Mtikisiko wa uchumi duniani wa mwaka 2008 umetoa changamoto nzito kuhusu majukumu ya benki kuu katika kusimamia uchumi.
Malengo ya sera za uchumi baada ya Vita ya Pili ya Dunia katika nchi zilizoendelea yaliasisiwa na fikra mpya za uchumi mkubwa zilizoanzishwa na John Maynard Keynes. Malengo hayo yalikuwa kuwapo na ajira kwa wote, kukuza uchumi, kuwapo kwa utengamavu wa uchumi mkubwa kwa kudhibiti mfumuko wa bei, kuwapo na urari wa malipo ya nje na akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kuruhusu malipo ya kawaida ya uagizaji wa bidhaa na huduma bila kuweka vizuizi vya biashara.
Majukumu ya Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve Board) yalielezwa wazi kuwa ni kudhibiti mfumko wa bei na kuhakikisha kuwapo na ajira kwa wote.
Mfumko wa bei katika nchi zilizoendelea hasa Marekani na Uingereza katika miaka ya 1970, kulikuwa na mapinduzi makubwa yaliyotokana na mabadiliko ya sera. Hii ilichochewa na kuingia madarakani kwa Margret Thatcher nchini Uingereza na Ronald Reagan, Marekani.
Fikra za mchumi wa mlengo wa kulia, Milton Friedman, zilizosisitiza kuwa jukumu la benki kuu ni kudhibiti mfumko wa bei, zilipewa umuhimu mkubwa katika uandaaji na utekekezaji wa sera za uchumi.
Mfumko wa bei wa juu uliotokea Ujerumani baada ya Vita ya Kwanza ya Dunia, wateja walihitaji kubeba kapu kubwa lililojaa noti kununua bidhaa za kawaida kama vile mkate, kumewafanya Wajerumani waogope na kuchukia mfumko wa bei.
Baada ya Vita ya Pili, Benki Kuu ya Ujerumani (Bundesbank) ilijikita zaidi katika kudhibiti mfumko wa bei. Wajerumani hawakufurahia kuacha sarafu yao (Deutsch Mark) na kuanza kutumia Euro mwaka 1999.
Ujerumani ilihakikisha kuwa sheria iliyoanzisha Euro inatamka wazi kuwa lengo la benki kuu ya Ulaya litakuwa kudhibiti mfumuko wa bei na haitajihusisha na kulipia nakisi ya bajeti ya Serikali wanachama wa Euro.
Baada ya Vita ya Pili, benki kuu zilizoanzishwa katika nchi maskini na zimepata uhuru kutoka kwa Wakoloni wa Ulaya zilikuwa na majukumu ya kuleta maendeleo ya uchumi. Benki kuu ziliwajibika kuanzisha na kusimamia usambazaji wa huduma za benki na upatikanaji wa mikopo kwa wananchi wengi.
Benki Kuu ziliwajibika kuanzisha na kusimamia Benki za Maendeleo zenye malengo ya kugawa mikopo ya muda mrefu kwenye sekta ya viwanda, kilimo na ujenzi wa nyumba. Benki kuu pia zilihusika na kuanzisha utaratibu wa kusaidia kampuni ndogo na za kati kuweza kupata mikopo.
Kuanzia mwanzoni wa miaka ya 1980, mtazamo wa Mashirika ya Kimataifa ya Fedha na Uchumi na tasnia ya uchumi kuhusu nafasi ya Benki Kuu katika maendeleo ya uchumi haikufanana na historia ya Benki Kuu katika nchi zilizoendelea. Mtazamo wa kihafidhina ni kuwa Benki Kuu ziwe huru na zisiingiliwe na Serikali.
Lengo la msingi la Benki Kuu ni kuhakikisha kuwa hakuna mfumko wa bei wa juu. Ikiwezekana Benki Kuu ziwe na lengo rasmi la mfumko wa bei usiozidi asilimia 5 au ufanane na nchi ambazo ni wabia katika biashara ya bidhaa na huduma.
Katika kufikia malengo ya kuzuia kuwepo kwa mfumko wa bei, Benki Kuu isitumie sera za moja kwa moja za kudhibiti ukuaji wa mikopo na karadha kama vile kuweka kiwango cha mikopo itakayotolewa, badala yake Benki Kuu zitumie riba inayotoza benki zinapokopa kutoka Benki Kuu kudhibiti ongezeko la mikopo inayotolewa na benki za biashara.
Uhuru wa Benki Kuu maana yake Serikali isiitumie Benki Kuu kugharimia shughuli zake na kulipia nakisi ya bajeti. Benki Kuu isichape noti kuziba pengo kati ya matumizi na mapato ya Serikali.
Lengo la msingi la benki kuu ni kudhibiti mfumko wa bei na kwa hiyo benki kuu haitajihusisha na malengo mengine kama vile kuongeza ajira au kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi ikiwa malengo haya yatahatarisha mfumuko wa bei.
Benki kuu haipaswi kuelekeza mikopo katika sekta muhimu za uchumi kama vile kilimo, viwanda na miundombinu. Soko huria la fedha liruhusiwe kuamua riba ya mikopo.
Benki kuu isitowe ruzuku kupunguza riba kwa sekta maalumu na isipange riba zitakazotozwa na benki za biashara. Benki kuu isingilie kati soko la fedha za kigeni na kwa hiyo thamani ya sarafu iwekwe na soko huria la fedha za kigeni. Kuzuia fedha za kigeni kuingia au kutoka siyo kazi ya Benki Kuu.
Msimamo na sera ya kuwa Benki Kuu ziwe huru na kazi yake pekee ni kuhakikisha kuwa hakuna mfumko wa bei unakinzana na historia ya sera za benki kuu katika nchi zilizoendelea.
Historia ya Benki Kuu Marekani, Uingereza na nchi nyingine za Ulaya inaonyesha wazi kuwa kazi kubwa ya benki kuu na kwa kweli benki kuu zilianzishwa kugharimia matumizi ya serikali, kupanga thamani ya sarafu na kusaidia sekta za uchumi ambazo serikali iliamua kuwa ni kipaumbele kwa kuzitengea mikopo na karadha. Jukumu la benki kuu kudhibiti mfumko wa bei halikuwa jukumu pekee, bali lilikuwa miongoni mwa majukumu muhimu ya benki kuu. Katika nchi za Ulaya, Benki Kuu zilikuwa na jukumu la kugharimia vita dhidi ya dola nyingine.
Nchi za Ulaya kama Ufaransa, zilizokuwa nyuma kwa maendeleo ya viwanda ukilinganisha na Uingereza, zilitumia Benki Kuu kugawa mikopo kwa kampuni za ndani ili zianzishe na kukuza viwanda. Japan ilitumia Benki kuu yake kuchochea mapinduzi ya viwanda.
Benki kuu katika nchi zilizoendelea zimesaidia nchi zao kukuza na kuleta mabadiliko ya mfumo wa uchumi. Benki kuu za Uingereza na Marekani zimetumiwa kukuza sekta ya fedha na hasa katika shughuli za biashara na uwekezaji nchi za nje kwa kutumia sera ya riba ya chini ili kumotisha utoaji wa mikopo.
Benki kuu zilizojikita katika maendeleo ya miundombinu na viwanda kama vile Benki Kuu ya Japan na Korea Kusini zimechangia zaidi katika kukuza na kubadilisha mfumo wa uchumi kuliko nchi ambazo benki kuu zao ziliweka kipaumbele katika kukuza sekta ya fedha. Benki kuu katika nchi zilizoendelea zilianza kama benki binafsi na baadaye kuchukuliwa na Serikali. Ukitazama historia, majukumu muhimu ya benki kuu ni pamoja na, mosi; kuchapisha noti na kufua sarafu za nchi.
Pili; benki kuu ni benki ya Serikali. Shughuli za kibenki za serikali zinasimamiwa na Benki Kuu. Tatu; benki kuu ni benki ya benki za biashara. Benki za biashara zinaweka akiba zake na kukopa toka benki kuu. Sehemu ya akiba zinazowekwa na wateja katika benki za biashara inawekwa na benki hizo katika benki kuu.
Nne, benki kuu ni mkopeshaji wa mwisho wa sekta yote ya fedha. Benki za biashara na asasi nyingine za fedha zinapokabiliwa na matatizo ya ukata wa fedha ambao unaweza kuathiri mfumo wote wa fedha, zinategemea kukopa toka Benki Kuu.
Tano; benki kuu ni msimamizi na mtekelezaji wa sera za fedha na thamani ya sarafu na inaweka akiba ya fedha za kigeni za nchi. Sita, benki kuu inasimamia sera za fedha ili kuhakikisha shughuli za uchumi na biashara zinafikia uwezo uliopo wa uzalishaji wa bidhaa na huduma. Saba; benki kuu inadhibiti ukuaji wa mikopo na karadha kufikia malengo ya taifa hususan kuhusu mfumko wa bei.
Kuanzia mwaka 1978, Tanzania iliingia katika mgogoro mkubwa wa uchumi. Mfumko wa bei uliongezeka na bidhaa muhimu zilipotea madukani. Sera ya serikali ya kupanga bei ilishindwa kudhibiti mfumko wa bei. Marekebisho ya sera ya uchumi yaliyoanza wakati wa awamu ya Rais Mwinyi pia yalihusu sekta ya fedha.
Sheria ya benki na taasisi za Fedha ya mwaka 1991 iliruhusu uanzishwaji wa benki binafsi. Sheria ya benki kuu ya 1995 na ya 2006 imeipa uhuru Benki kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa na Serikali.
Sheria ya benki kuu ya mwaka 1966 iliipa Benki Kuu majukumu ya kuchochea maendeleo ya uchumi. Mfumko wa bei wa wastani wa asilimia 30 kila mwaka kati ya 1981 na 1995 uliambatanishwa na kuwepo kwa benki kuu yenye malengo mengi na isiyo kuwa huru.
Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006 na ile ya 1995 imesisitiza kuwa lengo kuu la sera za benki kuu ni kudhibiti mfumuko wa bei. Mfumuko wa bei katika kipindi cha muda mrefu, uwe wa wastani wa asilimia 0 – 5.
Mfumko wa bei wa miaka 1980 – 95 haukusababishwa na Benki Kuu kuwa na malengo ya maendeleo. Mfumuko wa bei ni matokeo ya kushindwa kuendeleza kilimo na uzalishaji wa chakula na kutosimamia kwa makini mashirika ya umma yaendeshwe kwa ufanisi na kupata faida.
Tanzania inahitaji benki kuu yenye malengo ya maendeleo pamoja na kudhibiti mfumko wa bei. Malengo ya benki kuu yawe utengamano wa uchumi mpana, ukuaji wa uchumi ulio endelevu na shirikishi unao ongeza ajira, maendeleo ya sekta ya fedha yaliyo shirikishi kuwawezesha Watanzania wengi kupata huduma za fedha.
Benki kuu iwe mstari wa mbele katika kuanzisha benki za maendeleo ya viwanda, kilimo na nyumba zinazoweza kutoa mikopo ya muda mrefu. Jambo la kuzingatia Benki za Maendeleo ziendeshwe kwa weledi na ufanisi. Benki kuu iisaidie serikali iwe na bajeti inayotekelezeka na iache utaratibu wa bajeti ya fedha taslim (cash budget) ambao unaathiri sana miradi ya maendeleo. Kwa mfano Benki Kuu ya Tanzania inaweze kuikopesha serikali kwa riba nafuu siyo zaidi ya asilimia 10 ya mapato yake ya kodi ya miezi 12 iliyopita.
Rais atakayechaguliwa Oktoba 2015 arekebishe sheria ya benki kuu na kuifanya iwe nyenzo ya kuleta maendeleo shirikishi bila kuchochea mfumko wa bei.
No comments :
Post a Comment