NA GIDEON MWAKANOSYA
26th November 2013
Mtoto huyo alijeruhiwa vibaya sehemu za usoni na mdomoni na kusababishwa ashonwe nyuzi sita, alipatwa na mkasa huo mwishoni mwa wiki iliyopita na anayetuhumiwa kufanya kitendo hicho ni Ronginus Haule (58), mkazi wa eneo hilo.
Haule anadaiwa kushambulia mtoto huyo ambaye ni mtoto wa Mtangazaji wa kituo kimoja cha redio cha mjini Songea kwa mapanga kwa tuhuma za kumkuta akichuma mapera katika bustani yake jirani na nyumba yake.
Mtoto Benson alipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Ruvuma na kulazwa Chumba cha Uangalizi Maalum (ICU) ambako alishonwa nyuzi sita na hali yake sasa imeelezwa kuwa inaedelea vizuri.
Mama mzazi wa Benson, Rwosita Nyoni, alisema siku ya tukio, mtoto wake aliondoka nyumbani tangu saa 7:00 mchana.
“Nilimtafuta ili aje ale chakula cha mchana, lakini sikumuona. Ilipofika saa moja jioni wakati nikitoka kanisani, niliona mkusanyiko wa watu wakimshangaa mtoto ambaye hakufahamika akiwa amejeruhiwa vibaya huku mwili wake umetapakaa damu na amepoteza fahamu,” alisema mama wa mtoto huyo.
Hata hivyo, mmoja wa majirani alisema alimshauri amwangalie vizuri majeruhi huyo huenda ni mwanawe.
“Na kweli nilipomsogelea, niligundua kuwa ni mwanangu Benson, jambo ambalo lilinishtua sana. Ndipo nilipoamua kwenda polisi ambako nilipatiwa PF 3 na nikampeleka Hospitali ya Mkoa kwa matibabu,” alisema.
Kwa upande wake, muuguzi wa zamu wodi namba tano alikolazwa mtoto huyo, Ernesta Kapinga, alisema alipofikishwa hospitalini hapo, alikuwa na hali mbaya na alipelekwa ICU kwa uangalizi zaidi.
Kwa mujibu wa muuguzi huyo, mtoto huyo aliumizwa sehemu za ndani ya kichwa jambo lililosababisha kukojoa damu.
“Tunahisi ameumizwa ndani kwa ndani na damu zitakuwa zimevujia kwenye ubongo na sehemu za tumbo, kwa sasa tunasubiri majibu ya X-ray ili tubaini ameumia zaidi maeneo gani,” alisema muuguzi huyo.
Mmoja wa wanaharakati wa Kituo cha Wasaidizi wa Sheria, Wanawake na Watoto mkoani Ruvuma, Fatuma Misango, alielezea kusikitishwa kwake na tukio hilo ambalo alisema adhabu aliyopewa mtoto huyo haiendani na umri wake pamoja na kosa lenyewe.
Kwa msingi huo, Misango amelitaka Jeshi la Polisi kutolifumbia macho tukio hilo kwani vitendo vya ukatili dhidi ya watoto vinazidi kuongezeka katika jamii.
Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Songea, Dk. Benedicto Ngaiza, alithibitisha kumpokea mtoto huyo na kwamba kwa sasa anaendelea kupatiwa matibabu akiwa chini ya uangalizi maalum.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Revokatus Malimi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kumshikilia Haule kwa tuhuma za kumfanyika ukatili mtoto huyo.
Malimi alisema kuwa polisi walimtia mbaroni mtuhumiwa huyo baada ya kupata taarifa za kumjeruhi mtoto huyo kwa kucharanga mapanga baada ya kumkamata kwenye bustani yake kwa tuhuma za kuchuma mapera Novemba 22, mwaka huu saa 12.30 jioni katika mtaa wa Madizini Lizaboni.
Alisema inadaiwa siku hiyo ya tukio mtuhumiwa huyo akiwa ndani ya pagale alimnyemelea mtoto huyo na kumjeruhi vibaya usoni na sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia kitu chenye ncha kali.
Alisema kuwa taarifa za tukio hilo zilifikishwa katika kituo kikuu cha polisi na Mwenyekiti wa Mtaa wa Madizini, Addo Mkanula, akiwa amembeba majeruhi huyo na baadaye alipatiwa hati namba 3 ya matibabu kisha majeruhi huyo alipelekwa hospitalini na kulazwa.
Alisema kuwa hali ya majeruhi huyo bado ni mbaya na anaendelea kupatiwa matibabu.
Kamanda huyo alisema polisi wanaendelea kumuhoji mtuhumiwa na kutafuta ushahidi zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Alisema watakapokamilisha vitu hivyo, polisi watamfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo kujibu mashtaka.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment