CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeweka hatima yake, hadhi yake, na sifa zake zote mikononi mwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa. Kwa kumchukua kama mwanachama wake na siku ya pili kumpa ugombea urais kwa sababu tu ya jina na historia yake, Chadema kimeamua kufanya kitu ambacho hakikufikiriwa kinawezekana miezi michache tu nyuma, yaani kuweka mayai yake yote kwenye kikapo atakachobeba Lowassa. Kitu pekee ambacho wana Chadema wanakiombea ni kuwa Lowassa asijikwae.
Ujio wa Lowassa Chadema umepokelewa kwa baadhi ya watu kama ni nafasi ya dhahabu kwa upinzani kuweza kuking’oa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani. Hii ndiyo sababu pekee kubwa na yenye kuvutia ambayo imetolewa na viongozi mbalimbali wa upinzani wakiwemo Tundu Lissu, Profesa Mwesiga Baregu na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.
Wote hawa na wengine ambao wamekumbatia ujio wa Lowassa Chadema (na kwa umbali zaidi ndani ya Ukawa) wamechukua uamuzi huu wakiamini kabisa Lowassa haji tu na jina lake lakini pia anakuja na kura za ziada kwa urais na wabunge ambazo bila ya yeye Chadema isingeweza kuzipata kama ingemsimamisha mgombea mwingine yeyote. Kwamba, wakiwa na Lowassa kura zao zitatosha na hivyo CCM itaanguka.Hii ni kamari kubwa sana ya kisiasa ambayo imechezwa na wanasiasa hawa na kwa kweli kama wana mizimu au miungu au Mungu wanayemwamini inawapasa waombee kweli itokee. Endapo itatokea kweli CCM ikaondolewa Lowassa akawa Rais kupitia Chadema na Bunge likachukuliwa na Chadema na washirika wake kwenye Ukawa viongozi hawa wataandikwa katika historia kama ‘magenius’ ambao waliweza kucheza kete zao za kisiasa vizuri kabisa hata kwa gharama ya kukipasua chama chao ili wavune zawadi ile nono ya madaraka ya urais na wabunge.
Endapo hata hivyo haitatokea iwe hivyo – yaani Chadema na washirika wake washindwe kuing’oa CCM madarakani wakiwa na “Messi” wao waliyemsajili dakika za majeruhi basi Mbowe na wenzake wataingia katika historia kama wanasiasa waliocheza kamari mbaya zaidi ambayo itawapasa iwagharimu nafasi zao ndani ya chama siku moja tu baada ya matokeo kuthibitisha kuwa Chadema na washirika wake wameanguka mbele ya CCM licha ya kumchukua Lowassa.
Ni vizuri kufikiria kuwa mambo makubwa mawili yataweza pia kutokea; ama Lowassa ataonekana shujaa kweli kweli hasa kama ataweza kuleta ushindi ambao wapenda mageuzi wameahidiwa au Katibu Mkuu wa Chadema ambaye inaonekana hadi hivi sasa hayuko hasa na pendekezo hili la Lowassa ataonekana kama shujaa aliyekataliwa.
Kitendo cha kumweka pembeni Dk. Slaa, kiongozi wao wenyewe na mtu ambaye tayari alikuwa na mtaji mkubwa tu wa kisiasa ili tu wampokee Lowassa kwa zaidi ya mtaji mkubwa zaidi kitaangaliwa vizuri sana wakati wa kampeni na wakati wa matokeo ya uchaguzi.
Ikumbuke kuwa kuelekea kampeni viongozi wote wakubwa ambao wanaonekana kumkaribisha Lowassa wa wenyewe wataenda kubanwa na CCM majimboni. Mbowe, Lissu, Mnyika, Mwesiga na wengine watatakiwa waendee kutetea majimbo yao (ya zamani au mapya) na kampeni za urais zitaachwa kwa viongozi wengine na bila ya shaka watu wa Lowassa mwenyewe. Hili litaonekana ubaya wake siku ya Uchaguzi na ni kamari nyingine ambayo uongozi wa Chadema itabidi wawe tayari kuilipa.
Lakini kuna jambo jingine ambalo linahitaji kutafakariwa kwa makini sana na matokeo yake. Kwa kumfanya Lowassa kuwa ndiye mgombea wake pekee Chadema imejiweka pabaya zaidi kuliko watu wanavyoweza kufikiria kwani wameamini kuwa ni lazima Lowassa atagombea urais.
Miezi mitatu ni mingi sana na ikitokea kwa sababu yoyote ile Lowassa anaamua kujitoa kwenye kinyang’anyiro au hawezi tena kugombea Chadema itabidi ijiulize inamtafuta nani mwenye mvuto tena kama wa Lowassa na anayeweza kuvuta kura za wananchi tena. Wataweza kumuomba Slaa tena agombee kama walivyofanya 2010? Au itabidi wamuombee Lipumba? Au kwa vile wanaamini CCM inachukiwa sana wanaweza hata kumuomba Mbowe mwenyewe agombee.
Vyovyote vile ilivyo, Lowassa ni kamari ambayo Chadema na uongozi wake wa kitaifa wanaweza kuvuna sana – kama wakishinda au wao wenyewe watajikuta wanavunwa kama wakishindwa. Ni matumaini yangu wangu wananchi na wanachama ambao wameunga mkono uamuzi huu na wale ambao wamepinga wawe tayari kufuata njia moja au nyingine. Endapo Chadema itashindwa kuleta matokeo makubwa sasa Mbowe na viongozi wenzake ni LAZIMA watakiwe kujiuzulu nafasi zao za uongozi wa chama. Hii ni kanuni ya kidemokrasia tu.
Kiongozi mkuu wa upinzani aliyeongoza harakati za kutaka Scotland ijitenge toka Uingereza aliposhindwa kwenye kura hakufikiria mara mbili; alijiuzulu ili kutoa nafasi kwa wengine.
Ni matumaini yangu kama Mbowe atashindwa kutimiza hii ahadi ya kwenda na Lowassa na kupata ushindi wa kishindo yeye ni lazima awe wa kwanza kujiuzulu akifuatiwa na wale wote waliounga mkono wazo hili. Hii ni demokrasia. Wasiachwe waongoze chama hata kwa siku moja mbele.
Lakini kama wakishinda na kuchukua Urais na Bunge (Spika na Uwaziri Mkuu) Mbowe na wenzake wataenziwa na historia kwa uamuzi wao wa kijasiri, wa kimkakati na wa kukumbukwa. Hakuna njia ya tatu.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/kamari-waliyoicheza-kina-mbowe-na-lowassa-isipolipa-watalipa#sthash.PWMQ7H0a.dpuf
- See more at: http://raiamwema.co.tz/kamari-waliyoicheza-kina-mbowe-na-lowassa-isipolipa-watalipa#sthash.PWMQ7H0a.dpuf
No comments :
Post a Comment