Chama cha Mbowe, Zitto na Slaa Ingawa Chadema kilianzishwa zaidi ya miaka 20 iliyopita, chama hicho hakikuwahi kupata umaarufu iliokuwa nao kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambako Dk. Slaa alipata kura zaidi ya milioni mbili akiwa mgombea urais wa Chadema dhidi ya Rais Jakaya Kikwete. Kwa mujibu wa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo, watu watatu waliipa Chadema umaarufu iliokuwa nao mwaka 2010 na ilionao hadi sasa. “Akina Mzee Edwin Mtei walianzisha chama lakini hakikuweza kukua kwa kasi na siku zote kilikuwa nyuma ya vyama kama NCCR-Mageuzi, CUF na Tanzania Labour (TLP).
Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika baada ya Mbowe kupata Uenyekiti. “Ni Freeman ndiye aliyeingiza kundi la vijana wasomi wenye akili na wasomi wengine ndani ya chama hicho. Aliwalea na kuwapa nafasi kubwa za uongozi pasipo kujali umri wao au uzoefu katika uongozi. “Katika vijana hao, alikuwepo Zitto Kabwe ambaye alikuja kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema.
Baadaye walikuja vijana kama John Mnyika na Halima Mdee ambao nao walifanya kazi yao vizuri kwenye chama. “Umaarufu wa Chadema ulianza kupaa kwenye Bunge la Tisa kati ya mwaka 2005 hadi 2010. Zitto na Dk. Slaa ndiyo waliokuwa vinara bungeni kwa kutoa hoja kama ile ya Buzwagi na Orodha ya Mafisadi katika Viwanja vya Mwembeyanga jijini Dar es Salaam.
“Hoja zile bungeni na kwenye mikutano ya hadhara ya Mbowe, Zitto na Slaa ndiyo iliyoleta chachu ya mabadiliko kwenye siasa za Tanzania na matokeo yake Chadema ilipaa na kuwa chama kikuu cha upinzani hapa nchini,” alisema Kitila ambaye kuna wakati alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema. Zitto alifukuzwa Chadema, pamoja na Kitila kwa madai ya usaliti, na msomi huyo wa masuala ya siasa aliliambia gazeti hili kuwa kama Slaa naye ameondoka maana yake ni kwamba Chadema imebaki na figa moja katika mafiga matatu yaliyokijenga chama hicho. “Wakati Zitto alipofukuzwa Chadema mtikisiko haukuonekana kwa sababu Slaa alikuwepo. Watu waliendelea kukitazama chama hicho katika mrengo ule ule kwa sababu ya Katibu Mkuu huyo. Sasa kwa sababu ameondoka, ni wazi kutakuwa na mtikisiko,” alisema. Raia Mwema linafahamu kuwa Slaa alikuwa amepangwa kuwa Meneja Kampeni wa Lowassa kwenye uchaguzi huo kutokana na kupendwa kwake na wananchi lakini itabidi sasa Chadema itafute mtu mwingine wa kufanya kazi hiyo.
Mbunge huyo wa zamani wa Karatu anadaiwa kutokukubaliana na hatua ya Chadema kumtangaza Lowassa kuwa mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, akieleza kwamba waziri mkuu huyo aliyejiuzulu kwa kashfa ya zabuni ya kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond, alitakiwa kwanza aikane CCM ndiyo akubalike kwenye chama hicho. Hata hivyo, akizungumza na wajumbe wa Baraza Kuu la Chadema, Jumatatu wiki hii, Mbowe alisema Slaa alikubaliana na jambo hilo katika hatua za awali lakini alibadilika baadaye. “Katika vikao vyetu tulivyokuwa tunakaa tulikuwa tunakubaliana lakini katika dakika za mwisho mwenzetu alibadili msimamo. Kamati Kuu ya chama ikaanza mazungumzo naye (Dk Slaa), lakini hadi jana (Jumapili iliyopita), nimezungumza naye bado msimamo wake ni ule ule,” alisema Mbowe na kuongeza; “Kwa hiyo tunamruhusu apumzike kwanza kupisha kipindi hiki cha uchaguzi, baadaye huko mbele ya safari kama atataka ataungana nasi. Hatuwezi kuacha mamilioni ya wanachama eti kwa sababu ya matakwa ya mtu mmoja awe Dk. Slaa ama Mbowe”.
Ingawa Slaa hakuwa mmoja wa wenyeviti wanaounda Ukawa, lakini ilikuwa ikifahamika kwamba ndiye mtu mmoja aliyekuwa na nafasi zaidi ya kuteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya umoja huo kabla ya Lowassa kuingia Chadema. Mmoja wa viongozi wa juu wa Chadema aliyehudhuria mkutano wa Baraza Kuu hilo na kuzungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutotajwa jina, alisema wako wana Chadema wanaoamini kwamba kura milioni mbili walizozipata mwaka 2010 zilitokana na imani watu waliyokuwa nayo kwa Slaa kuliko hata chama hicho. “Kama utakumbuka, kuna maeneo ya kambi za jeshi ambako Chadema iliibuka mshindi na kule hakuna wanachama wa chama chetu. Watu waliokuwa wakimwamini wengine hawakuwa hata wana Chadema na hawa ndiyo wanahitajika kushinda uchaguzi,” alisema mjumbe huyo kutoka Mkoa wa Iringa. Slaa mwenyewe aliwasiliana na gazeti dada la hili la Raia Tanzania toleo la Agosti Mosi mwaka huu na kusema; “Imeniumiza sana! Na ninaomba ujue mimi shida yangu si urais. Ila siko tayari kuiong’oa CCM kwa kuwa tu tunataka kuingia madarakani bila principles (misingi).
“Nimezoea kusimamia maadili ninayoamini. Nimeheshimu na kutii dhamira yangu daima kwa kuwa naamini Mungu huzungumza nasi kupitia dhamira zetu, ndiyo maana binadamu tuko tofauti na viumbe wengine. Watasema mengi, propaganda daima hazijengi,” alisema. Mmoja wa wahadhiri waandamizi katika Kitivo cha Siasa na Utawala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Alexander Makulilo, aliliambia gazeti hili Jumatatu wiki hii, kuwa Slaa atakuwa na madhara zaidi kama atahamia chama kingine kuliko akibaki kimya ndani ya Chadema. Kwanza niseme kwamba sina uhakika kama Slaa ameacha uanachama wake Chadema kama ilivyoripotiwa kwenye magazeti.
Mimi ni mtafiti na hivyo ni muhimu kuzungumza kitu ambacho nina uhakika nacho. “Lakini, kama tukiamua kukubali kuwa Slaa ameondoka Chadema, naona itakuwa mbaya zaidi kama atahamia chama kingine. Lakini, kama atabaki Chadema tu bila kufanya lolote, sidhani kama kutakuwa na tatizo kubwa sana. “La muhimu kufahamu ni kwamba Slaa ana haki ya kuhama Chadema na kwenda chama kingine na haki hiyo iko kikatiba. Ni uamuzi wake kubaki au kuhama chama hicho lakini hadi mojawapo kati ya kuhama na kubaki na litakapofanyika, ndipo hasa tutajua athari zake kwa Chadema na Ukawa,” alisema mhadhiri huyo.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/dk-slaa-kuiumiza-ukawa-0#sthash.FGwi2NOH.dpuf
No comments :
Post a Comment