Ripoti Maalum: Maajabu Songosongo
15th January 2014
Umeme, maji, shule, usafiri wa ndege bure
Nyumba zote kisiwani humo, zikiwamo ndogo kabisa zilizojengwa kwa udongo na mawe na kuezekwa kwa makuti, zimeunganishiwa umeme ambao ni wa bure.
Watumiaji hawalipi hata senti tano, hiyo ikiwa ni fursa ya kipekee kwani ni asilimia 17 tu ya Watanzania waliounganishiwa nishati huyo hadi sasa huku lengo la Serikali likiwa ni kufikia asilimia 30 hadi ifikapo mwishoni mwa mwaka 2015.
Wakati Serikali ikipanga kuwa hadi kufikia bajeti ya 2015/2016 ndipo asilimia 74 ya Watanzania wapate maji safi na salama, Songosongo mambo yao si mabaya. Kila kaya hupatiwa maji safi na salama bure.
Na wenye safari za kwenda jijini Dar es Salaam, Lindi na Mtwara husafirishwa kwa ndege bure huku neema kubwa kuliko yote ikiwa ni ile ya watoto wao 10 wanaofaulu darasa la saba katika kila mwaka hupelekwa katika Shule ya Sekondari ya Makongo iliyopo jijini Dar es Salaam na kusomeshwa pia bure.
Hawa hupewa fursa hii kuanzia kidato cha kwanza hadi kufikia ukomo wao darasani; kwa maana ya kugharimiwa kila kitu hadi chuo kikuu bila kujali ikiwa watafikia ngazi ya udaktari na hata uprofesa.
Aidha, vinono wanavyovipata watu wa Songosongo hunogeshwa pia na ukweli kuwa wamejengewa kituo kizuri cha afya ambacho kimesakafiwa kwa marumaru na wagonjwa wote huketi kwenye masofa wakati wakisubiri kumuona daktari au kupata huduma zote kama za kuchoma sindano na kupimwa afya zao.
Kama hiyo haitoshi, mgonjwa anapozidiwa na kuonekana kuwa ni lazima ahamishiwe kwenye Hospitali ya Wilaya ya Kilwa Kivinje, husafirishwa bure pia kwa boti iendayo kasi, umbali wa zaidi ya maili 16.
“Hizi ni baadhi ya neema tele wanazopata wananchi wa Kisiwa cha Songosongo katika wilaya yetu hii,” ndivyo anavyosema Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Abdallah Ulega, katika mahojiano maalum na NIPASHE ofisini kwake wiki iliyopita.
Ulega alisema kuwa chanzo cha neema zote hizo kwa wananchi wa Songosongo ni kuwapo kwa miradi ya uchimbaji gesi katika kisiwa hicho inayofanywa na wawekezaji, kampuni ya PanAfrican Energy Tanzania (PAT).
“Nenda mwenyewe Songosongo na utashuhudia... kwa kweli kuna mengi mazuri ambayo wananchi wenyewe ndiyo watakaokusimulia vizuri,” alisema Ulega.
Aliongeza kuwa siyo vibaya kwa wawekezaji wa maeneo mengine nchini kufika Songosongo ili kujifunza namna ya kuishi vyema na wenyeji ambao ni wadau muhimu katika kufanikisha mradi wowote ule.
UKWELI
Baada ya kupata maelezo ya Ulega, mwandishi alikwenda Songosongo. Akapanda boti iitwayo Tuluino ‘Chuma kwa Chuma’, ambayo ndiyo pekee yenye vifaa vya kuokolea (life jackets) kati ya zile zinazoanzia safari zake katika Bandari ya Kilwa Kivinje.
Safari ilianza saa 10:15 jioni. Licha ya bahari kuchafuka sana kutokana na pepo kali za Kaskazi, hasa katika maeneo ya Jewe, Jengela na Chapachapa, hatimaye boti hiyo iliyokuwa ikiendeshwa na nahodha Atupele Ngara Gwakabale ilifika salama kisiwani Songosongo. Muda huo ilikuwa ni saa 11:54.
Mara tu baada ya kufika kisiwani humo, mwandishi akaanza kujionea maajabu. Kweli, nyumba karibu zote zilikuwa na umeme ndani yake, zikiwamo za makuti. Hata hivyo, siyo nyingi zilizoonekana kuwa na nyaya za umeme kutoka kwenye nguzo kwani wengi hupitisha umeme wao ardhini. Kuzibaini kuwa zina umeme huwa ni rahisi sana kwani balbu huwaka muda wote usiku na nyingine hadi mchana; huku nyingi pia zikiwa na majokofu kwa vile shughuli ya wakazi wengi ni uvuvi, hivyo kifaa hicho ni muhimu zaidi kwao kwa ajili ya kuhifadhia samaki.
Miundombinu ya Kituo cha Afya cha Songosongo kilichopo eneo la Kisunni pia ni ya kipekee. Jengo zima ambalo kwa mara ya kwanza lilizinduliwa mwaka 1987 na aliyekuwa Waziri Mkuu wa wakati huo, Joseph Warioba, limefanyiwa ukarabati mkubwa na kweli, sakafu yake imenakshiwa kwa marumaru na wagonjwa husubiri huduma wakiwa kwenye makochi, tofauti na hali ilivyo katika vijiji vingi nchini.
Kwa msaada wa wawekezaji wa gesi, wakazi wa Songosongo wamejengewa pia shule nzuri ya chekechea, sekondari yenye bweni maalum kwa ajili ya wasichana na pia wameboreshewa baadhi ya majengo ya shule yao ya msingi.
“Kwa kweli tunajiona kuwa ni wenye bahati ya pekee ndani ya nchi yetu... tunapata umeme bure, hatujui kabisa mambo ya Luku kama huko kwenu (Dar es Salaam) wala nini,” anasema Mwatime Ahmad (35), maarufu kwa jina la Mama Salma, mama lishe anayefanya shughuli zake katika eneo la Funguni kisiwani humo.
“Na sasa kila mmoja wetu amekuwa akichangamkia fursa hii ya kupatiwa umeme bure kwa namna anayoijua mwenyewe katika kujiendeleza kiuchumi... mimi ninauza chakula na pia ninauza maji baridi. Maisha yanakwenda vizuri,” anasema Mama Salma.
Hamad ambaye ni dereva wa bodaboda anayefanya shughuli zake katika maeneo ya Gatini, anasema huduma bure wanayopatiwa ya umeme na maji imemsaidia kujiendeleza haraka kiuchumi na anaamini kuwa siku moja na yeye atamiliki pikipiki yake.
“Maji ya kunywa ni gharama sana katika maeneo ya kisiwa kama huku kwetu. Dumu la maji safi (ujazo wa lita 20) linauzwa hadi kwa Sh. 700... lakini sasa tumepunguziwa mzigo kwa sababu maji ya kunywa na kupikia tunapewa bure, umeme bure, wadogo zetu 10 wanasomeshwa bure kila mwaka, ndege tunapanda bure, wagonjwa wanapozidiwa wanasafirishwa bure kwa boti iendayo kasi... tutake nini tena kama siyo kufurahia nafasi kama hii,” anasema.
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Songosongo, Juma Hemed Mchenga, anasema maji wanayopewa bure na PAT hutolewa kwa utaratibu maalum kila siku kuanzia saa 3:00 asubuhi, kwenye vituo vitano vikiwamo vya Stumai, Funguni, Mayungiyungi, Kisunni na Makondeni.
Anasema kila siku hupewa lita 30,000 ambazo hutokana na kubadilishwa kwa maji ya bahari kuwa mazuri ya kunywa kunakofanywa kwa gharama kubwa na PAT, wakiyagawa kwa mgawo na kiasi wanachopata wanaume wasio na wake kikiwa ni dumu mbili huku kaya nyingine zikipata dumu tano hadi saba.
Mjasiriamali Arafa Kessy (27), mvuvi Omar Bin Said (60) na mwendesha pikipiki ya kubeba mizigo (yenye miguu mitatu), Yusuf Suleiman (20) na mwanafunzi wa kidato cha pili, Maisara Yaum (16) ni baadhi ya wakazi wa Songosongo wanaothibitisha kusafirishwa na ndege bure kwenda jijini Dar es Salaam, tena zaidi ya mara moja.
“Mimi nimeshapanda ndege bure zaidi ya mara tatu... mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2008 wakati nilipoamua kwenda Muhimbili (Dar es Salaam) kutibiwa tumbo,” anasema Arafa.
“Mimi nimeshapanda ndege zaidi ya mara sita kwenda Dar es Salaam na Lindi... bila ya kuwapo kwa neema hii ya gesi kisiwani kwetu nisingeota kupanda ndege katika umri wangu huu,” anasema mzee Omar Bin Said.
Diwani wa Kata ya Songosongo, Hassan Swaleh, anasema kuwa kazi waliyo nayo wakazi wake wanaokuwa na safari za kwenda jijini Dar es Salaam ni kujiandikisha tu kwa mtendaji na kupewa barua.
“Wakishapata barua ya uthibitisho kutoka kwa mtendaji wanakuwa wamemaliza kazi... ndege inapokuwapo wanapanda bila masharti na kusafirishwa bure. Wengi wanaifurahia sana huduma hii na nyingine nyingi tunazopata,” anasema Diwani Swaleh.
AFYA, ELIMU
Alipofika kwenye kituo cha afya cha Songosongo, mwandishi aliwakuta wagonjwa kadhaa wakiwa wameketi kwenye masofa kumsubiri daktari. Hiyo ilikuwa ni Jumamosi ya Januari 4, mwaka huu saa 4:22 asubuhi.
Laila Ahmad (24), alikuwa amefika kituoni hapo kwa ajili ya kupata matibabu ya mtoto wake Shadya.
“Kwa kweli kama unavyoona, hapa hatuna tatizo la miundombinu. Isipokuwa watumishi ni wachache sana... hapa tulipo tumekaa kwa muda mrefu tukimsubiri dokta,” anasema Mama Shadya.
Mgonjwa mwingine, Zarina Ali, anaungana na Mama Shadya kuelezea tatizo la watumishi.
“Serikali sasa ifanye utaratibu wa kutuongezea watumishi wa hiki kituo. Tunatumia muda mwingi kusubiri huduma kwa sababu hakuna madaktari wa kutosha... ila jambo zuri ni kuwa mgonjwa anapozidiwa ghafla hupelekwa Kivinje kwa boti iendayo kasi,” anasema Zarina.
Mwandishi wa NIPASHE alibahatika pia kukutana na wanafunzi zaidi ya 10 wanaosomeshwa katika Shule ya Sekondari ya Makongo kwa ufadhili wa PAT.
Falhia Nachide, Aziza Mohamed, Mwanaimani Falakhi, Hamis Saady, Asna Abdallah, Najma Mohamed, Hassan Issa, Sheha Mwinyi, Mwamba Khalid, Ali Hashim, Maisara Yaum na Selemani Ali ni miongoni mwa wanafunzi wanaothibitisha kusomeshwa Makongo kupitia ufadhili wa wawekezaji wa miradi ya gesi kisiwani mwao, PAT.
“Kila mwaka huwa wanachukuliwa wanafunzi 10 waliofanya vizuri zaidi darasa la saba. Tulishafika 40, lakini mwenzetu mmoja alifeli kidato cha pili. Hivi sasa tunaosomeshwa tuko 39. Hawa wawekezaji (PAT) wanatusafirisha bure kutoka hapa Songosongo hadi shuleni Makongo, wanatulipia ada ya bweni ambayo gharama zake kwa mwaka ni zaidi ya Sh. milioni 1.5 na pia wanatununulia vifaa vyote vya shule,” anasema Nachide ambaye hivi sasa yuko kidato cha tatu.
“Jukumu la wanafunzi ni kufaulu kwa kiwango cha juu, wazazi ni kutununulia vitu vidogo na kutupatia pesa za matumizi... hii gesi inatusaidia sana kwa sababu bila ya hivyo, mimi na wengine wengi tusingeota kusoma Dar es Salaam kwa sababu gharama ni kubwa, tena katika shule nzuri ya bweni kama ya Makongo,” anasema Maisara, anayesoma kidato cha pili.
Afisa Mtendaji wa Kata ya Songosongo, Shamte Saidi Bungara, anasema tatizo la watumishi katika kituo chao cha afya wanalijua na hivi sasa wanalitafutia ufumbuzi.
Kuhusiana na elimu, anasema kuwa ufadhili kwa wanafunzi bora 10 umesaidia kuongeza ari ya kusoma kwa watoto wao kwani kila inapobaki miezi minne kabla ya mtihani wa taifa, vijana huwa wanafanya mitihani ya mara kwa mara na matokeo yake, pamoja na yale ya taifa ya darasa la saba, husaidia kupatikana kwa vijana 10 bora wanaofuzu kwenda Makongo.
“Ni mpango mzuri. Hivi sasa vijana wamebadilika. Hawashindi pwani badala yake wanajituma sana kwa sababu kila mmoja hutaka awemo katika kumi bora ili naye akasome Makongo,” anasema Bungara.
“Kwa kweli sisi tunaridhishwa sana na ushirikiano tunaoupata kwa hawa jamaa. Ukiwasema vibaya, wananchi wote hapa Songosongo watakuona mbaya. Tunajua wao wanapata, lakini na sisi pia tunachokipata si haba... wawekezaji katika maeneo mengine nchini waje kujifunza kwetu," anasema Bungara.
Meneja wa PAT katika eneo la mradi wa Songosongo, Andrew Hopper alielezea kufurahishwa kwake na namna wananchi wanavyoridhishwa na ushirikiano wanaoutoa kwao, lakini akakataa kuzungumza zaidi kwa maelezo kuwa yeye si msemaji rasmi wa kampuni yake.
Hata hivyo, kupitia tovuti ya PAT na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), inaonekana kuwa wawekezaji hao wametumia dola za Marekani 455,000 (zaidi ya Sh. milioni 700) kwa kipindi cha kuanzia 2004 hadi Desemba 2012 kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii, ikiwamo ya kugawa maji bure, kusomesha wanafunzi wanaopelekwa Makongo kila mwaka na kuwekeza kwenye miundombinu ya kijamii kama ya afya na elimu.
BEI YA VYAKULA
Karibu nyumba zote Songosongo zina umeme na siyo ajabu kukuta nyingi zikiwa na paa la makuti, lakini nje zina ungo kwa ajili ya kukamatia matangazo ya televisheni na ndani pia kuwa na vifaa ghali kama majokofu. Ni dalili nzuri za kuimarika kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Hata hivyo, changamoto kubwa kwa wakazi wa Songosongo ni bei ya vyakula. Tofauti na hali ilivyo katika vijiji vingi nchini ambako vyakula huuzwa kwa bei ya chini kutokana na kilimo kuwa shughuli kuu ya kiuchumi, bei ya vyakula Songosongo iko juu kama ilivyo katika miji mingi nchini.
“Hapa nafuu yetu iko katika kitoweo cha samaki tu. Ardhi yetu haikubali mazao mengi na hivyo bei ya vyakula iko juu kama mjini,” anasema Selemani Said, mvuvi.
“Kama tungeuziwa umeme, na kama maji ya kupikia na kunywa yasingetolewa bure, hali ingekuwa mbaya sana kwetu... huduma bure za maji na umeme zinasaidia kutupunguzia makali ya maisha na kwa hili, tunaishukuru sana Serikali kwa kutuletea wawekezaji wanaotujali,” anasema Said.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi umebaini kuwa hali ngumu ya usafiri usiotabirika kutoka katika bandari za Kivinje, Njia Nne, Somanga na Masoko pia huchangia kuongeza bei ya vyakula na bidhaa nyingine mbalimbali.
“Boti ya uhakika ni moja tu. Mizigo husafirishwa kwa nauli kubwa kwenye majahazi na wakati mwingine, bahari huchafuka na vitu kibao hutoswa baharini kuokoa maisha ya watu. Hili nalo linachangia kupanda sana kwa bei za bidhaa,” anasema Said.
Baadhi ya bei za vyakula Songosongo ni kama ifuatavyo:
Unga wa sembe kilo Sh. 1,200, kilo ya maharage ya Soya Sh. 2,000 na njano 2,200, sukari kilo Sh. 2,000, nyama kilo Sh. 6,000, maji madogo Sh. 600, mafuta ya kula chupa Sh. 2,000, mafuta ya taa lita Sh. 2,600, pakiti ya chumvi Sh. 200, fungu dogo la nyanya Sh. 300, kitunguu Sh.100, ndimu Sh. 100 na kila vocha ya simu ya Sh. 1,000 huuzwa kwa Sh. 1,200.
Sifa nyingine ya pekee kwa Songosongo ni kutokuwapo kwa kituo chochote cha polisi wala matukio makubwa ya kihalifu.
”Eneo letu siyo kubwa sana na wakazi wengi tunajuana. Pikipiki tunalaza nje. Mtu akiiba atatoka nayo vipi hapa kisiwani bila kujulikana? Pia hatuna daladala wala taksi. Usafiri ni baiskeli na bodaboda tu,” anasema Said.
*Habari hii imekamilika kwa msaada wa TMF
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment