kusimamia rasilimali za nchi na wakati mwingine kupiga kelele na kukumbusha jinsi alivyosimamishwa ubunge baada ya kuwasilisha hoja ya mkataba uliosainiwa na serikali kupitia kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Naziri Karamagi kuhusu mgodi wa Buzwagi.
Alisema ingawa alisimamishwa ubunge, lakini leo hii Watanzania wameweza kunufaika kwa kutengenezwa sheria mpya ya madini ya mwaka 2010.
“Sioni hapa kama ni suala la umaarufu wa kisiasa, bali hapa ninaliona ni suala la kiutendaji, mimi nazungumza kitu ambacho ninakiamini,” alisema.
Kuhusu gharama za uchunguzi wa sakata la ufichaji wa fedha hizo nje, Zitto alisema kuwa hakutumia fedha katika uchunguzi huo uliosababisha kuwakilisha hoja binafsi bungeni.
Alisema katika uchunguzi huo alisaidiwa na chama chake, wabunge wenzake na waandishi wa habari za uchunguzi ambao walikuwa na mawasiliano na baadhi ya watu katika nchi za Uingereza, Afrika Kusini na Uswisi
Aidha, alisema atakwenda nchini Ujerumani na kwamba pamoja na shughuli nyingine, atawasiliana na watu waliomsaidia katika uchunguzi huo ili kuwaomba kukisaidia kikosi kazi kilichoundwa kuchunguza sakata hilo.
Katika hoja yake binafsi aliyoiwasilisha katika mkutano wa Bunge uliopita, Zitto alilitaka Bunge liazimie serikali kupeleka bungeni muswada wa kupiga marufuku kiongozi yeyote wa umma au familia yake kuwa na akaunti nje ya nchi.
Alitaka muswada huo uwasilishwe katika mkutano wa 11 wa Bunge, utakaofanyika Aprili mwakani.
Aidha, alitaka Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi waeleze wamezipataje na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru) ichukue hatua za kisheria dhidi ya watu wote wenye kumiliki fedha na mali kinyume na mapato yao halali.
Hoja hiyo kwa mara ya kwanza iliibuliwa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina (CCM), katika Bunge la Bajeti la mwaka wa fedha 2012/ 2013 ambapo alikabidhi tafiti za utoroshaji wa fedha nje ya nchi.
Hata hivyo, Bunge liliazimia serikali ifanye uchunguzi kuhusiana na tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yake katika mkutano wa Bunge wa Aprili mwakani.
Zitto anadai kuwa jumla ya fedha zilizototoshwa nchini na kufichwa nje ya nchi ni zaidi ya Sh. bilioni 300.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment