zanglassworks

AirFreight

Kwarara Msikitini

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, July 19, 2015

Mwinyi avunja ukimya kilichotokea Dodoma

Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein (aliyeinamisha kichwa) na viongozi wengine wa dini na serikali wakiomba dua baada ya sala ya Eid el Fitr iliyosaliwa jana , mjini Zanzibar
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amevunja ukimya kuhusu namna mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM, ulivyokuwa Dodoma mpaka akapatikana Dk John Magufuli.

Mwinyi ambaye ni sehemu ya Baraza la Wazee la CCM, lenye mamlaka na ushawishi katika vikao vyote vya juu vya chama hicho, alizungumzia mchakato huo jana alipokuwa akitoa salamu za Sikukuu ya Idd, baada ya kumaliza sala katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.

“Mambo yalikuwa magumu kidogo kule Dodoma, lakini tunamshukuru Mwenyezi Mungu jahazi lilifika salama, kwa pamoja tuendelee kuwa watulivu hadi Uchaguzi Mkuu utakapofika na tuilinde amani,” alisema Mzee Mwinyi.

Mzee Mwinyi alimshukuru Mungu akisema japo mambo yalikuwa magumu wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi, suala hilo lilimalizika salama bila kuwepo kwa tatizo lolote.

Alisema Uchaguzi Mkuu utakapofika mwezi Oktoba, Watanzania wanapaswa kuchagua viongozi wazuri watakaoleta amani, mapatano na maendeleo.

Alitaka Watanzania waachane na fikra za kibaguzi kwani hakuna aliye bora kuliko binadamu mwingine hapa duniani, huku akishauri waumini wa dini zote kuombea Taifa lipite salama katika uchaguzi huo.

Ugumu wenyewe

Ingawa Mzee Mwinyi hakutaka kufafanua kuhusu ugumu huo, lakini moja ya mambo yaliyoashiria ugumu wa mchakato, ilikuwa kujitokeza kwa wawania urais 42 waliochukua fomu, huku 38 kati yao wakirejesha na kutoa nafasi kwa vikao, kukabiliana na ugumu wa kuchambua majina yaliyotakiwa kufanyiwa uamuzi na vikao mbali mbali vya chama.Rais Jakaya Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM naye alikiri ugumu huo alipokuwa akitoa hotuba ya kuaga wabunge, ambapo alisema wagombea wamejitokeza kwa wingi na wengi ni vigogo na kuwashauri wasinune baada ya vikao vya chama kufanya uamuzi.

Miongoni mwa vigogo hao ni pamoja na wasaidizi na washauri wakuu wa Rais Kikwete, ambaye alishaweka wazi msimamo wake kuwa hana mgombea, akiwemo Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

V i g o g o w e n g i n e ni pamoja na mawaziri wakuu w a s t a a f u , a k i w e m o F r e d e r i c k Sumaye wa Awamu ya Tatu na Edward Lowassa, aliyeongoza katika miaka miwili ya mwanzo ya Serikali ya Awamu ya Nne.

Pia kulikuwa na mawaziri wengi wa Serikali inayoongozwa na Rais Kikwete, wakuu wa zamani wa Taasisi ya Usalama wa Taifa, mabalozi, wabunge na makada wengine wa CCM, wenye sifa za kitaifa na kimataifa, mvuto na nguvu ya ushawishi katika nafasi hiyo.

*Mchujo wa vikao
Ugumu mwingine ulioonekana, ulikuwa kazi ya mchujo ambayo kwa kuongozwa na vigezo vilivyokuwa bayana, ilianza na vikao vya mashauriano, ikafuatiwa na kikao cha Kamati Ndogo ya Usalama na Maadili na kuingia katika Kamati Kuu ya CCM, ambayo ilitakiwa kupitisha panga kali na kuja na wagombea watano.

Kamati Kuu iliyoongozwa na Rais Kikwete ilifanya kazi yake na kuja na majina ya makada watano, kati ya hao mawaziri ni wanne akiwemo wa Ujenzi, Dk John Magufuli, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Balozi wa Umoja wa Afrika nchini Marekani, Amina Salum Ali.

Ugumu wa upatikanaji wa majina hayo yaliyopelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, ulijidhihirisha kwa kuwa hata washauri wa karibu wa Rais Kikwete; yaani Makamu wa Rais Dk Bilal na Waziri Mkuu Pinda, pamoja na mawaziri wakuu wa zamani, Sumaye na Lowassa, hawakuwamo katika majina matano ya awali.

Tukio la baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu, Dk Emmanuel Nchimbi, Sophia Simba na Adam Kimbisa kujitenga na uamuzi wa kikao walichoshiriki, ni moja ya kielelezo cha ugumu huo.

Hata hivyo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alifafanua kuwa uamuzi wowote katika vikao unafanyika kwa kura, ambapo wengi hupewa na wachache husikilizwa, akimaanisha kuwa wajumbe wengi wa Kamati Kuu zaidi ya 30 waliridhia majina hayo matano, isipokuwa hao watatu.

Ugumu NEC

Wakati wa ufunguzi wa vikao vya NEC uliokuwa wazi, baadhi ya wajumbe waliimba nyimbo za kumsifu Lowassa, ambaye ni mmoja wa wagombea vigogo, ambaye jina lake halikuwa miongoni mwa majina matano yaliyopaswa kujadiliwa na kupigiwa kura na NEC.

Hata hivyo, taarifa za ndani zilieleza kuwa wajumbe hao wa NEC baada ya kujadiliana, waliridhia kwa umoja kupigia kura majina hayo matano yaliyopendekezwa na Kamati Kuu, ambapo Dk Magufuli, Balozi Amina na Dk Migiro walipita na majina yao kwenda katika kikao cha Mkutano Mkuu.

Usalama wa jahazi

Huenda kauli ya Mzee Mwinyi kuwa jahazi lilifika salama, ilimaanisha katika Mkutano Mkuu uliooneshwa moja kwa moja na televisheni mbalimbali, kwani tofauti na ilivyokuwa katika vikao vingine hasa Kamati Kuu na NEC, Mkutano Mkuu ulidhihirisha uimara na umoja wa chama hicho, ambapo wagombea walipata nafasi ya kujieleza na kupigiwa kura na wajumbe.

Uchaguzi huo wa kumpata mgombea wa CCM, uliweka historia ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya chama hicho, tangu wakati wa kupigania Uhuru, wakati huo ikiwa Tanu na baadae Tanu ilipoungana na ASP kuunda CCM, wanawake wawili walipenya kuingia katika Mkutano Mkuu.

Kukubalika kwa uamuzi wa Kamati Kuu na NEC, kulijidhihirisha katika Mkutano Mkuu uliofanyika kwa shangwe, ambapo baada ya kura, Dk Magufuli aliibuka na ushindi wa kishindo wa baada ya kupata kura 2,104 kati ya kura halali 2,416, sawa na asilimia 87.1 ya kura zote.

Balozi Amina alifuata kwa kupata kura 253 sawa na asilimia 10.5 huku Dk Migiro akipata kura 59 sawa na asilimia 2.4, huku kura sita tu zikiharibika, jambo lililodhihirisha kuwa CCM ni moja, imempata mgombea wake kwa umoja na kufifisha mgawanyiko na hofu iliyotokana na vikao vya awali, hasa Kamati Kuu na NEC.

*Kukubalika kwa Magufuli

Ugumu na hofu ya mchakato wa kumpata mgombea wa CCM viliendelea kufifia, pale washindani wakuu wa Dk Magufuli; Dk Migiro na Balozi Amina, walipomuunga mkono na kufuatiwa na shangwe ya kumkubali kutoka kwa wajumbe wote wa Mkutano Mkuu.

Shangwe hiyo ilifuata mpaka katika maoni ya wananchi, waliomkubali mgombea huyo kwa historia yake ya uchapakazi na kuchukia uzembe, huku vigogo wengi wa chama hicho, wakiwemo waliowania kuteuliwa kugombea urais, wakikubali chaguo hilo la CCM na wengine kuamua kustaafu, huku wengine wakijipanga kuwania ubunge.

Hatua ya Magufuli kumteua Samia Suluhu Hassan kuwa Mgombea Mwenza, iliweka historia nyingine katika chama hicho, ambapo kama mgombea huyo akipitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwania urais na kuchaguliwa na Watanzania, Tanzania itaweka historia ya kuwa na mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais.

Dk Shein, sera

Akizungumza na viongozi mbalimbali waliohudhuria sherehe za Baraza la Idd Unguja jana, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein aliwataka viongozi wa dini na vyama vya siasa, kusisitiza umuhimu wa amani na utulivu pamoja na kufuata sheria kuelekea Uchaguzi Mkuu, ili kuepuka Taifa kuingia katika vurugu za kisiasa.

Akizungumza na viongozi mbalimbali waliohudhuria katika sherehe za Baraza la Iddi, alisema vurugu za kisiasa zinazotokana na chuki zinatakiwa kuepukwa kwa kufuata sheria na katiba ambayo ndiyo muongozo wa nchini.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kushindana kwa sera zitakazosisitiza amani na maendeleo kwa ajili ya kutumikia wananchi.

“Nawaomba viongozi wa dini na vyama vya siasa kuhimiza umuhimu wa kutunza na kudumisha amani wakati taifa likielekea katika Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Alisema Oktoba 25, Zanzibar itaingia katika Uchaguzi Mkuu wa viongozi wakuu ikiwemo Rais wa Zanzibar na kusisitiza maamuzi ya Tume ya Uchaguzi (ZEC), yaheshimiwe kwa mujibu wa Katiba ambao ndiyo waliopewa jukumu la kusimamia uchaguzi.

“Oktoba 25, tutafanya Uchaguzi Mkuu wa viongozi mbalimbali ikiwemo Rais wa Zanzibar ambapo nawaomba wanasiasa kufuata sheria na katiba kwa kuheshimu uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ambayo kwa mujibu wa katiba ya mwaka 1985 sura ya tisa imepewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi huo,” alisema.

Aliwanasihi wazazi kuwalinda watoto wao na kuacha kujiingiza katika matukio ya vurugu wakati wa Uchaguzi Mkuu kwa sababu wanasiasa wamekuwa wakiwatumia kutekeleza matakwa yao.

Alisema vyombo vya ulinzi vimejizatiti kulinda amani na utulivu katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu ili kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki vizuri katika mchakato wa demokrasia.

Mufti Zanzibar, viongozi

Awali Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Kabi aliombea dua Taifa la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na viongozi wake, ili wawe na hekima kubwa katika kuongoza nchi na kusimamia amani wakati wa Uchaguzi Mkuu.

Alisema mafundisho ya dini ya Kiislamu yanasisitiza amani, upendo, subira na uvumilivu kuwa ndiyo njia sahihi zaidi ya kuongoza nchi na waumini wake.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa ngazi za juu akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais, Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi pamoja na mgombea mwenza wa nafasi ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, Samia Suluhu Hassan.

/HabariLeo

No comments :

Post a Comment