NA MWANDISHI MAALUM
8th September 2013
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema hayo wakati akifungua majengo mapya ya Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya mjini hapa.
Alisema, “serikali inachukua jitihada mbalimbali za kuendelea kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wetu wa sekta ya afya kwa kutambua umuhimu wao.”
Aliongeza kuwa maslahi ya watumishi hao yataboreshwa kadri uchumi utakavyoruhusu na kwa kuzingatia miundo ya utumishi iiyopitishwa hivi karibuni.
Alisema changamoto kubwa inayoikabili serikali katika kutekeleza azma hiyo ni ukosefu wa fedha jambo ambalo alikiri kuwa si kwa Zanzibar pekee bali katika nchi nyingi duniani.
Dk. Shein aliwaambia wanachuo na wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa ajira kwa wanafunzi wanaohitimu mafunzo katika sekta ya afya hazicheleweshwi na kwamba zitafanyika kwa kuzingatia muundo wa utumishi kwa watumishi wa sekta hiyo.
Katika hotuba yeke hiyo Rais wa Zanzibar alitangaza rasmi uamuzi wa Serikali wa kukiweka chuo hicho chini ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (SUZA).
“Tumeamua chuo hiki kiwe chini ya uongozi wa SUZA bila ya kubadili mitaala yake ya masomo na kwamba taratibu za mabadiliko haya yanashughulikiwa na kamati iliyoundwa kufanya kazi hiyo”alieleza Dk. Shein na kusisitiza kuwa hakuna mjadala tena wa jambo hilo.
Sambamba na kutangaza uamuzi huo Dk. Shein alitoa wito kwa Wizara na uongozi wa chuo cha afya kukubali mabadiliko vinginevyo watabaki nyuma wakati wengine wakisonga mbele.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment