Mawaziri hao ni walioshindwa katika kura za maoni za marudio.
Waliotemwa katika uteuzi wa Kamati Kuu ni Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani (Busega); Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dk. Seif Rashid (Rufiji) na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk. Biligith Mahenge (Makete).
Kamati Kuu ilikutana jana katika ofisi ndogo za CCM Lumumba, Dar es Salaam jana chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, waliopitishwa niJerry Silaa (Ukonga), Edward Mwalongo (Njombe Kusini), Venance Mwamoto (Kilolo), Dk. Raphael Chegeni (Busega) na Edson Ngonyani (Namtumbo).
Wengine ni Mohamed Mchengerwa (Rufiji), Dk. Norman Sigara (Makete), Martin Msuha (Mbinga Vijijini) na Joel Makanyanga Mwaka (Chilonwa). Nape aliyataja majimbo yaliyokuwa hayajatolewa maamuzi kuwa ni Jimbo la Singida na Kiteto mkoani Manyara.
Nape alisema mbali na kikao hicho kuteua majina ya wagombea, pia kilijadili ajenda za uchaguzi mkuu ujao ambao utafanyika Oktoba 25, mwaka huu.
“Kura za maoni siyo kigezo pekee cha kumpitisha mgombea kuwania nafasi ya ubunge, hivyo kuna taratibu na kanuni za vikao mbalimbali vya chama, tathmini imefanywa na kusimamisha hawa, tumekuwa tukibadilisha taratibu za kupata wagombea ubunge mara kwa mara,” alisema Nape.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment