Kinana amvaa Sefue.
9th March 2015
Kinana alitoa ombi hilo katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Dodoma juzi jioni ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kuimarisha chama hicho na kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi.
“Mimi ninamuomba na kumshauri Katibu Mkuu Kiongozi awaweke kando watumishi wote wa serikali wanaohusishwa na sakata la Escrow hadi tuhuma zao zitakapokwisha, kama ilivyofanya CCM kuwaweka kando watu wake,” alisema Kinana.
Kinana alikuwa anamaanisha kusimamishwa kwa Mbunge wa Bariadi , Andrew Chenge; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka kuhudhuria vikao vya Halmashuri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kutokana na kuguswa na kashfa hiyo. Tibaujuka pia amesimamishwa ujumbe wa Kamati Kuu (CC) ya CCM.
Chenge na Prof. Tibaijuka wanadaiwa kupokea Sh. bilioni 1.6 kila mmoja wakati Ngeleja Sh. milioni 40.
Chenge na Prof. Tibaijuka wanadaiwa kupokea Sh. bilioni 1.6 kila mmoja wakati Ngeleja Sh. milioni 40.
Kinana alisema haiwezekani watu wanaotuhumiwa kwenye sakata la hilo kuendelea kuwapo ofisini wamekalia viti hivyo, hivyo ni vema wakae kando.
“Kuna watu wametajwa kwenye Escrow, wana CCM waliotajwa tumewaambia kaeni kando, wabunge waliotajwa tumewaambia kaeni kando, nataka nimuombe katibu Mkuu Kiongozi watendaji wa serikali wanaohojiwa na vyombo vya serikali na yeye awaambie kwa sasa wakae kando,” alisema.
“Ndiyo, kuna watu wamehojiwa juzi, unahojiwaje kwa jambo baya halafu unakaa pale pale ofisini, mtu ana kesi kama ukiwa na kesi ya ajali umemgonga mtu, ukiwa na kesi ya trafiki, ajali inaeleweka,” alieleza Kinana na kuongeza:
“Ukiwa umeingia kwenye masuala yanayohusu mambo ya fedha yanayohusiana na uadilifu ukatuhumiwa, wakati unahojiwa, unachunguzwa kaa kando.”
Katibu huyo alisema lazima watu wawajibishwe kwani nchi ni ya Watanzania wote na si ya watu walioko madarakani.
“Mimi nataka nimuombe Katibu Mkuu Kiongozi, maana hawa waandishi wa habari bwana wasije wakaandika kuwa Katibu Mkuu CCM amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, mimi sina mamlaka hayo, mwenye mamlaka ni rais, ila mimi namshauri tu,” aliongeza.
“CCM tumewaweka kando wabunge, kwa serikali mwenye mamlaka ni yeye, inabidi awaweke kando mpaka migogoro ya Escrow iishe, ndiyo kama hutaki kuwekwa kando jihadhari na kama hutaki kuwekwa kando usipokee pokee, kama hutaki kuwekwa kando acha, kazi unataka na nini unataka,” alisema Kinana.
Hata hivyo, alisema watu wanabishana katika jambo la kawaida ambalo mtu amechomoa fedha bado anang’ang’ania na hataki kung’oka.
“Mtu amechomoa fedha hataki kuomba msamaha na kuaga bye bye (kwaheri), mimi nimeharibikiwa bwana naomba kuachia ngazi, badala yake wanatafuta utetezi, unaambiwa toka bwana, unasema siondoki, unaondolewa unalalamika,” alisema Kinana.
Alisema siku hizi umeanza utamaduni mbaya nchini wa kuwatetea wezi halafu wanakusanya kikundi cha watu wa kuwatetea.
“Kinajitokeza kikundi cha watu cha kumtetea eti huyu bwana hivi, anakubalika kwa watu msifanye hivi, kama ulikuwa unajua hivyo kwanini ufanye hivyo. Siku hizi mtu anakosea kisha anaporudi nyumbani kwao anapokelewa kwa sherehe, jambo hili si sawa,” alisema na kusisitiza kuwa:
“Lazima Watanzania wakuamini kwa kauli, kwa vitendo, kwa tabia njema.”
Alisema waliohusika kwenye Escrow wakae kando na iwapo tuhuma dhidi yao hazitakuwa na ukweli wataendelea na kazi na kama watabainika kuwa na makosa hatua nyingine zifuate.
WATUMISHI WA UMMA WANAOTUHUMIWA
Watumishi wa umma wanaotajwa kupokea mgawo wa Tegeta Escrow ni Mnikulu, Shaban Gurumo, anayedaiwa kupokea Sh. milioni 80; Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufilisi na Udhamini (Rita), Philip Saliboko, anatuhumiwa kupata mgawo wa Sh. milioni 40 na Naibu Kamishna Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Loicy Appollo.
Wengine ni Jaji Aloysius Mujulizi anayedaiwa kupata mgawo wa Sh. milioni 40.4 na Jaji Prof. John Eudes Ruhangisa, anayedaiwa kupata mgawo wa Sh. milioni 400.25.
Wamo pia Mkurugenzi wa Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Julius Angello; Meneja wa Misamaha ya Kodi wa TRA, Kyabukoba Mutabingwa; Mhandisi Mkuu wa Mradi wa Umeme Vijijini (Rea), Theophillo Bwakea na Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma.
Wote wanadaiwa kupokea mgawo huo kutoka kwa mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering and Marketing Ltd, James Rugemalira ambaye kampuni yake ilikuwa mwanahisa katika Kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL) kwa kumiliki asilimia 30.Mtumishi pekee ambaye alisimamishwa kazi na Katibu Mkuu Kiongozi ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, kupisha uchunguzi dhidi yake wakati aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alijiuzulu.
Wakati CCM ikichukua hatua ya kuwaweka kando makada wake, Bunge la Jamhuri ya Muuungano nalo liliwavua Chenge na Ngeleja uenyekiti wa kamati za kudumu za Bunge za Bajeti na Katiba, Sheria na Utawala kutokana na kashfa hiyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment