zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, July 19, 2015

Kwa nini haikuwa Jaji Ramadhani? Lula wa Ndali Mwananzela


Na Lula Wa Ndali Mwananzela
KUNA
swali linahitaji kujibiwa na ninaamini linastahili kujibiwa. Katika ya majina yote yaliyokatwa katika mchakato wa kumtafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM uliomalizika mwishoni mwa juma huko Dodoma. Swali hili ni kwa nini jina la Jaji Augustino Ramadhani ambao baadhi yetu tuliamini kuwa alikuwa ndiye mgombea pekee anayekuja na sifa ya usafi na asiyechafuliwa na historia ya CCM. Kwamba, iliwezekana vipi mtu kama yeye ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kushindwa hata kuingia kundi la tano bora na kupitwa hata na Januari Makamba ambaye wadhifa pekee mkubwa aliowahi kuushika ni Unaibu Waziri au kupitwa na Amina Salum Ali ambaye kwa miaka hii ya karibuni alikuwa hasikiki kwani alikuwa akiwakilisha Jumuiya ya Afrika huko Marekani (Umoja wa Mataifa na kwa Taifa la Marekani). Ni wazi yapo maswali mengine yanayowahusu wagombea wengine waliokatwa mapema. Nina uhakika tukiuliza kwa mfano kwa nini Mbunge wa Monduli alikatwa mapema majibu yanaweza kuwa mengi kama vile watoaji wa majibu hayo watakavyokuwa. Wapo ambao wanaweza kusema tatizo ni Kikwete, wengine wanaweza kumtaja Membe, na wengine wanaweza kutaja lolote lile ilimradi kuonesha kwa nini Lowassa alikatwa.Hata ukitaka kujua ilikuwa watu kama Mwandosya aliyekuwa tatu bora miaka kumi iliyopita aliwekwa pembeni au imekuwa mzee wa viwango naye akafyekwa. Unaweza ukashindwa hata pa kuanza ukitaka kujua Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Kayanza Peter Pinda na Makamu wa Rais wa Sasa Bilal nao walikatwa hata tano bora hawakuingia na wao wakapitwa na Naibu Waziri! CCM ina mambo lakini mambo mengine hata ukianza kuyatafutia maelezo utajikuta ukubali tu – CCM wana mambo. Lakini hawa wengine binafsi naweza kutafuta sababu mbalimbali za kuwakata – za ukweli na za kuwasingizia. Lakini ni huyu aliyekuwa Jaji Mkuu aliweza vipi kufyekwa kabla hata hajakanyaga ardhini. Hapa labda kuna swali jingine kwanza linahitaji kujibiwa na yeye mwenyewe au watu wake wa karibu. Ni nani Alimshawishi Jaji Augustino Ramadhani Kuchukua Fomu? Tetesi zilikuwepo kwa muda kuwa kuna watu kweli wanataka Jaji Ramadhani achukue fomu. Na alipochukua fomu hata gazeti lako hili (ambalo liliziandika baadhi ya tetesi hizo huko nyuma) lilimuweka kwenye kurasa za mbele kuwa anaweza kuwemo pamoja na Membe na Magufuli. Membe na Magufuli walikuwemo tano bora Jaji Ramadhani hakuwepo. Lakini hatujui hasa ni kina nani na kwa nini walimfuata Jaji huyu aliyejijengea heshima kwa muda tu kuwa ni mtu msafi na mwadilifu kuchukua fomu ndani ya CCM chama ambacho kisheria alitakiwa asiwe mwanachama wake kwa muda wote aliokuwa anatumikia Mhimili wa Mahakama – baada ya kurejea kwa mfumo wa vyama vingi. Ni kitu gani watu hawa walimwambia Jaji huyo kiasi cha kumfanya na akili zake zote akiongozwa na maongozi yote ya kiroho aliyokuwa nayo kama kasisi kwenda kufufua uanachama wake (kama kweli ulikuwa umekufa). Hatujui kama alichukua kadi mpya pale alipoacha Ujaji au alienda kutafuta kadi yake ya zamani na kuilipia tena. Vyovyote vile waliomfuata na kumwambia kuna kitu walimwambia ambacho kiliondoa vizingiti vyote vya kiakili moyoni mwake. Na tukumbuke kuwa hawa waliomfuata kimantiki kabisa hawawezi kuwa watu wa chini kama akina siye pangu pakavu tia mchuzi. Ni lazima watakuwa ni watu wazito, watu wenye sauti na watu ambao wakipiga simu ni lazima mtu kama Jaji apokee yeye mwenyewe. Ni lazima watu wawe kwenye nafasi za juu wao wenyewe na wawe na ahadi za kutosha kumfanya aamini kuwa yeye akifanya upande wake na wao watafanya la upande wao – kuhakikisha anapita hadi dakika ya mwisho. Na alipochukua kadi baadhi yetu tuliona kuwa hatimaye mchakato mzima umempata mtu ambaye ni vigumu kusema ana makundi, au amefanya kampeni chafu huko nyuma. Jina lake lilipotajwa ukiondoa tatizo la kuwa yeye alikuwa Jaji muda mrefu ambao sisi wengine tumekuwa tukihangaika na CCM kumbe mwenzetu kimoyo moyo akijifungia ndani anachukua chetezo na kufukiza ubani kwenye altare ya CCM! Kuna kitu aliambiwa, kikamshawishi, na akaamua kujitokeza na shati lake la kijani kuchukua fomu. Kitu hiki ni vigumu kukijua lakini tunachojua ni kuwa hakikutosha hata kumuingiza tano bora. Yaani pamoja vyote alivyoambiwa kwenye Kamati Kuu peke yake hakuwa na sapoti ya kutosha kumfanya wamfikirie hata kumpa nafasi ya kwenda mbele ya NEC – chombo ambacho sijui kama amewahi hata kuhudhuria (labda akiwa mgeni mwalikwa). Mchujo wa awali ulimuondoa. Ndio maana swali letu limebakia; imekuwaje walimkata? Naomba kupendekeza majibu kadhaa. Kwanza, kosa kubwa naamini tulilifanya sisi waandishi na wachambuzi ambao tulimfikiria kuwa angeweza kupitishwa hata kuwa mgombea wa CCM. Kosa hili lilitokana na kudhania vibaya (bad assumption). Tulidhani – angalau nikijisemea mimi mwenyewe – nilidhania kuwa CCM hatimaye wameelewa tatizo lao na sasa wako tayari kuanza kujisafisha. Nilidhania kuwa CCM baada ya kuchafuka na kashfa mbalimbali za ufisadi miaka ya utawala wa Mkapa na Kikwete hatimaye waliamua kuanza upya. Kwamba waliomfuata kumtoa Jaji huko aliko walikuwa wanafikiria kumleta mtu ambaye ataweza kusafisha chama hasa ukizingatia wasifu wake katika medani ya kupata haki. Nilidhania kuwa CCM watamtaka mtu ambaye hawezi kuhusishwa na ufisadi hata kwa mbali. Lakini pia nilidhania kuwa mtu huyu – Jaji Ramadhani – atapitishwa kwa sababu hawezi kutajwa kuwa ni zao la mfumo huu huu. Wagombea wengine wote 37 walikuwa kwa namna mbalimbali ni watumishi wa chama hicho hicho kwa muda mrefu au wamekuwa wakivuna mavuno yao kwenye shamba lao la CCM. Kuanzia Amina Salum Ali hadi yule Mwanakijiji wa Kigoma wote walikuwa ni mazao ya CCM isipokuwa Jaji Ramadhani. Naamini hapa ndipo lilipo jibu hasa. Kwamba, CCM walilikata jina lake kwa sababu hizo hizo ambazo miye nilijengea dhana zangu. Kwamba, hawakuwa tayari kuanza upya na mtu msafi wasiyemjua. Waliamua kwenda na watu “wao” ambao angalau wanawajua. Augustino angesema “anauchukia ufisadi” CCM wengine wangeanza kupagawa kwa sababu wasingejua kama ni mwanasiasa anazungumza au Jaji anazungumza. Lakini Magufuli akisema “nachukia ufisadi” wenyewe wanajuana! “Mwenzetu huyu” Walilifuta jina lake kwa sababu Jaji Ramadhani siyo mwenzao. Ni kama mtoto ambaye hapendi kucheza mpira na wenziwe. Kila akipewa pasi anataka kucheza yeye hadi goli. Wanaweza kumnyima mpira lakini rahisi zaidi ni kutokumpanga kwenye timu. Jaji Ramadhani hakutakiwa hata kuwemo kwenye hii timu – asingecheza mpira na wenzake. Hili lilikuwa ni tishio. Lakini pia ni kuwa huko ndani ya CCM hawakuwa wanamjua kuwa na yeye ni mwana CCM mwenzao. Magufuli na hao wengine wanajulikana. Rejea hotuba ya kuomba kura ya Magufuli utaona kuwa wenyewe kwa wenyewe wanajuana sasa Jaji angesimama pale angeomba-ombaje kura. Angekuwa ni mgeni kabisa. Ingekuwa ni kama kumkaribisha Tundu Lissu agombee urais kupitia CCM. Wasingechukua hatua hiyo na kusalimika. Hivyo, CCM wakaamua kuanzia vikao vya chini kwenda na uchaguzi rahisi na salama kwao (kwa kiasi). Wawachague watu ambao ni wenzao na ambao watacheza mpira na wenzao vizuri. Hawakuweza kuchagua mtu ambaye atawasafisha wao wenyewe kwanza kabla ya kusafisha taifa. Magufuli ambaye watu wameona anashangiliwa na watu wengine ati kumuita ni “jembe” hana tofauti na mgombea mwingine yeyote wa CCM – wote maslahi yao ya kwanza ni CCM (na kauli zake zinafahamika katika hili) na anayedhania kuwa chini ya Magufuli CCM itakuwa tofauti anajidanganya. Walichofanya ni kumchagua “mwenzao” kwani ni salama kwao. Na hili ni somo kwa watu kama Jaji Ramadhani ambao wanafikiri CCM ya sasa ni ile. Kwamba kwa namna fulani inaweza kutengenezwa upya. Kama Makongoro – aliyepigania chama hakufika mbali kama yeye ni lazima lipo somo kwa wengine wote ambao wanafikiria kukitumikia chama hicho. Kitu pekee ambacho Jaji anaweza kufanya sasa ni kuamua tu kuyaweka magwanda yake kama ukumbusho wa mojawapo ya makosa makubwa ya kimaono aliyowahi kuyafanya. Ila kama anaamini CCM ni wenzake tumuone akisimama kumnadi Magufuli jukwaani.

- See more at: http://raiamwema.co.tz/kwa-nini-haikuwa-jaji-ramadhani#sthash.GPPvveLo.dpuf

No comments :

Post a Comment