Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Saturday, September 27, 2014

Rasimu Ya Bunge Yapingwa

WAKATI WATU wa kada mbalimbali wakikosoa rasimu iliyoandikwa na Bunge Maalum la Katiba, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema atazungumzia jambo hilo leo.
Akizungumza na NIPASHE jana, Jaji Warioba alisema: “Sijajua kilichoandikwa humo (kwenye rasimu ya Bunge), kwa hiyo siwezi kusema chochote sasa. Kesho (leo), nitakuwa kwenye sherehe za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), njoo nitazungumza.”
Aliongeza: “Na wenzako wengi wamenipigia simu nimewaambia nitazungumza nao kesho.”
DK SEMBOJA
Katika hatua nyingine, Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Semboja Haji alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliandika rasimu na kilichofanywa na Bunge ni kuandika rasimu nyingine na kwamba watakaokuwa na uamuzi wa mwisho ni wananchi.
Alishauri kuwa kwenye kura ya maoni wananchi wanapaswa kupewa nafasi ya kuamua muundo wa Muungano, aidha wa serikali mbili au tatu: “Isingewezekana rasimu ya tume ikapita kama ilivyo,” alisema na kuongeza:
“Katiba ni makubaliano kati ya wananchi na serikali yao…mwanzo ni mwanzo…wananchi watakuwa na nafasi ya kutoa maoni yao kuhusu muundo wa serikali…wawe na sauti ya kusema wanataka serikali ngapi,” alisema Dk Semboja.
Kuhusu madaraka ya Rais, alisema rasimu ya Bunge imeyaweka kwenye mfumo na kwamba ‘angalau tumeanzia mahali’.
Akizungumzia ukomo wa ubunge alisema wananchi wanaweza kuuweka kwa kutomchagua mbunge ambaye hawawakilishi ipasavyo:
“Utaratibu wa kumwondoa mbunge ni mzuri…lakini utekelezaji wake ni mgumu na ni mbaya kwa nchi hasa maskini kama sisi. Watu wanaweza kumwondoa mbunge kwa hila na unajua anayekuwa ameshindwa huwa hakubali…kwa hiyo inaweza kuwa shida…Hivyo kilichofanyika ni sawa” alisema Dk Semboja.
BASHIRU ALLY
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Bashiru Ally alisema mchakato wa Katiba umekufa zamani kinachoendelea ni mchakato kuingiliwa na wanasiasa ambao hawalitakii mema Taifa kuwa na amani:
“Kifupi mchakato wa katiba ulikufa zamani hivi sasa hakuna kinachafanyika…sasa wanaendelea kupaka mafuta ili uonekane unang’aa ni hilo tu,” alisema na kuongeza:
“Haitakuwa busara azimio la Arusha lilikufa kihuni…halafu leo CCM na Muungano ufe huku tukishuhudia wakati ndivyo vimetufikisha hapo tulipo haiwezekani,” alisema Bashiru.
Alisema Tume ya Jaji Warioba ilifanya kazi nzuri ya kukusanya maoni na kuandika rasimu na kwamba kinachofanywa na Bunge ni marudio.
DK BANA
Mhadhiri Mwandamizi wa Sayansi ya Siasa na Utawala wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala, Dk Benson Bana alisema Rasimu ya Bunge haikutoka sana nje ya ile Rasimu ya Tume ya Jaji Warioba.
“Isipokuwa kuna mambo ambayo yameachwa bila sababu ya kueleweka. Kwa mfano kurejesha mamlaka ya uteuzi wa Katibu Mkuu Kiongozi…makatibu wakuu na manaibu wao moja kwa moja kwa Rais bila ya kupitia kamati ya uteuzi siyo kitu mwafaka,” alisema Dk Bana.
Alisema hata kama wametoa ulazima wa kuthibitishwa na Bunge, lakini ilikuwa ni muhimu sana Rais apate majina matatu ya kuteua watu kwenye nyadhifa hizo kutoka kwenye chombo hicho.
Dk Bana alisema hata kitendo cha kuondoa kamati ya makatibu wakuu kama ilivyokuwa imependekezwa kwenye rasimu ya tume haina tija kwa sababu kamati hiyo ingeimarisha uwajibikaji wa utendaji serikalini.
Kuhusu suala la kuondolewa kwa muda maalumu wa wabunge kushikilia nyadhifa hizo…kinyume cha ilivyokuwa imependekezwa na Rasimu ya Tume ya Warioba…Dk Bana alisema hilo nalo si suala jema kwani linakaribisha usultani na umangimeza:
“Ukomo unafaa kuzuia hali ya mtu kujisahau na kuona nafasi hiyo kama ni ya kwake tu na hasa ukichukulia kuwa rushwa imekuwa ikitumika kupata nafasi hizo,” alisema Dk Bana.
PROFESA BAREGU
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mbadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu ameiponda Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na Bunge Maalum, akidai kwamba ‘imetupa maoni ya wananchi’ huku akiwataka Watanzania kukubali mawazo yao yametupwa:
“Nadhani tukubaliane mchakato mzima umevurugika kwa sababu malengo waliyojiwekea Watanzania katika Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba siyo iliyofikiwa na Rasimu iliyowasilishwa juzi na Mwenyekiti wa Kamati ya Uandishi Andrew Chenge…hivyo Rasimu hiyo inakosa uhalali wa kisiasa kwa kuondoa mawazo ya wananchi,” alisema Prof. Baregu.
Alisema Rasimu ya Bunge ambayo pamoja na mambo mengine imeongeza madaraka ya Rais maradufu, haijabeba mapendekezo na matakwa ya wananchi walio wengi isipokuwa matakwa ya watawala.
Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Patrick Ole Sosopi alisema rasimu iliyowasilishwa na Chenge inaonyesha namna ambavyo taifa limepoteza dira ya kisiasa kutokana na mkakati uliosukwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuficha aibu ya kupindua mawazo ya wananchi, ili kuendelea kujinufaisha kisiasa.
Naye, Mtaalam wa Tiba na Afya anayeheshimika Kanda ya Kaskazini, Dk Godwin Mollel alisema Rasimu iliyopendekezwa na Bunge Maalum imepindua mawazo ya wananchi ili watawala wajijengee himaya nyingine ya miaka 50 ijayo bila ya kujali hata familia zao zitakuwa ni sehemu ya watakaolalamika kuhusu ubovu wa Katiba hiyo.
ASKOFU SHAO
Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Martin Shao alisema kilichowasilishwa na Chenge ana wasiwasi kama ndiyo yalikuwa mawazo ya Watanzania na kama yatakubaliwa na walengwa:
“Msimamo wetu ni ule ule uliotolewa na Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) pamoja na ule unaohusu Wakatoliki kwamba Bunge hilo linapaswa kusitisha shughuli zake hadi baada ya uchaguzi mkuu ujao.”
Aliongeza: “Na ndiyo maana nina wasiwasi Rasimu hiyo inayopendekezwa haina maoni ya wananchi ila wanasiasa fulani fulani,” alisema Askofu Shao.
Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari alisema kwa kuwa Rasimu hiyo ya Bunge, imetupilia mbali hata pendekezo la kuwapo kwa Tume ya Walimu nchini ni wazi kwamba Tanzania, imejitoa kwenye ushindani wa elimu katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
CPCT: RASIMU ISIYO NA MAONI YA WANANCHI HATUITAMBUI
Nalo Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), limesema lenyewe lilishakaa na kukubaliana kwamba, rasimu itakayotambuliwa ni ile yenye maoni ya wananchi ambayo yalikusanywa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.
Katibu Mkuu wa CPCT, Mchungaji David Mwasote, alisema wao walishatoa tamko kwamba maoni ya wananchi yaheshimiwe na iwapo rasimu iliyotolewa na Bunge Maalumu la Katiba haina maoni hayo, hawaitambui:
“Sisi tulishatoa tamko kwamba maoni ya wananchi yaheshimiwe…kama maoni ya wananchi hayapo hatuitambui…Tulishatoa maoni yetu kwa Tume ya Warioba…hivyo maoni ya wananchi yaheshimiwe,” alisema Mwasote.
JUKATA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba (Jukata), Deus Kibamba alisema vipengele vilivyowataka viongozi wawaheshimu wananchi vimeondolewa.
Alisema mbunge kuwajibishwa na wananchi na kutokuwa Waziri kama ilivyopendekezwa na rasimu ya Tume ya Warioba imetoa nafasi ya kiongozi huyo kuwa na madaraka mengi zaidi ya moja:
“Kipengele hiki kimetoa fursa kwa Mbunge kufanya anavyotaka iwapo mbunge asipoonekana jimboni na pia kazi ya mbunge ni kuiwajibisha serikali na waziri kazi ni kutumikia wananchi si vinginevyo, ” alisema. Kibamba
Hata hivyo, alisema rasimu ya Bunge Maalum kuondoa kipengele cha kuonyesha ukomo wa ubunge kinatoa nafasi kwa mbunge kuongoza zaidi ya miaka 40:
“Kuna wabunge ambao mwakani katika Uchaguzi Mkuu watakuwa wanatimiza miaka 40 ya kuwa wabunge. Hii si sahihi huo umri ambao mtu anaweza kugombea nafasi ya urais…anaweza kuwa mbunge kwa miaka atakayo,” alisema Kibamba.
Pia, alizungumzia mgombea binafsi wa kiti cha urais kutaja kiasi cha fedha alichonacho ni kuleta kikwazo kwa mgombea kwani hata mgombea asiye binafsi kupitia chama chochote anatakiwa kutaja fedha alizonazo kabla.
Naye Katibu katika Taasisi ya Mfuko wa Vijana wa Kilimo nchini (Tayoaf), Gasper Mahekula alisema maoni ya wananchi yalipaswa kuheshimiwa kutokana na umuhimu wake.
Kuhusu wananchi kutoruhusiwa kumwajibisha mbunge anaposhindwa kutimiza wajibu wake, alisema siyo sahihi kwa kuwa kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakijisahau na kushindwa kutimiza ahadi na wajibu wao baada ya uchaguzi, hivyo kuchangia maendeleo kuchelewa katika majimbo yao.
MWANZA WASHANGAA RASIMU YA CHENGE
Tryphone Cosmas mkazi wa Ilemela, Mwanza alisema kisheria rasimu ya pili iliyowasilishwa na Tume ya Warioba, ndiyo iliyofaa kutumika katika kupata katiba itakayoongoza Tanzania na siyo vinginevyo:
“Hii Rasimu ya Chenge imesheheni mawazo ya watu wachache waliokaa pale Bungeni Dodoma na wala si maoni ya Watanzania waliowengi…wengi walipendekeza Rais apunguziwe madaraka lakini ajabu ameongezewa lukuki,” alisema Cosmas.
Alisema Rasimu ya Chenge imebadili yale yote ambayo yalipendekezwa na wananchi kwa mfano ukomo wa wabunge, na mawaziri kutotokana na ubunge, lakini yote hayo yamekiukwa.
Cosmas alisema rasimu iliyowasilishwa juzi inazidi kuwakandamiza wananchi wa kawaida na kuwapa nguvu viongozi na kumuongezea madaraka Rais, na hivyo mpango wa Tume ya kukusanya maoni ulikuwa mzuri na ulitoa fursa kwa kila mmoja kushiriki.
Naye Leodigald Byabato mkazi wa Mkuyuni, alisema rasimu ya juzi imekiuka maoni ya wengi kuhusu madaraka ya rais na inatoa mwanya mkubwa wa rushwa kwa viongozi wa serikali, upotofu wa nidhamu na utendaji mbovu kwa sababu viongozi wanaoteuliwa na rais hawatalitumikia taifa bali watamtumikia Rais.
Kuhusu suala la muungano, Byabato alisema rasimu ya pili inalinda Muungano ambao siyo ridhaa ya wananchi wote bali ni ridhaa ya viongozi wachache. Aliwataka waige mfano wa Scotland ambayo wananchi wake waliweza kujadiliana na kuafikiana.
Naye, Soweto Michael mkazi wa Mabatini, alisema Watanzania wanahitaji katiba mpya ambayo itapatikana kwa ridhaa ya wananchi wote ikijali maslahi ya mkulima, mfanyabiashara, haki, demokrasia na usawa na siyo katiba kandamizi.
MTANDAO WAPONGEZA
Mtandao wa Wanawake na Katiba umepongeza Bunge Maalum la Katiba kuwezesha kuingizwa masuala ya jinsia katika rasimu mpya ili kujenga nchi isiyo na ubaguzi wa aina yoyote ile ukiwamo wa jinsia.
Mwanaharakati wa Masuala ya Jinsia, Prof Ruth Meena alisema baada ya uchambuzi wa rasimu hiyo iliyosomwa bungeni, usawa wa jinsia umebainishwa kama msingi mmoja wapo wa utawala bora.
ASKOFU ANGLIKANA
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Morogoro, Godfrey Seheba alisema rasimu ya Bunge imekosea kwa kutoweka ukomo kwa wabunge kama ulivyo kwa Rais kuongoza kwa vipindi viwili.
Samuel Msuya, Diwani wa Mbuyuni Manispaa ya Morogoro alisema ameshangazwa na mapendekezo ya Rasimu ya Bunge hilo kwa kushindwa kupitisha mapendekezo ya Jaji Warioba ya nafasi za juu za utumishi wa umma kama ya Jaji Mkuu , Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu (CAG) Katibu Mkuu Kiongozi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) uteuzi wao kuidhinishwa na Bunge kwa kuwa nafasi hizo ni muhimu.
Alisema kuendelea kuruhusu Wabunge kuwa Mawaziri kutasababisha kuendelea kushindwa kuwajibika katika kazi zao.
Mwingine ni Maliki Malupo, Mwenyekiti wa Muungano wa Vyama visivyo vya kiserikali mkoani Morogoro alisema amefurahishwa na Rasimu ya Bunge maalum kuruhusu kipengele cha wanawake kumiliki ardhi.
Issa Saleh, mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Waislamu alisema ameshangazwa na Bunge kumuongezea madaraka Rais badala ya kupunguza.
MAONI KUTOKA TANGA
“Baada ya kutoka nje ya Bunge Wajumbe wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) tulijua kwamba kinachoandaliwa si Katiba ya wananchi bali ni Katiba ya CCM kulingana na mahitaji yao.”
“Haiwezekani mawazo yale ya Watanzania yaliyotolewa na Tume ya Jaji Warioba yawe ni ya kipuuzi kiasi hicho na hata baadhi ya vipengele kutupwa nje kabisa,” alisema Mbaruku Shehe, mfanyabiashara na mkazi wa Tanga.
Mbaruku alisema kitendo cha kuondolewa kwa kipengele cha wananchi kuwa na mamlaka ya kumwajibisha mbunge na mawaziri ni wazi kuwa waliokuwemo wengi ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambao walikuwa wakitetea maslahi yao binafsi:
“Sasa hivi niulize waliokuwamo mule ni wabunge wa bunge la Jamhuri kweli wataacha kutetea maslahi yao wawaangalie Watanzania. Suala lingine lile la serikali mbili si matakwa ya Watanzania walio wengi …sisi tunataka serikali tatu kwa nini wanatulazimisha?” alihoji Shehe.
Naye, Martha Owenyo aliwataka Watanzania kuungana kupinga rasimu hiyo kwa nguvu zote kwani ipo kwa ajili ya kutetea watu wachache na siyo kulinda maslahi ya Watanzania.
Naye, Laurent Joseph alisema kama hawaoni sababu za Mbunge kutakiwa kuwa na sifa ya elimu angalau ile ya kidato cha nne, serikali haina sababu ya kuendelea kujenga shule za kata kwani wangeongeza madarasa ya elimu ya watu wazima ili Watanzania wajue kusoma na kuandika na hatimaye waruhusiwe kuwa viongozi.
MAONI KUTOKA ZANZIBAR
Ramadhan Khalfan, ambaye ni mwanasheria mjini Zanzibar, alisema rasimu iliyowasilishwa na Jaji Warioba ni mapendekezo tu, hivyo yawezekana yakakubaliwa, kurekebishwa, kupitishwa au kukataliwa, siyo kwamba kila kilichowasilishwa katika rasimu hiyo kuwa kila kitu kilipaswa kukubaliwa.
Mchungaji Bunga, Eduwadi wa Kanisa la Sabato Zanzibar, alimpongeza Jaji Warioba na timu yake kwa kuandaa rasimu iliyokuwa na maoni ya wananchi licha ya mambo mengi kufutwa na kuhoji Bunge limetumia kigezo gani cha kubadilisha maoni ya wananchi kuhusu muundo wa serikali.
Suleiman Ali Seif mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar (Suza), alisema rasimu iliyokuwa ikijadiliwa bungeni ilikuwa ya kisiasa zaidi kwani mchakato mzima ulihodhiwa na wanasiasa na hasa chama tawala.
Rais wa Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (Zalefa), Awadhi Ali Said alisema tayari mchakato umeondoka kwa wananchi kwani tume ndiyo iliyopewa mamlaka na Bunge ni kuboresha.
WAJUMBE BMK
Ally Omar Juma, mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba kutoka kundi la 201 kutoka Zanzibar alisema haungi mkono Rasimu hiyo kwa kuwa vimeanzishwa baadhi ya vifungu ambavyo siyo halali kwa mujibu wa sheria na pia inapunguza sana mamlaka ya Zanzibar kama nchi.
Alisema kuanzishwa kwa sura na vifungu vipya vinavyohusu masuala ya ardhi, bahari na rasilimali za baharini kisha kuzifanya kuwa masuala ya Muungano kwake anaona kuwa siyo sahihi, kwa kuwa kabla ya kufanya hivyo ilipaswa kwanza wananchi wa pande zote mbili za Muungano wapewe fursa ya kutoa maoni yao juu ya rasilimali hizo.
Mjumbe mwingine kutoka katika kundi hilo la 201 akiwakilisha watu wenye ulemavu, John Josephat Ndumbaro, pamoja na kuipongeza Rasimu ya Katiba ya tatu iliyowasilishwa bungeni na Chenge, alisema rasimu ya awali ilitoa zaidi kipaumbele katika malengo ya kisiasa na kutoweka mkazo katika masuala ya kiuchumi.
Mjumbe mwingine, Juma Khamis Faki alisema kuwa tofauti iliyopo kati ya rasimu inayopendekezwa na BMK na ile ya Tume ya Mabadiliko ni ndogo, hivyo kwa mtazamo wake ameridhishwa na kazi iliyofanyika mpaka sasa.
Imeandikwa na Raphael Kibiriti, Restuta James, Isaya Kisimbilu, Muhibu Said, Christina Mwakangale, Theonest Bingora, Leonce Zimbandu na Enles Mbegalo, (Dar), Godfrey Mushi, Moshi; Daniel Mkate na Kisiroti Zacharia, Mwanza; Ashton Balaigwa, Morogoro; na Lulu George, Tanga; Rahma Suleiman, Zanzibar na Emmanuel Lengwa, Edita Majura, John Ngunge na Jacqueline Massano, Dodoma.
CHANZO: GAZETI LA NIPASHE

No comments :

Post a Comment