dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, June 22, 2013

Shivji aipasua rasimu

NA MWANDISHI WETU

22nd June 2013


  Ashangaa wanaoshabikia uwepo wa serikali tatu
  Zitaleta migogoro, ubabe na kuuvunja Muungano
Mwenyekiti wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shviji
Mwenyekiti  wa Kigoda cha Taaluma cha Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shviji, ameitolea macho Rasimu ya Katiba mpya huku akitahadharisha wanaoshabikia muundo wa serikali tatu kuwa, nchi itagawanyika vipande vipande na watakaoumia ni wananchi wa pande zote mbili.
Profesa Shivji amepinga kipengele cha Rasimu hiyo kinachopendekeza uwepo wa serikali tatu, kwa maelezo kuwa kutaleta migogoro, ubabe na kuuvunja Muungano.
Alisema anadhani Rasimu hiyo iliyowasilishwa na Tume ya kukusanya maoni ya Katiba Mpya chini ya Jaji Joseph Warioba, maoni mengi yalipatikana baada ya kuwepo mivutano mikali kati ya wajumbe wa Tanzania Bara na Zanzibar.
Akizungumza katika mhadhara wa kuaga nafasi hiyo, Profesa Shivji alitahadharisha kama umakini hautakuwepo na kushabikia muundo wa serikali tatu,  ile ya Shirikisho, Tanzania bara na Zanzibar, nchi itagawanyika vipande vipande na watakaoumia ni wananchi wa pande zote mbili.

Alisema kilichoteka kwenye rasimu hiyo anadhani ni kuwepo kwa ukinzani na hatimaye pande hizo kukubaliana kwa shingo upande ili kutokwamisha maamuzi na maudhui ya jambo hilo.
"Bahati mbaya hatuna mwenendo wa majadiliano ya Tume, lakini kwa vipengele vilivyopo ndani ya rasimu, hapana shaka yalikuwa maelewano na sio muafaka ambao wananchi wengi walitarajia kuiona Tanzania mpya," alisema Profesa Shivji.

Alisema ibara nyingi ndani ya Rasimu hiyo zina utata au ziko kimya katika masuala muhimu yanayozungumzia Muungano, ikiwamo mipaka ya nchi wanachama, mamlaka ya utawala, udhibiti wa Benki Kuu, raslimali za Muungano na vikosi vya ulinzi na Usalama.


Kitendo hicho, alikielezea kinaonyesha dhahiri Serikali ya Muungano haitakuwa na nguvu na udhibiti wa dola kikamilifu, hivyo kuna hatari nchi mwanachama mwenye nguvu kiuchumi kuingilia kazi za serikali ya Muungano.

"Kwa mfano ndani ya Rasimu inaonyesha Benki Kuu ya Muungano haitakuwa na majukumu muhimu ya kusimamia na kudhibiti mwenendo wa fedha kwenye benki kutoka pande mbili za nchi, hivyo itakuwa kama baraza la sarafu, kitu ambacho hakikubaliki," alisema.
Hata hivyo, alionya uwepo wa viongozi wanaotamani kuona katiba ya Tanganyika na kushangilia serikali tatu, ambayo itasababisha hasara kwa Watanzania na kunufaisha nchi za nje zinazonyemelea wingi wa rasilimali zilizopo nchini.
Alisema kihistoria hakuna nchi hata moja iliyoingia kwenye shirikisho ya serikali zaidi ya moja ikadumu, alitolea mfano nchi ya iliyokuwa Urusi, Yogoslavia na Bulgaria.

Wakitoa maoni yao, baadhi ya watu walioshiriki kongamano hilo walisema hakuna haja ya kuharakisha upatikanaji wa katiba mpya, badala yake waliomba kuwepo na muda wa kujadili ili kupatikana katiba inayokidhi matakwa ya nchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alipendekeza kuwepo muda mrefu wa kuijadili rasimu hiyo, ili kutoa fursa pana kwa wananchi walio wengi kushiriki.

Mkuu wa kwanza wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Ualimu Dar es Salaam (Duce), Profesa Herman Mushi, alitaka iwekwe wazi wanaohitaji muundo wa utawala kiserikali nchini.
Alikosoa kuundwa kwa wilaya na mikoa mingi nchini na kusema katika dunia yenye ushindani katika ukuaji uchumi, sayansi na teknolojia, hakuleti ufanisi.
Akichangia hoja kwenye mhadhara huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Hellen Kijo Bi-Simba alisema kuwa, mara baada ya kutangazwa kwa rasimu hiyo, walianza kuichambua na kuipongeza tume kwenye yale waliyoyaleta lengo likiwa ni kuiboresha.
Alisema wachangiaji wengi jana wamezungumzia muungano na kuomba suala hilo liangaliwe kwa uzito wake.
Pia ametaka suala la rasilimali liangaliwe kwa sababu nchi tayari imeshuhudia migogoro huko Mtwara na Arusha.
Profesa Shivji akitoa neno la mwisho kabla ya kufungwa kwa mdahalo huo, alisema nia yake sio kuponda bali ni kufanya uchambuzi ili kuionyesha jamii yale ambayo hayaonekani moja kwa moja kwenye rasimu hiyo.

Akijibu baadhi ya maoni yaliyotolewa na wachangiaji, alisema sio kweli wasomi hawatoi njia mbadala kama ilivyoelezwa na kwamba binafsi amewahi kutoa mfumo mbadala wa muungano.
Aliongeza kuwa, jambo muhimu alilotegemea kutoka kwenye tume ni kuwaondosha kutoka mjadala wa Muungano na kuhoji kuwa kitaaluma nani anasema kuna serikali mbili.
“Kuna serikali mbili na nusu, tuondokane na msamiati huu, sisi na wasomi tuzungumzie muungano wetu kwa jicho la kidemokrasia hii inawahusu Tanzania Bara na Visiwani,” alisema.
Akihitimisha mahadala huo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mkandara, alisema kuwa tukio hilo limewafungia kipindi cha hekaheka cha kufundisha darasani. Aidha, Mkandara alimsifu Profesa Shivji kwa mada yenye weledi na ufanisi.
“Naamini yametoa hamasa kwetu na wanaotusikiliza, pia mjadala umetupa ari wa kutimiza wajibu wetu kiraia katika kuipata katiba itakayokubalika kwa kila Mtanzania,”alisema.
Alisema Shivji ameandaa mhadhara huo kama Profesa wa kigoda cha Mwalimu Nyerere ambaye ni mshiriki wa karibu katika kubuni kigoda hicho.

Aliwashukuru marafiki wa kigoda waliopo ndani na nje ya nchi na kukishukuru kituo cha televisheni cha ITV kwa kurusha moja kwa moja matangazo hayo.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment