Source: HABARI LEO
SHIRIKA la Biashara la Zanzibar (ZSTC) linatarajia kutumia jumla ya Sh bilioni 32.5 kwa ajili ya kununua karafuu kwa msimu wa uchumaji wa zao hilo, uliyoanza visiwani humo.Naibu Mkurugenzi wa Shirika hilo, Suleiman Jongo alisema jana kuwa msimu wa kuchuma karafuu umeanza na Shirika limeanza kununua karafuu kutoka kwa wananchi.
“Tumeanza kununua karafuu kutoka kwa wananchi kote Unguja na Pemba…sambamba na kazi ya ZSTC ya kuimarisha vituo vyake vya kuuzia karafuu kwa upande wa Pemba, ili kuwa vya kisasa kabisa,” alisema Jongo.
Alisema ZSTC, imekadiria kununua kutoka kwa wananchi kiasi cha tani za karafuu 4,852 ambapo kiwango kikubwa ni kutoka kisiwani Pemba.
Serikali ya Zanzibar, bado inategemea zao la karafuu katika kuimarisha uchumi wake, ambapo pia inaelezwa hadi sasa Kisiwa cha Pemba, kinazalisha asilimia 90 ya zao hilo.Mapema katika maelezo yake, Naibu Mkurugenzi huyo aliwapongeza wananchi wa Pemba, kwa kuuza karafuu zao kwa ZSTC na kuwashukuru kwa kuacha kuzisafirisha kwa magendo.
Serikali ya Zanzibar, kupitia taasisi zake za kilimo na masheha imeweka msisitizo kwa wananchi wa Unguja na Pemba, wanaomiliki mashamba kufufua ulimaji wa zao hilo.
Tangu kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya saba ya umoja wa kitaifa, imefungua milango zaidi ya kushajiisha wananchi kurudisha moyo wa kulima mikarafuu.
Huku ikiwahimiza wananchi kupanda kwa wingi mikarafuu, serikali imekuwa ikizingatia mafanikio ya wananchi kwa kununua karafuu zao kwa bei ya kuwavutia.
Serikali ya Zanzibar, imepandisha bei ya zao hilo na sasa inanunua kutoka kwa mwananchi kilo moja ya karafuu daraja la kwanza kwa Sh 17,000/- na daraja la pili ni Sh 14,000/-..
No comments :
Post a Comment