10th November 2013
Msimamo uliotangazwa na Rais Jakaya Kikwete wakati analihutubia Bunge katikati ya wiki hii, ulidhihirisha kuwa Tanzania haina mpango wa kujitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Huu ni msimamo thabiti usio na chengachenga. Hongera sana Rais wetu.
Awali, ilikuwapo minong'ono ya muda mrefu kuwa Tanzania imebaguliwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, suala ambalo lilifafanuliwa vizuri na Rais Kikwete wiki hii kwamba Tanzania haiwezi kujiondoa kwani haijafanya jambo lolote baya dhidi ya Jumuyia hiyo au dhidi ya nchi yoyote mwanachama na wala hakuna ushahidi wa jambo hilo.
Rais Kikwete alizikumbusha nchi wanachama kuwa Tanzania imekuwa mwanachama mwaminifu, mvumilivu na mtiifu kwa Jumuiya hiyo, na ndiyo maana vitendo vinavyofanywa na viongozi wa nchi tatu wanachama, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Yoweri Museveni wa Uganda pamoja na Paul Kagame wa Rwanda alisema vinazua maswali mengi ambayo hayana majibu.
Tunaamini kwa vitendo ambavyo vimefanywa na viongozi hao, vya kufanya majadiliano kwa nchi tatu tu yanayohusu Jumuiya bila kuhusisha nchi za Tanzania na Burundi, ambazo pia ni wanachama halali, wamekiuka Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kuwa na vikao vya pamoja.
Rais Kikwete alisema yapo madai kwamba ushirikiano wa nchi hizo tatu ungeliwezesha kuharakisha maendeleo ya Jumuiya hiyo, sisi tunaamini kuwa hayo ni madai yasiyokuwa na ukweli wowote, kwani haiwezekani wakaacha kuwaalika baadhi ya viongozi wa ndani ya Jumuiya halafu wenyewe wakadai nchi ambazo hazikualikwa hawana utayari.
Akasema tunaamini Tanzania inaheshimu mkataba ulioanzisha Jumuia hiyo, na ndiyo maana iko tayari kuchangia dola za Marekani milioni 12 kila mwaka kwa ajili ya Jumuia ya Afrika Mashariki. Huo ni moja ya ushahidi wa ishara ya uzalendo wa dhati wa Tanzania katika Jumuiya.
Sasa inawezekanaje wakati huo huo Tanzania ikageuka na kuwa nchi ya kwanza kuidhoofisha Jumuiya hii? Kama lipo ambalo Tanzania haijafanya vizuri ni kwa sababu tu za msingi na siyo vinginevyo. Jumuiya ya Afrika Mashariki ni chombo kikubwa, kinachowaunganisha wananchi wa nchi zote wanachama kiuchumi, kitamaduni na hata kijamii.
Yapo masuala mengi yanayotakiwa kuzingatiwa kabla ya kuwajumuisha wananchi wa nchi wanachama kama familia yenye mwelekeo mmoja. Na ndiyo maana Rais Kikwete aliwaambia wabunge kuwa kinachoonekana kuwakera viongozi wa nchi zingine ndani ya Jumuiya hiyo, ni msimamo wa Tanzania katika kupinga kuharakisha kwa Shirikisho, na katika eneo la umiliki wa ardhi, uhamiaji na ajira.
Ni ukweli usiopingika kuwa jambo jema, lililojengeka katika misingi imara, hudumu kwa muda mrefu. Hii ndiyo sababu Tanzania inaingiwa hofu ya kukimbilia kwenye Shirikisho kabla ya kuimarishwa vipengele na taasisi muhimu zinazoimarisha ushirikiano wa Jumuiya yenyewe.
Hatua muhimu zinazotakiwa kuzingatiwa kwenye Jumuiya ni pamoja na kuundwa kwa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Fedha ndipo hatua ya kuundwa kwa Shirikisho la kisiasa kufanyike, tena hiyo inakuwa baada ya kupata ridhaa kwa kupigiwa kura za maoni toka kwa wananchi wa nchi wanachama.
Tunaunga mkono na kupongeza hoja zote zilizotolewa na Rais Kikwete wakati anahutubia Bunge na kuelezea msimamo wa Tanzania kuhusu ushiriki katika EAC. Hakika, huo ndiyo msimamo wa wananchi wote kwani kimsingi kila nchi ina maslahi yake kwa wananchi wake, ambayo yanatakiwa yalindwe kisheria na kuwanufaisha wahusika bila upendeleo.
Shirikisho la Afrika Mashariki ni suala muhimu katika kuinua uchumi wa pamoja wa nchi wanachama, na ni lazima misingi na sheria zilizowekwa katika kulianzisha ziheshimiwe, zifuatwe na kutekelezwa hatua kwa hatua. Tunaamini huo unaweza kuwa msingi wa kulifanya Shirikisho la Afrika Mashariki likadumu kwa muda mrefu kwa faida ya wananchi wake.
Tunaamini pia mafanikio katika mchakato huu wa kuundwa kwa Shirikisho la Afrika Mashariki yatakuwapo kama taratibu na sheria zitazingatiwa. Na zaidi ya yote, nchi za EAC zinatakiwa kuvumiliana, kuheshimiana pamoja na kushirikiana kwa masuala yote ya Shirikisho bila kubaguana. Wanaokiuka makubaliano wapime, wajiridhishe kama wako sahihi au la.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment