zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, September 6, 2013

Kikwete ajiponza kwa uongozi wake mwenyewe

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete
Ahmed Rajab
Toleo la 314
4 Sep 2013
KUNA nyakati ambapo huruma zangu hunifanya nitamani kutafuta chetezo na ubani niende Ikulu, Dar es Salaam, nikamzungue Rais Jakaya Kikwete. Amelemewa na mengi.  Amezongwa na mengi.
Kila uchao inazidi kubainika kwamba Rais wetu anakabiliwa na changamoto nyingi zaidi kushinda tunavyomfikiria.
Mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame, amemtia ndaro kiasi cha kumfanya atikisike. Kwa miezi mitatu sasa viongozi hao wawili wamekuwa wakizozana.
Uhusiano wao ulianza kwenda kombo pale Kikwete alipoishauri Rwanda ifikirie kuzungumza na kundi la wanamgambo wa Kihutu la Forces Démocratiques pour la Libération du Rwanda (FDLR), lenye kusema kwamba linapigania ukombozi wa Rwanda na ambalo kwa sasa linafanya mashambulizi mashariki mwa Congo-Kinshasa.
Wenzake Kikwete ndani ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki wanamshtumu kwa ajizi aliyonayo katika kuchukua hatua zinazohitajika za kufanikisha Shirikisho la Afrika ya Mashariki.
Huo usiri wake Kikwete umewamahanisha wenzake. Mwezi Novemba Kagame, Uhuru Kenyatta na Yoweri Museveni wanatazamiwa kukutana mjini Arusha. Watapokutana watakuwa wamekwishaipitia rasimu ya katiba ya shirikisho la kisiasa la Afrika ya Mashariki.
Kikwete hatokuwa amechangia kitu katika rasimu hiyo. Hivyo, Tanzania itawekwa nyuma tu katika mipango ya kuleta umoja wa kisiasa wa nchi za Afrika Mashariki.
Uhuru na Museveni wanamuonyesha kwamba wao peke yao, bila ya yeye, wanaweza kuiongoza Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuielekeza kwenye shirikisho la kisiasa.
Hivi majuzi Kagame, Museveni na Uhuru walikutana Mombasa kushauriana kuhusu miradi kadhaa ya miundombinu.  Hawakumwalika Kikwete lakini walimwalika Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi ingawa alikhiyari asihudhurie. Badala yake alimpeleka waziri wake wa usafiri, Deogratias Rurimunzu ahudhurie mkutano huo.
Sudan ya Kusini, ambayo bado si mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki, nayo pia ilialikwa kwenye mkutano huo wa Mombasa.
Hayo ni ya nje ya mipaka ya Tanzania. Nchini, Kikwete anakabiliwa na uhasama mkubwa wa wazi na wa chini kwa chini ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ambacho yeye ndiye mwenyekiti wake. Wiki iliyopita alionekana jinsi alivyoshindwa kuzuia Mansoor Yussuf Himid asijadiliwe na kufukuzwa chamani.
Sasa kuna waliokwishapania mashati kutaka kuukwamisha mchakato wa kulipatia taifa Katiba Mpya. Hawa ni wale wenye mawazo yalioganda wenye kufikiri kwamba hatima ya Tanzania inategemea vile kitakavyo chama chao cha CCM.
Ni mkosi gani uliomfika Kikwete? Nadhani ni namna yake ya kuongoza. Uongozi wa urais una mushkeli usio mdogo.  Kishindo kikubwa anachokipata Rais ni pale anapojaribu kuongoza na akiangalia nyuma akaona kwamba hana mtu nyuma yake.
Mara nyingi Urais huonekana kuwa na nguvu zaidi ya zilivyo hasa. Na sisi waandishi, wasomi na hata marais wenyewe tumezoea kuzikuza nguvu hizo laisa kiasi.
Tukijaribu kuangalia ni Rais gani aliyekuwa na athari kubwa juu ya Tanzania tangu nchi hii izaliwe baada ya Tanganyika na Zanzibar kuungana hamna shaka yoyote ile kwamba atayechomoza atakuwa Julius Nyerere. Si athari zake zote zilizokua nzuri. Lakini ukweli ni huo kwamba aliiweza Tanzania.
Kuna wataalamu wa nadharia za uongozi wenye kuamini kwamba kwa hakika athari ya marais juu ya mambo yanavyokwenda nchini ni ndogo. Wanaikisia kuwa kama asilimia 10 au 15 tu. Asilimia kubwa ni ya msukumo wa nguvu nyingine katika jamii.
Ni nadra sana kumpata kiongozi anayekuwa na athari kubwa kiasi cha kuifanya jamii imfuate bila ya kumtilia shaka. Mfano mkubwa labda ni ule wa Nelson Mandela alipokuwa Rais wa Afrika Kusini.
Kweli Rais anapaswa awe kiongozi, awe na uwezo wa kuongoza. Lakini katika siasa za urais uongozi au huo uwezo wa kuongoza unaweza ukaficha mengi.
Uongozi unahitaji sifa fulani. Miongoni mwa sifa hizo ni ustadi wa kisiasa. Kiongozi awe na ujasiri, kwa mfano, wa kushirikiana na mahasimu wake wa kisiasa inapohitajika.
Ustadi huo tuliushuhudia Zanzibar pale Rais mstaafu Amani Abeid Karume, akiwa makamu mwenyekiti wa CCM, na Maalim Seif Sharif Hamadi, akiwa katibu mkuu wa CUF, walipokubaliana kwamba vyama vyao viachane na uhasama wao na viwe na maridhiano. Viongozi hao wawili ni mfano mzuri wa viongozi walio mastadi wa kisiasa.
Sifa nyingine anayohitaji kuwa nayo kiongozi ni uwezo wa kung’amua pale anapodanganywa na wafuasi wake.  Udanganyifu huu ni wa hatari. Aghalabu wafuasi wake, hasa wale wanaojipendekeza kwake, wanakuwa na tabia ya kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa. Wanamwambia mambo ambayo wao wanahisi kuwa yeye angependa kuyasikia.
Kiongozi hawi kiongozi mzuri ikiwa hana uwezo wa kuendesha mambo au ikiwa hawezi kuyakiri makosa yake na kuyatumia makosa hayo kuwa funzo kwake.
Kadhalika kiongozi anatakiwa awe na umahiri wa kuwateua watu walio wachapa kazi, walio waadilifu na walio tayari kumueleza ukweli bila ya hofu ya kumuudhi.
Kiongozi haonekani kuwa ni kiongozi wa kweli ikiwa hajui namna ya kuhutubu lakini kiongozi mzuri ni yule ambaye pia anajua wakati gani akae kimya, afunge mdomo wake, asiseme kitu.
Na pale anapokuwa anataka kukwamishwa na wenzake — kama hivi sasa ambapo kuna wanaotaka kumkwamisha Kikwete kuhusu mchakato wa Katiba — kiongozi anapaswa aweze kuuendea umma moja kwa moja kutaka ridhaa yao badala ya kutegemea vikao vya chama chake.
Nadhani uongozi wa matao ya chini unaweza ukawa na athari kubwa kushinda ule wenye kujigamba kwa uadilifu na wenye kutumia umahiri wa balagha — uwezo wa kuzungumza kwa fasaha na kuweza kuwashawishi watu kwa hoja.  Hata hivyo, sidhani kwamba uongozi aina hiyo, ambao ndio alionao Kikwete, unayafaa mataifa kama yetu.
Ninaamini Nyerere akiogopwa kwa sababu hakuwa kiongozi wa matao ya chini. Akiongoza kwa mikogo huku akijigamba kwamba sera zake zilikua zinakwenda sambamba na maadili mema na kwa falsafa yake ya kupigania wanyonge na kupinga kila aina ya ufisadi.
Zaidi ya yote alibarikiwa kipaji kikubwa cha balagha kilichomfanya awateke akili wengi wa wananchi wenzake.
Kweli Ali Hassan Mwinyi, Rais wa pili wa Tanzania, aliliongoza taifa kwa matao ya chini na aliweza kuwa na athari kubwa juu ya mwelekeo wa uchumi wa kitaifa. Hata hivyo, nadhani alilazimika kuufungua uchumi kwa sababu hali halisi ilishurutisha afanye hivyo. Asingeufungua basi uchumi ungelizidi kudidimia na hata taifa lingeliweza kusambaratika.
Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete wote hawakuingia Ikulu na falsafa yoyote yao wenyewe waliotaka kuitekeleza. Wote ni viongozi waliokuwa wakiongozwa. Kinyume na Nyerere aliyekuwa akikiongoza chama cha CCM hawa watatu walikuwa wakiongozwa na chama chao.
Nyerere alikuwa na ndoto ya kutaka kuiumba tena Tanzania iwe taifa linalofanana na jinsi alivyotaka taifa lake liwe.  Waliomfuatia hawakuwa na ndoto hiyo. Wala hawakuwa na fikra zilizoweza kuivuka mipaka ya Tanzania kama zilivyokuwa zikivuka fikra za Nyerere.
Ndio maana hii leo sauti ya Tanzania imefifia katika majukwaa mbalimbali — toka ya kanda hii ya Afrika ya Mashariki, ya Afrika na hadi ya kimataifa.  Na ndio maana hii leo jirani zetu wa Afrika ya Mashariki wakathubutu kuipuuza Tanzania, wakawa tayari kuchukua hatua wanazotaka bila ya kuisubiri Tanzania.
Pia kiyume na Nyerere hawa watatu hawakuwa na wafuasi kokote kwingine, si Afrika si nje ya Afrika.
Nyerere lakini alichukua hatua moja ambayo hawa watatu hawakuichukua.Alilitumbukiza taifa vitani.Aliyapeleka majeshi yake Uganda kwenda kumpindua Rais Idi Amin.Si kwamba tunataka nchi iingie vitani lakini ujasiri huo Kikwete hanao.
Chanzo: Raia Mwema

No comments :

Post a Comment