Waalimu wakipita mbele ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa Mkoani Mwanza.
- Kauli hiyo aliitoa wakati akihutubia kwenye sherehe za Siku ya wafanyakazi Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani hapa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Mwanza. Wafanyakazi jana walimsomea Rais Jakaya Kiwete madai 11 wanayomtaka awatimizie kabla ya kumaliza muda wake Oktoba, lakini mkuu huyo wa nchi amesema ataishia pale atakapoweza na kumuachia mrithi wake kazi ya kushughulikia mengine.
Kauli hiyo aliitoa wakati akihutubia kwenye sherehe za Siku ya wafanyakazi Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani hapa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Rais alikuwa akijibu hoja kadhaa zilizokuwapo kwenye risala ya Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta)iliyosomwa na katibu wake mkuu, Nicholaus Mgaya ambayo ilitaja madaio hayo, yakiwamo ya kuongeza kima cha chini cha mshahara hadi kufikia Sh315,000, kupunguza kodi ya malipo kadri unavyopata na kuundwa kwa Tume ya Usuluhishi.
“Tuna madai 11 ambayo ni kima cha chini cha mishahara, maboresho ya pensheni, makato ya kodi, Tume ya Usuluhishi ambayo bado ina changamoto kubwa kwani sheria inasema suluhisho kati ya mwajiri na wafanyakazi linatakiwa kufanyiwa kazi ndani ya siku 30, lakini kwa sasa inafikia mwaka mmoja, na uhuru wa kujiunga kwenye vyama vya wafanyakazi na mengine ambayo ni changamoto kwa wafanyakazi. Tunaomba utusaidie kuyatafutia ufumbuzi,” alisema Mgaya katika risala hiyo.
Lakini, Rais Kikwete, ambaye jana alizungumza akichanganya na utani, alisema changamoto za wafanyakazi amezikuta na haziwezi kumalizika, hivyo anamwachia Rais ajaye azishughulikie.
“(Rais wa Serikali ya Awamu ya Kwanza) Mwalimu Julius Nyerere kwa miaka 27 alishindwa kuzimaliza (changamoto za wafanyakazi). Rais wa awamu ya Pili, All Hassan Mwinyi hakuzimaliza, Rais wa awamu tatu Benjamini Mkapa hakuzimaliza, na mimi siwezi kuzimaliza. Hivyo zitakazobaki nikitoka madarakani, ninamwachia Rais ajaye azishughulike,” alisema Kikwete.
Wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Kwanza na ya Pili, wafanyakazi walikuwa wakitarajia kusikia nyongeza ya mishahara kutoka kwa Rais kwenye sherehe za Mei Mosi, lakini Mkapa akaondoa utamaduni huo baada ya kueleza waziwazi kwenye moja ya sherehe hizo kuwa Serikali itaongeza mshahara kama watu watachapa kazi.
Kikwete alitumia muda mwingi wa hotuba yake kuaga na akaeleza kuwa hana mpango wa kuongeza muda kama baadhi ya wanasiasa wanavyodai.
“Nawashangaa wanaodai kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza muda wa urais, kwani sina mpango wa kufanya hivyo,” aliongeza Kikwete ambaye aliingia Ikulu mwaka 2010 kwa ushindi wa zaidi ya asilimia 80. .
“Kwanza naomba niwashukuru wafanyakazi wote kwa kukutana tena Mwanza. Wakati naanza urais mwaka 2006 sherehe zangu za kwanza za Mei Mosi zilifanyika Mwanza, na furaha kubwa sherehe za mwisho tena nafanyia Mwanza. Katika kipindi changu cha uongozi nimefanya mambo mengi kushugulikia changamoto za wafanyakazi.”
Bango la walimu lamkuna JK
Rais pia hakusita kueleza jinsi alivyokunwa na ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye mabango ya vikundi kadhaa vilivyopita mbele yake mwanzoni mwa sherehe hizo, hasa bango la walimu lililokuwa na ujumbe usemao “shemeji unatuachaje”.
“Nimesoma ujumbe wenu kupitia mabango. Niwaambie kwamba ujumbe umefika na yote nitayafanyia kazi… hata ule wa shemeji zangu pia,” alisema Rais Kikwete huku akicheka na kuingiza utani akisema “kuoa mwalimu kazi”.
Akizungumzia suala la kupunguza kodi kwa mishahara ya watumishi wa umma kutoka asilimia 12, hadi tisa, Rais Kikwete alisema ataliangalia suala hilo hata kama haitafikia asilimia hiyo mrithi wake anaweza kufikia huko.
Madai ya walimu
Akizunguzmia madai ya walimu na wauguzi kuhusu malipo ya stahiki zao, Rais Kikwete alisema Serikali imeanza kulipa malimbikizo ya madeni ya walimu na kwamba tayari kuna baadhi wameshanza kulipwa.
Kauli mbiu ya Mei Mosi
Kuhusu kauli mbiu ya Mei Mosi mwaka huu, Rais Kikwete alisema kuwa kauli mbiu hiyo ni sahii kipindi hiki cha Uchaguzi Mkuu na kwamba wafanyakazi wajitokeze kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura ili waweze kuchagua kiongozi wanaomtaka na kupata nafasi ya kuipigia kura Katiba Inayopendekezwa.
“Mfanyakazi kajiandikishe, kura yako ina thamani kwa maendeleo yetu. Hii ni kaulimbiu sahii kwa kipindi hiki. Mkijiandikisha mtaweza kupiga kura na kuchagua madiwani, wabunge na Rais ambaye atawatetea,” alisema.
“Mtambue kuwa kitambulisho cha zamani hakitatumika tena kupigia kura, hivyo mjitokeze kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura,” alisema Rais Kikwete.
Vibali vya ajira kwa wageni
Kuhusu ongezeko la utoaji holela wa vibali vya kazi kwa wageni, Rais alimtaka Waziri wa Kazi na Ajira kuandaa kanuni zitakazoratibu utekelezwaji wa sheria mpya ya vibali vya ajira ili ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.
Alisema tayari Bunge limeshapitisha sheria hiyo itakayoangalia kwa kina vibali vya ajira kwa raia wa kigeni na kinachosubiriwa kwa sasa ni kuanza utekelezaji.
“Kumekuwepo na malalamiko kadhaa kuhusu wageni wanaokuja kufanya kazi katika sekta mbalimbali nchini, hasa katika maeneo ambayo hata Watanzania wana ujuzi nayo. Tumeliona hilo tayari limeshatungiwa sheria kinachosuburiwa kwa sasa ni kanuni ili utekelezaji wake uanze mapema iwezekanavyo”alisema
Rais pia alizungumzia changamoto ya mawakala wa ajira na kuwalezea kuwa baadhi yao wamekuwa kiini cha kuwakandamiza wafanyakazi, hali inayosababisha kukosa stahili zao za msingi.
Alisema Serikali haitasita kuwachukulia hatua stahiki mawakala wa ajira wanaokiuka sheria za kazi na ajira ikiwa ni pamoja na kujivika joho la waajiri na kukodisha wafanyakazi kwenye makampuni.
Kikwete aibukia kwenye Bongo Fleva:
Rais Kikwete pia hakusita kuburudisha wananchi waliohudhuria sherehe hizo baada ya kujisifu kuwa ana kipaji cha uimbaji alichokionyesha kwa kuimba sehemu ya wimbo wa bendi ya Orchestra Safari Sound wa “Mimi Msafiri”, akisema kama asingekuwa Rais, angeweza kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya.
Kama vile anaelezea maisha yake yataendelea hata baada ya kuondoka Ikulu, Rais aliimba kipande cha wimbo huo kisemacho “Mimi msafiri msafiri bado nipo njiani, sijui lini nitafika”.
“Nafikiri nisingekuwa rais ningekuwa msanii wa bongo fleva kwani sauti yangu sio mbaya sana japo siwezi kuwashinda wasanii kama Ali Kiba na Diamond,”alisema Kikwete Wimbo huo ulitungwa na kuimbwa na mwimbaji nguli kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kikumbi Mwanza, maarufu kwa jina la King Kiki, ambaye pia ametunga wimbo unaomsifu Kikwete.
Ujumbe wa Tucta
Akizungumza kwenye sherehe hizo katibu mkuu wa Tucta alisema kuwa kabla Rais hajamaliza muda wake, wanatarajia kuwa ataendelea kuwahimiza waajiri wa sekta ya umma wawalipe wafanyakazi wao kima cha chini walichopendekeza mwaka 2006 ambacho ni Sh315,000.
Pia alisema wanaomba kodi wanayokatwa wafanyakazi ipunguzwe hadi kufikia asilimia tisa pamoja na kuridhia mikataba ya Shirika la Kazi Duniani (ILO).
“Bado kuna changamoto kubwa kwa wafanyakazi wa sekta za umma na binafsi, lakini tunatarajia kabla hujamaliza muda wako utatusaidia kupunguza kodi hadi kufikia asilimia tisa, kuridhiwa kwa mikataba ya Hifadhi ya Uzazi namba 183 na mkataba wa 155,” alisema Mgaya.
Hali ilivyokuwa
Baadhi ya washiriki wa sherehe hizo za Mei Mosi zilizofanyika Uwanja wa CCM Kirumba walizuiliwa kuingia uwanjani kutokana ujumbe wa mabango yao.
Washiriki hao walisababisha mshangao kwa wananchi waliokuwa wamehudhuria sherehe hizo kutokana na ujumbe uliokuwa umeandikwa kwenye mabango waliyobeba.
Baadhi ya mabango hayo ni pamoja na ujumbe wa Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu, wamachinga yaliyokuwa na ujumbe unaosomeka “Katiba Pendekezwa ni Haki ya Kila Mmoja , Isome na Uielewa na Uipigie Kura ya Ndio, Akili za Kuambiwa Changanya na Zako”.
Dodoma
Mkoani Dodoma, Tucta iliishambulia Serikali kwa kitendo chake cha kuwalipa mishahara midogo ambayo ni sawa na posho ya siku moja kwa baadhi ya viongozi wa Serikali na taasisi zake.
Akisoma risala ya mkoa katika maadhimisho yaliyofanyika Uwanja wa Jamhuri, mratibu wa Tucta, Ramadhan Mwendwa alisema: “Kipato cha ujira wa mishahara wa mwezi tunacholipwa wafanyakazi hakiridhishi kabisa kwa sababu ujira huo ni sawa na posho ya siku moja ya kikao cha baadhi ya viongozi wa serikali na taasisi zake.”
Huku akishangiliwa na wafanyakazi, alisema malipo hayo kidogo athari yake ni kukosekana kwa tija kazini kwani wafanyakazi hutumia muda wa kazi kutafuta njia nyingine ya kujiongezea kipato.
Alisema wafanyakazi wengi hutumia mishahara yao kwa sijy saba tu.
“Wafanyakazi tunaamini kuwa serikali ina uwezo wa kulipa kiwango hicho cha mishahara tulichopendekeza cha Sh315,000 kutokana na rasilimali tulizonazo kama kama ipo dhamira ya dhati,” alisema.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa, ambaye alikuwa mgeni rasmi, aliwataka wafanyakazi kutofanya kazi kwa mazoea na badala yake kufanya kazi kwa bidii, kuwa wabunifu na waadilifu ili kuongeza tija.
Geita.
Mkoani Geita, Tucta iliitaka serikali kutatua kero za wafanyakazi yakiwemo madeni ya watumishi, kuimarishwa kwa vikao vya mabaraza ya wafanyakazi na kudhibiti upandaji wa bei za bidhaa.
Akizungumza kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kalangalala, mratibu wa shirikisho hilo, James Kimola alisema endapo changamoto hizo hazitatatuliwa, shirikisho litaishtaki mahakamani serikali ya mkoa.
Kimola alisema moja ya maeneo yanayosumbua wafanyakazi ni mabaraza ya wafanyakzi kuchukuliwa kama jambo la dharula na lisilokuwa na umuhimu wowote, kutokana na mabaraza hayo kutoitishwa na wakurugenzi karibu halmshauri zote, na yanapoitishwa wajumbe hawalipwi stahili za vikao hivyo.
Alisema kutoitishwa kwa mabaraza hayo ambayo ni chombo cha muhimu cha kumshauri mwajiri, kumesababisha wafanyakazi kushindwa kujadili changamoto zinazowakabili.
“Wafanyakazi kutolipwa fedha za uhamisho wanapopewa uhamisho, hususani walimu, baadhi yao wanapodai gharama za uhamisho huambulia vitisho na hata hufunguliwa mashtaka ya kusingiziwa. Hali hii haiwezi kuvumiliwa hata kidogo. Tunaomba serikali ichukue hatua madhubuti kwa waajiri wanaoendelea kuwahamisha watumishi huku wakijua hawana fedha,” alisema Kimalo.
Ruvuma
Mkoani Ruvuma, mkuu wa mkoa, Said Mwambungu amesema Serikali haitawafumbia macho waajiri wanaowatoa vitisho, lugha chafu na masimango yasiyokuwa na ukomo kwa watumishi wao kwa kuwa ni unyanyasaji.
Akizungumza kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea, Mwambungu alisema waajiri na waajiriwa wanapaswa kuheshimiana badala ya kutoleana vitisho ambavyo havina tija.
Alisema, waajiri watambue na kukubali kuwa ufanisi katika sehemu za kazi hutegemea uhusiano mzuri uliopo kati ya mwajiri na mwajiriwa, hivyo lugha za mwajiri zinapaswa kuwa nzuri kwa wafanyakazi wao.
Tanga
Wafanyakazi wa Mkoani Tanga jana waliadhimisha siku ya Mei Mosi kwa kuiomba Serikali kufanyia kazi ipasavyo changamoto iliyopo ya viwanda muhimu kufa au kuhamishiwa nje ya nchi na mikoa mingine.
Mratibu wa mkoa, Ahmed Ngereza alisema jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani Jijini hapa kuwa kufa kwa viwanda muhimu vilivyokuwa vikitoa ajira kwa idadi kubwa ya wakazi wa Tanga na vingine kuhamishiwa mikoa mingine kumeathiri maisha ya wakazi.
Alisema licha ya kwamba jitihada zimeanza kuchukuliwa kwa kuandaa maeneo na kulipa fidia kwa waliotakiwa kupisha ujenzi wa Bandari ya tanga, bado kuna kusuasua.
Kilimanjaro
Mkoani Kilimanjaro, Tucta imewataka waajiri kuboresha mazingira ya watumishi ili waweze kuondokana na hali duni ya maisha inayosababisha kuwa wajasiriamali na hivyo ufanisi kupungua.
Kaimu Mwenyekiti wa Tucta mkoani Kilimanjaro, Alan Mbwambo alisema kwenye sherehe za Mei Mosi zilizofanyika Uwanja vya Ushirika, kuwa mishahara duni imesababisha wafanyakazi wengi kufanya shughuli za kujipatia fedha tofauti na ajira zao.
“Kilio kikubwa kwa wafanyakazi ni mishahara midogo ni vyema waajiri wangeongeza viwango vya mishahara kwa wafanyakazi, ili waweze kuondokana na hali duni za maisha,” alisema Mbwambo.
Mbeya
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro amewataka Watanzania kuacha tabia ya kuukumbatia uduni na ukabila kwani kufanya hivyo kutaliingiza Taifa katika vita isiyokuwa na tija.
Akihutubia katika sherehe za Mei Mosi zilizofanyika kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, alisema hivi sasa kuna viashiria vya ukabila na udini, jambo ambalo alisema ni hatari kwa mustakabali wa Taifa na kutaka kila mmoja kuheshimu dini na imani ya mwenzake.
“Tuheshimiane, udini tusiukumbatie, ukabila hauna nafasi katika dunia ya leo. Masuala ya ukabila yanahusiana na matambiko tu lakini sio kuingiza katika jamii hivyo tusithubutu kuligawana Taifa kwa misingi ya udini na ukabila kwani hivyo vilishapitwa na wakati,” alisema Kandoro.
Awali, risala ya Tucta iliyosomwa na katibu wa Tamico, Tabia Mwanjetile iliilaimikia Serikali kwamba watumishi wamekuwa wakitozwa kodi kubwa katika mishahara yao huku ikiwaachia wafanyabiashara ambao wamekuwa vinara wa kukwepa kulipa kodi.
Dar es Salaam
Sherehe za Mkoa wa Dar es Salaam zilizofanyika, Uwanja wa Uhuru, Mratibu wa Mei Mosi, Mkoa wa Dar es Salaam, Charles Ngasha alitaja maombi yao kwa sasa kuwa ni nyongeza ya kipato cha mshahara kutoka makadirio ya chini ya Sh100,000-150,000 hadi Sh720,000 kutokana na mazingira ya hali ya uchumi kwa sasa.
“Lakini pia, tunaomba Sheria ya Ajira iwalazimishe waajiri kutambua vyama vya wafanyakazi katika ofisi za mashirika na kampuni binafsi. Wafanyakazi wanaopandishwa vyeo waharakishiwe kuongezwa mishahara, malipo ya madeni ya likizo, uhamisho na changamoto za walimu zishughulikiwe,” alisema Ngasha.
Akijibu madai hayo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadick alikiri madai hayo kuwa ya msingi na kwamba atamfikia rais ambaye ni mkuu wa nchi ili aweze kuyashughulikia.
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila ameamua kuichongea CCM kwa wafanyakazi, akidai kwamba chama hicho tawala kinawakandamiza kwa kuwabebesha mzigo wa kodi na kwamba kinajali maslahi ya wafanyabiashara wakubwa.
Alisema licha ya asili ya CCM kuwa inatokana na harakati za wafanyakazi na wakulima wadogo kama bendera yake inavyoonyesha nyundo na jembe, chama hicho kimewatelekeza.
“Hivyo ni aibu kwa chama kilichoasisiwa na wafanyakazi leo kinaongoza kwa kunyonya wafanyakazi kwa kodi kubwa kuliko nchi yoyote Afrika Mashariki,” alisema.
Aliwashauri wafanyakazi waiombe CCM iondoe alama ya nyundo kwenye bendera yake kwa kuwa ni kejeli kwao,kwani chama hicho kwa sasa kipo kwa maslahi ya wafanyabishara wakubwa.
“Hao ndio wanafaidi uchumi kwa misamaha ya kodi na ukwepaji mkubwa. Ni maoni yangu kwamba kodi ya mshahara inapaswa kushuka kwa 50, itoke asilimia 18 hadi 9% wastani wa kuanzia,” alisema Kafilila.
Sharon Sauwa, Elizabeth EdwardSalum Maige, Kelvin Matandiko, Joyce Joliga, Buruhan Yakub, Fina Lyimo, Albert Msole Hadija Jumanne, Aidan Mhando Justa Mussa na Beatrice Mosses na Ngollo John.
No comments :
Post a Comment