Mwakilishi wa Hospitali ya Al-Rahma akipokea zawadi baada ya kuchaguliwa kuwa taasisi bora binafsi kwenye maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani hapo uwanja wa amani mjini Zanzibar.
Ukosefu wa uaminifu pamoja na kutofanya kazi kwa bidii miongoni mwa wafanyakazi ndio hali inayowafanya baadhi ya wawekezaji kutoka nje ya nchi kuwaajiri wageni na kusababisha hali ya mazingira ya ajira kwa Wazanzibari kutokuwa nzuri. Hivyo umuhimu wa wafanyakazi nchini kufanya kazi kwa bidii na maarifa utaendelea kuhitajika ili kukuza tija kazini sambamba na kurejesha imani kwa taasisi zinazotoa ajira.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idi kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohammed Sheni wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi zilizofanyika katika uwanja wa Amani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema kumekuwa na minong’ono kwa baadhi ya taasisi na makampuni yanayotowa ajira hasa yale yaliyomo ndani ya sekta ya Utalii dhidi ya baadhi ya Wanzibari na matokeo yake fursa hiyo huchukuliwa na wafanyakazi kutoka nchi jirani.
Alisema pamoja na kwamba Serikali ilijiwekea lengo la kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kutoka asilimia 7% mwaka 2007 hadi asilimia 4% mwaka 2010 lakini bado changa moto hiyo inaendelea kuliumiza kichwa Taifa.
Balozi Seif aliwataka Vijana kubadilika kwa kujenga utamaduni wa kujiajiri wenyewe kupitia vyama vya ushirika vya uzalishaji mali pamoja na kuunda saccos ili kujipatia tija itakayotoa unafuu.
“ Uzoefu unaonyesha kuwa Vijana wetu wengi wamekosa utamaduni wa kufanya kazi katika sekta binafsi. Matokeo yake vijana wetu huacha kazi baada ya kipindi kifupi cha kuajiriwa na nafasi zao kuchukuliwa na vijana wa je ya nchi “. Alisisitiza Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia wafanyakazi wote nchini kwamba Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha maslahi yao ikiwemo mishahara, posho, mazingira mazuri ya kufanyia kazi na maslahi mengine kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.
Alisisitiza kwamba kamwe Serikali Kuu haitaweza wala kuthubutu hata siku moja kuwatelekeza wafanyakazi waliomo ndani ya Taasisi zake kwa vile muda wote inatambua kilio cha wafanyakazi wake kikubwa kikiwa ni suala la maslahi bora.
Alisema suala la kulindwa na kupewa kwa maslahi wafanyakazi wa sekta ya umma kulingana na kazi wanazozifanya litapewa msukumo wa hali ya kipekee ili kujenga mazingira ya upendo na kuaminiana kati ya pande hizo mbili.
Hata hivyo Balozi Seif aliwakumbusha wafanyakazi kutekeleza wajibu wao kazini huku wakizingatia kwamba hakuna haki isiyokuwa na wajibu,akimaanisha kwamba haki na wajibu ni watoto pacha.
Akizungumzia suala la migogoro makazini Balozi Seif alisema kuwepo kwa kitengo cha usuluhishi na uamuzi wa migogoro ya mambo ya kazi ni hatua muhimu katika kupunguza migogoro ya kazi na mrundikano wa kesi mahakamani.
Alifahamisha kwamba kitengo hicho kimesaidia kuimarisha uhusiano mwema kazini kati ya waajiri na waajiriwa wakati inapotokea hitilafu ambapo hupata wasaa wa kujadiliana pamoja na hatimae kufikia usuluhishi unaofaa.
Akitoa salamu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo kwa Nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda Bibi Hopolang Phororo alisema ukosefu wa ajira kwa vijana, changamoto nyingi wanazozipata katika kutafuta kazi zenye staha ni masuala muhimu ya kuzingatia kwani yanaweza kuleta hatari na kuacha makovu ya kudumu katika Jamii.
Bibi Hopolang Phororo alisema Mataifa wanachama yanatakiwa kushughulikia kwa umahiri kipaumbele cha maendeleo ya kimataifa ambacho ni uzalishaji wa ajira zisizo za kulazimisha wala kubaguwa hasa kwa vijana .
Bibi Hopolang aliihakikishia Tanzania na Zanzibar kwa ujumla kwamba Shirika la Kazi Ulimwenguni litaendelea kuunga mkono harakati za Taifa hili katika kuimarisha viwango vya ajira Nchini Tanzania.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Jumuiya ya Waajiri Zanzibar (ZANEMA) Ndugu Salahi Salim Salahi aliikumbusha Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi kutafuta mbinu za kujenga uwezo wa vijana wa kuwa na taaluma itakayoweza kujiuza wenyewe.
Nd. Salahi alisema waajiri wengi wamekuwa wakikabiliwa na tatizo kubwa la kuwapata waajiriwa hasa kundi kubwa la vijana wenye uwezo kamili wa kuwajibika taaluma.
Mkurugenzi huyo wa Jumuiya ya waajiri Zanzibar alishauri kupitiwa upya kwa mitaala iliyopo hapa nchini ili itengeneze mazingira yatakayotowa fursa kwa vijana wanapomaliza masomo yao kuwa na uwezo kamili wa kuingia katika soko la ajira hasa lile la afrika Mashariki.
Mapema Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama huru vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) Maalim Khamis Mwinyi Mohammed amesifu hatua kubwa zilizofikiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuunda kanuni za ajira pamoja na utatuzi wa matatizo ya wafanyakazi.
Maalim Khamis alisema kumekuwa na mafanikio makubwa yaliyotekelezwa na Serikali kuu ambayo yalikuwa kilio cha muda mrefu miongoni mwa wafanyakazi walio wengi hapa Nchini.
Maadhimisho hayo ya siku ya wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) yametanguliwa na maandamano ya wafanyakazi kutoka taasisi za Umma, sekta binafsi pamoja na vijana wanaondesha pikipiki wakiongozwa na Bendi ya Chipukizi.
Katika maadhimisho hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitoa zawadi ya fedha taslim kwa wafanyakazi bora wa taasisi za umma na zile binafsi pamoja na vyetu maalum kwa Taasisi bora.
Ujumbe wa mwaka huu wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duiani mei mosi unasema Katiba Mpya izingatie Haki, Maslahi na usawa kwa wafanyakazi Nchini.
Chanzo: ZanzibariYetu!
Chanzo: ZanzibariYetu!
No comments :
Post a Comment