Rais Jakaya Kikwete (pichani) amesema serikali ya awamu yake inajivunia mafanikio iliyoyapata tangu kuingia madarakani mwaka 2005 na kuweka msingi imara wa nchi katika kutekeleza Mkakati wa Maendeleo wa Mwaka 2025.
Mkakati huo unalenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Washington DC juzi wakati akitoa mhadhara katika Kituo cha Kimataifa cha Woodrow Wilson.
"Naamini mrithi wangu atayaendeleza na kujifunza kutokana na mafanikio haya na kuendeleza kutoka pale tutakapoachia," alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa pia anatarajia kwamba Tanzania itakuwa na sera na sheria ya kusimamia gesi na mapato yake kwa vile inatarajiwa kuanza kupatikana ifikapo mwaka 2020.
Katika mhadhara huo uliohudhuriwa na watu mbalimbali wakiwamo Mabalozi, wasomi na viongozi wa taasisi hiyo, Rais Kikwete alilezea mafanikio na changamoto katika uongozi wake wa miaka 10 katika elimu, siasa, uchumi na maendeleo ya jamii."Najivunia kuendelea kuliweka Taifa katika hali ya umoja pamoja na changamoto zote, tumepambana na vitisho pale vilipojitokeza na pia tumetoa mchango mkubwa katika harakati za kisiasa zilizofanya vyama viwili kutiliana saini maridhiano na kupata muafaka mwaka 2010," alisema.
Rais Kiwete alisema makubaliano hayo yaliiwezesha Zanzibar kufanya uchaguzi kwa amani na kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baina ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF).
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment