Mchakato wa Katiba Mpya ukawa kama shughuli ya kawaida au mzaha. Watanzania walipatwa na machungu, sambamba na hasira; wako kimya wakisubiri ishara za nyakati. Inashangaza, hapakuwepo viongozi wakuu husika wa chama tawala CCM, Serikali, Bunge, Mahakama au Tume ya Uchaguzi wa kuwajibisha au kuwajibika kwa uzembe huu; hata kusema samahani. Tume ya Uchaguzi ikawa kweli mtoto wa nyoka.
Kwa makusudi Wazalendo wakawa wamerejeshwa kwenye Katiba yenye shaka kubwa ya mwaka 1977. Matumaini yao ya Katiba Mpya yakawa yametoswa. Je, Umoja wa Katiba yaa Wananchi (Ukawa) unaojumuisha vyama vya siasa vya Chadema, CUF, NCCR, NLD na mgombea urais wao, Edward Lowassa [U-EL] watahakikisha nchi na taifa la Watanzania watakuwa na Katiba Mpya au itakuwa kuendeleza ukatili wa machungu?
Tangazo la Uchaguzi Mkuu
Mei 25, 2015, Mwenyekiti huyo huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji (mstaafu) Damiani Lubuva alitangaza ratiba ya Uchaguzi Mkuu; uteuzi wa wagombea urais, ubunge na udiwani kuwa Agosti 12, 2015, kampeni za uchaguzi kuanza Agosti 24, 2015 na Oktoba 25, 2015 kupiga kura. La mgambo likilia kuna jambo. Upepo mkali ukaanza kuvuma, nyasi zikaanza kutikisika na wananchi wapiga kura wakaanza kuchukua tahadhari ya joka. Ikawa safari ya kuendelea Uchaguzi Mkuu bila Tume Huru ya Uchaguzi, penda usipende. Inatisha na kusikitisha kwamba viongozi wamekula kiapo hiki ‘nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba nitahifadhi, kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, ewe Mwenyezi Mungu nisaidie. Hapa ndipo tuliopo na ndiko tuendako. Ikulu kuna mvinyo mtamu unaolevya kupindukia. Je, uongozi ujao baada ya Uchaguzi Mkuu utakumbuka tena Katiba Mpya ya Wananchi au utakuwa wamelewa madaraka ya Ikulu? Wananchi wamekariri kwamba ‘bila mabadiliko ya kuhakikisha uwepo wa Katiba mpya hakuna matumaini kutoka kwa mgombea yeyote kwa lolote’
Utabiri
Kwenye makala yangu; Gazeti la Raia Mwena toleo la 358, 359 na 380, Juni 2014 niliandika ‘Katiba Mpya ya Watanzania inatabirika’. Nilihitimisha kwa kusema “Pepo za bahari zinaweza kubadilika ghafla, chama kipya chenye unyenyekevu na adilifu wa itikadi na sera zenye kujikita kwenye falsafa ya wananchi kikatinga Ikulu. Wananchi wapiga kura watathibitisha nguvu yao kwenye sanduku la kura”. Tangu hapo mengi ya utabiri yametokea. Msomaji mmoja wa makala hiyo ndiye aliyenishawishi niandike makala hii. Nitavinjari kwa kifupi sana mantiki ya utabiri wangu kabla ya kujibu swali la makali hii.
Falsafa tatu
Makala ya mwaka jana ilichambua, kuainisha na kubainisha falsafa za makundi matatu nchini Tanzania kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2015. Falsafa ya kwanza ni ya wananchi yenye kusimamia haki waliyopewa na Mungu ya kumiliki utawala, mali na utajiri wa mamilioni kwa mabilioni na matrilioni ya madola wa nchi na taifa la Watanzania; kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo na maisha bora kwa kila mtu na vizazi vijavyo. Matumaini ya wananchi wapiga kura ni uhakika wa kuwepo na umiliki wa Katiba yao mpya na bora mapema iwezekanavyo.
Falsafa ya pili ni ya wageni wa nje na mawakala [makuwadi] wa ndani ya nchi ya ufisadi na uporaji wa mali na utajiri wa Watanzania kwa njia zozote kwa masilahi yao binafsi. Falsafa hii ilipiga hodi takriban karne 12 zilizopita; tangu Wazalendo wa Kilwa Kisiwani waanze kutawaliwa kimabavu na wageni kutoka Uarabuni. Utawala wa dhuluma uliendekezwa na Wareno, kisha ukoloni wa Wajerumani na hatimaye Waingereza wakitokea bara la Ulaya Magharibi. Mafisadi wana nyenzo nyingi, uwezo mkubwa wa pesa walizopora na mtandao mpana wa kuweza kufanikisha mbinu, mikakati na mipango yao kwa uhakika ikiwa ni pamoja na kuyumbisha uongozi na kuteka nyara utawala wa Katiba za nchi dhaifu. Mafisadi wana sura nyingi kama kinyonga; waporaji, wakoloni, wahisani, wafadhili, wawekezaji, washauri, wafanyabiashara wakubwa n.k.
Makuwadi wa mafisadi ni nyoka wa ndumilakuwili huuma na kupuliza; humwagiwa vijisenti vya masharti magumu ya kuwezesha uporaji wa mali au fedha wananchi ; walengwa ni viongozi wenye nafasi nyeti ndani na nje ya vyombo vya dola na vyama vya siasa. Adui mkubwa wa mafisadi ni falsafa ya wananchi na wanajua mwarobaini wao ni Katiba Mpya.
Falsafa ya tatu ya vyama vya siasa ni kuingia na kutinga Ikulu kwanza kwa njia zozote na mengine yatafuata; kwa chama tawala cha CCM ni kutinga Ikulu milele; kwa vyama vya siasa vilivyo nje ikiwa ni pamoja na U-EL ni kwanza kung’oa CCM ili kuingia na kutinga Ikulu. Falsafa hii iliasisiwa kwa makusudi kwenye mabadiliko ya kutayarisha Katiba za Jamhuri ya Tanganyika [1962] ambayo yalifanywa na wingi wa Bunge la chama cha TANU mara tu Wananchi waliporejesha uhuru [1961].
Falsafa hii imelindwa na kuendelezwa na vyama pekee tawala vya TANU na ASP kwenye Katiba ya 1965 na chama pekee tawala cha CCM kwenye Katiba ya 1977. Nyenzo kubwa ya TANU/ASP/CCM kutinga Ikulu ni kuhodhi na kumiliki Katiba ya Wananchi pamoja na Tume ya Uchaguzi, daftari la wapiga kura, masanduku la kura na hesabu zake kwa njia zozote. Masahibu wakubwa wa waumini wa falsafa ya kutinga Ikulu ni mafisadi kwa misingi ya nipe ~ nikupe; ni uhusiano wa kuvikwa gamba. Kwa hali hii, vyama vya siasa vimeshindwa kubuni itikadi na sera maendeleo ya wananchi na taifa na hivyo kutoa fursa kwa mafisadi kujipangia wagombea wa Uchaguzi Mkuu na uongozi wa kutinga Ikulu ili kulindana na kuendeleza masilahi ya kufuru za uporaji.
Kitendawili cha kamari za Ikulu
Kufuatana na Katiba ya 1977 tuliyoirudia; Katiba ni Rais na Rais ni Ikulu. Mafisadi wanajua, ili kulinda na kuendeleza mambo yao, uteule wa wagombea urais ni lazima upangwe kwa mapema, umahiri na usiri wa hali ya juu. Kwa hali hii, kamari ya mpangaji mpya wa Ikulu 2015 ilichowezwa zamani, iliyabaki ni usanii wa mchakato wa Uchaguzi Mkuu na igizo la kupiga kura na kutangaza Rais Mpya kwa mbwembwe. Historia inathibitisha mafisadi hawana mchezo na upangaji wa Ikulu na hawawezi kuvumilia mambo yao yakikwama, kuharibika au kulipuka.
Tangu Azimio la Zanzibar la CCM hadi leo, mafisadi wamewekeza sana Ikulu na wana mikataba yao ya siri inayatakiwa kulindwa kwa njia zozote. Uwekezaji huu umejenga ushindani na kulindania kati ya makundi mengi ya makuwadi wa mafisadi (magamba) ndani ya chama tawala hata kuzidi utitiri wa wagombea 38 tulioshuhudia. Kimkakati, CCM siyo mahali tulivu kwa mafisadi kuendelea kuwekeza kwa sababu ya urasimu mkongwe, umri mkubwa wa uongozi wa juu usiyoubali hoja na haja za mabadiliko, wenye kuweka vijana pembezoni kutokana na mtindo mpya wa kuridhisha chama kwa watoto na ndugu zao.
Isitoshe CCM wanashuka chati kutokana na kuchokwa na wapiga kura na kuishwa ubunifu wa mbinu za kujikwanua. Mafisadi wameangaza na kuanza kucheza nje ya CCM; wanaona mahali bora pa kuwekeza kwa muda mrefu ni Ukawa; wana vijana wengi viongozi, wanapanda chati na pia wana nguvu. Hakuna mchawi, yanayotokea na mchezo wa kamari za mafisadi na makuwadi wao uporaji kwenye kulinda na kusaka faida ya kufuru kama zamani. Ubunifu wa mbinu, mikakati na mipango mahiri wa kuhakikisha EL anakuwa mgombea Urais wa Ukawa ulibuniwa na kukamilishwa miaka mingi.. Iliyobaki ikawa taratibu za itifaki za Katiba ya mashaka ya 1977 yenye kuelekeza Uchaguzi Mkuu. Matokeo ya mchakato wa mashaka wa Katiba Mpya ni kuibuliwa kwa Ukawa, Ukawa kuungana na EL siyo mambo ya bahati nasibu, ndiyo mipangilio ya uhakika ya falsafa ya mafisadi na makuwadi wao. Wahenga wamelonga “ukiona vyaelea vimejengwa”. Ikulu ni ya U-EL labda wakufuru kwa kuvurunda!
Kampeni za 2015
Kinyang’anyiro cha kampeni ya Uchaguzi Mkuu zitakuwa za aina yake. Agenda kuu ni mustakabali wa Katiba Mpya. Hoja ya ufisadi haitakuwa na mashiko sana kuwa hakuna wa kumnyoshea mwenzake kidole kati ya mafisadi wingi ndani ya CCM dhidi ya mmoja wa U–EL. Watanzania wanaandamwa na ukwasi wa ubunifu wa itikadi na sera wa vyama na siasa na wagombea; hivyo wapiga kura watakabiliwa na siasa uchwara; ilani zenye orodha ndefu ya kero na mipango ya kusadikika na ahadi nyingi ya miradi hadaa. Kama ilivyoonekana kwenye mchakato wa uteuzi wa wagombea wa vyama, patakuwapo na matumizi makubwa ya vijisenti kutoka kwa makuwadi wa mafisadi kwa ajili ya kafanikisha ushindi wao. Taswira ya uwanja wa kampeni utakuwa wa makundi manne.
CCM
Kundi la kwanza ni chama pekee tawala TANU/ASP/ CCM tangu uhuru na wagombea wake. Mtaji wao wa ziada ni uzoefu mkubwa, mtandao mpana hadi kwenye ngazi ya nyumba kumikumi, fursa ya kutumia vyombo vya dola bila mipaka ikiwa ni pamoja na Tume ya Uchaguzi, ushindi kwenye uchaguzi wao wa viongozi wa serikali za mitaa, kanuni ya ushindi wa mgombea Urais kwa wingi wa kura zitakazopigwa na siyo kwa zaidi ya asilimia kufuatana na Katiba ya 1977. Hata hivyo, CCM inakabiliwa, kwa mara ya kwanza na changamoto nyingi na nzito; tuhuma za kufanya mabadiliko ya Katiba za nchi tangu uhuru bila ridhaa ya Wananchi, kutosa mchakato wa Katiba Mpya; kupuuza demokrasia na haki za binadamu; utata, ukimya, na usiri wa Azimio la Zanzibar dhidi ya Azimio la Arusha, kupuuza taarifa lukuki za Tume za Rais,; usiri wa mikataba ya nchi; usiri na uwajibikaji duni kwa kashifa za ufisadi na woga wa kuendelea kushuka chati kwa wapinga kura. Mazimwi ya EL na makada wengine waliohama CCM itawaandama na yumkini wasiorithika kwenye uteuzi wa ugombea wa Urais, ubunge na udiwani. CCM watapambana na U–EL pamoja na upepo mpya za upinzani wenye nguvu mpya na zenye kuhitaji ubunifu wa kuzimudu kwa haraka. CCM wanalazimishwa kubadilika, wanaogofya kung’olewa Ikulu kwa ghafla ikiwa hawajajitayarisha kisaikolojia. Hali ya ndani na nje ya CCM siyo tulivu, mambo siyo shwari kama zamani na upangaji wao Ikulu uko mashakani!
Ukawa-Lowassa [U-EL]
Kundi la pili ni U~EL. Mtaji mkubwa wa U-EL ni fursa ya kuendeleza mshikamano wao na wapinga kura na matumaini ya Katiba mpya ya Wananchi. Ujio wa EL utachochea kasi ya matumaini, kuongeza nguvu, ujasiri, mbinu na mikakati ya kuingia Ikulu ikiwa na pamoja na kuvutia mitandao ya mafisadi, makuwadi na vijisenti. Kimsingi falsafa ya U-EL ni kuingia Ikulu kwanza kwa njia yeyote hata ikiwa ni kwa kujivika gamba la falsafa ya Mafisadi, kujenga matumaini ya kujali na kula shahani moja na Wananchi Ikulu. Mjadala wa ufisadi kati ya U-EL na CCM na ndani ya U-EL hauna tija wala mashiko. Changamoto ya U-EL ni Tume ya Uchaguzi yenye kuegemea CCM na mabavu ya vyombo vya dola. Ukawa ina fursa kubwa ya kushinda wa mapema kabisa ikiwa kwanza, watakuwa na mkataba pamoja na ratiba ya kuhakikishia wapiga kura kwa utashi wa uwepo wa Katiba Mpya tangu siku ya kwanza ya kampeni. Pili kupanga na kufanya maandamano ya kidemokrasia ya wapinga kura kutoka kila pembe ya Tanzania kuhusu uwepo Katiba Mpya. Kosa kubwa na dhambi ya U-EL ni kujiamini kupindukia kwamba ushindi uko mikononi na hivyo kujisahau, kutosa unyenyekevu, kupuuza hekima ya kuchakua tahadhari kwa mambo madogo na ‘wadogo’ na kuendeleza ushabika mkubwa wa wafuasi ambao pengine hawakujiandikisha kupiga kura au ni mamluki; hatimaye kuangusha kifunguo za kuingia Ikulu!
Ukawa Asili [UA]
Kundi la tatu ni vyama vya upinzani ambavyo viko nje ya Ukawa. Mapema kwenye kampeni itabidi waeleweke kama wako mrengo wa CCM au wa U-EL ua wanajitegemea. Vyama vya upinzani vyenye kuenzi falsafa ya Wananchi kwa dhati na haya ya Katiba Mpya na bora vina fursa ya kujiunga kama “Ukawa Asilia”. [UA] itakuwa na jukumu na wajibu wa kuhakikisha U-EL hawateke nyara agenda ya Katiba Mpya kwa masilahi binafsi ya falsafa za mafisadi na kingia Ikulu kwanza. UA itakuwa imejaza ombwe la kisasa. Wananchi na UA wanatambua na kuendeleza michango ya Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba; Katiba Mkuu wa Chadema Dk. Willbrod Peter Slaa na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ingawa wamejiuzulu.
Ikiwa U-EL watapuuzwa au kuzembea ratiba na ahadi yao, na hivyo kutosa wapiga kura kama CCM ilivyotosa mchakato wa Katiba Mpya, basi UA watawajibika. Asilia watakuwa na jukumu la kujenga hoja na kuendeleza maandamano ya wapiga kura nchi nzima hadi Katiba Mpya iwepo. Hii itakuwa fursa yao ya kujijenga na hatimaye kuingia Ikulu. Changamoto yao itakuwa uwezo mdogo wa pesa na utulivu na mshikamano wa kubuni itikadi na sera mwafaka kwa fursa hii. .
Wapiga Kura
Kundi jingine ni wananchi wapiga kura ambao wamesoma ishara za nyakati na kuchukua fursa yao ya kidemokrasi kwenye Uchaguzi Mkuu. Walijipanga vema kwenye mchakato wa Katiba Mpya wa serikali ya CCM, wakapokea uhamasishaji wa Ukawa na sasa wako kwenye kampeni na U-EL na wagombea wa vyama vingine. Mtaji wa kwanza ni mkubwa ni falsafa ya Katiba Mpya ya Wananchi ambayo ndiyo agenda kuu yenye mashiko na kueleweka kwa makundi yote ya kampeni; huku ikiendelea kupanda chati ndani ya nchi na duniani. Pili, wapinga kura wana msukumo wa pepo za kasi zilioanza kuvuma tangu uhuru kwa kukataa mabadiliko ya Katiba yao bila sababu za kimsingi na bila ridhaa yao.. Msukumo ulipewa nguvu kwenye ripoti za Tume ilizoongozwa na Jaji Francis Nyalali na Jaji Robert Kisanga. Msukumo uliendelezwa kwenye Ilani ya Chadema ya Uchaguzi Mkuu wa 2010 ambayo iliweka ahidi na ratiba ya kuanza mchakato ndani ya siku tisini; mgombea wa uraisi akiwa Dk. Willbrod Slaa. Chama tawala cha CCM na serikali walilazimika, shingo upande, kuuendeleza msukumo wa kisheria [2011] ya mchakato wa Katiba Mpya hadi walipoisitisha Mei 2015. Msukumo wa pepo za Katiba Mpya zikaendelea chini ya Ukawa. Serikali ikalazimika kwa mara ya kwanza tangu uhuru kusambaza nakala 300 za Katiba Inayopendekezwa kwenye kata zote 3,800 nchini; ingawa hawajaona zozote, Katiba ya 1977 iliyobadilishwa na Rasimu ya Katiba toleo la pili ya Tume ya Katiba ambayo ina hoja za Ukawa. Kwenye kampeni hii, pepo za Katiba Mpya zitapata kasi na nguvu zaidi ya kimbunga cha Tsumani. Mtaji wa tatu wa wapiga kura na wananchi ni uwezo mkubwa na haki yao ya kidemokrasia ya kuandamana kwa kudumu kwa lengo la kuhakikisha uwepo wa Katiba Mpya ndani au nje ya U-EL; na hatimaye kuona kila neno lililoandikwa kwenye Katiba Mpya ndilo liwaalo. Changamoto kubwa ya wapiga kura hasa kwa Tanzania bara ni kujitokeza kwa uchache kwenye siku ya kupinga kura yumkini siyo wakati huu.
Vyombo vya hahari
Vyombo vya habari na wanahabari vina wajibu na jukumu la kitaaluma la kutoa habari sahihi kwa Wananchi bila woga pamoja na kufanya uchambuzi yakinifu ya matukio na mambo ya Uchaguzi Mkuu. Vyombo hivi vina mtihani mgumu wa kuachana na mambo ya siasa uchwara, kujibadilisha na kujipanga upya mbele ya falsafa hizi tatu na mabadiliko ya makundi ya kampeni ili viweze kutangulia, kuongoza jamii kwenye Uchaguzi Mkuu na hatimaye kwenye ushindani wa kasi ya maendeleo ya karne na milenia mpya. Vyombo vya habari vina jukumu na wajibu wa kuwa bega kwa bega na falsafa ya wapiga kura, Ukawa Asilia kwa sababu masilahi yao kwa kudumu yako kwa Wananchi vinginevyo watatoswa na kuteketea pamoja.
Tume ya Uchaguzi
Tume ya Uchaguzi imetwika mzigo mkubwa wa majukumu yenye kushinda uwezo wake. Tume siyo huru, imeegemea serikali ya chama tawala cha CCM na vyombo vya dola. Ilisukumiwa sura mbaya ya zigo la kusitisha mchakato wa Katiba mpya, kuendesha Uchaguzi Mkuu chini ya mashaka ya Katiba ya 1977 na sheria zake. Haina uwezo na utaalamu wa kumudu kikamilifu teknolojia mpya na tata wa BVR ambayo imetumika kutayarisha daftari ya wapiga kura, kudhibiti upigaji kura kwenye vituo 40,000 nchini na matokeo. Inabidi Tume ya Uchaguzi na vyombo vya dola vya mabavu vinavyotumika haswa polisi vibadilike na kuanza kuzingatia kwa ukamilifu maadili ya uhuru, demokrasia haki za binadamu za kimataifa za wananchi; vinginevyo watakuwa wahanga wa kwanza wa kubadilishwa kwa nguvu na pepo zinazovuma kwa nguvu.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu
Wahenga wamelonga, “ogopa wahesabu kura na siyo wapiga kura”. Katiba 1997 ya mashaka inatamka ‘ushindi wa mgombea urais ni kwa wingi wa kura na siyo kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa’; ‘hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa mgombea urais baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi’. Ushindi wa ubunge au udiwani na wingi wa kura. Vyama vya siasa pamoja na wapiga kura wamekuwa na mashaka kuhusu utashi wa Tume ya Uchaguzi wa kutoa matokeo ya haki na kweli. Matukio ya upigaji kura za wagombea ndani ya vyama vya siasa uedhibitisha kuwepo kwa michezo mchafu wa kupanga matokeo kwa njia mbalimbali za kilaghai. Itabidi makada wote wa vyama vya upinzani, U-EL na wapiga kura kuwa chonjo dhidi ya njama za kuvuruga matokeo kabla, wakati na baada ya kupiga kura. Ili kulinda amani, itabidi Tume ya Uchunguzi na vyombo vya dola husuka vihakikishe kwamba haki inatendeka na kuonekana kabla ya kutangazwa mshindi wa Urais, ubunge na udiwani.
Wajibu wa kudumu wa wananchi
Wananchi wanajua athari za falsafa za kutinga na kuingia Ikulu kwanza; mvinyo wa Ikulu ni mkali, mtamu na hulevya kupindukia. Kwa hali hii U-EL wanaweza wakasahau hoja na haja ya Katiba Mpya. Wananchi wapiga kura ndio pekee wenye utashi, jukumu na wajibu wa kuenzi falsafa yao na kuhakikisha uwepo wa Katiba yao mpya na bora na siyo kutegemea chama chochote cha siasa ikiwa ni pamoja na U-EL. Isitoshe, falsafa ya Wananchi ni kinzani na falsafa ya Ikulu kwanza na falsafa ya Ufisadi. Ili kuwa na uhakika wa uwepo wa Katiba mpya itabidi wapiga kura kuchukua tahadhari kubwa ya kuepuka kufuru ya kurudia makosa; kufanya mambo matatu yafuatayo kwa umahiri na uhakika. Kwanza, wapiga kura wahakiki uwepo wa ahadi na ratiba ya kuhakikisha uwepo wa katiba Mpya kwenye ilani ya U-EL au chama kingine. Ratiba ianze siku ya kwanza ya kampeni na siyo baada ya Uchaguzi Mkuu. Pili, wapiga kura watumie haki yao ya kidemokrasia na silaha ya maandamano ya kudumu tangu mwanzo wa kampeni hadi Katiba mpya imepatikana. Tatu, wapiga kura watumie silaha kuu iliyo mkononi mwao; kuwapa kura yao wagombea wa dhati wa Katiba Mpya. Wahenga wamelonga ‘Fimbo ya karibu ndiyo iuayo nyoka’. Chama na mgombea asiye na ahadi na ratiba ya Katiba mpya ndiye joka.
Hitimisho
Tuhitimishe kwamba suala la uwepo wa Katiba mpya ni jambo zito la kitaifa, la kufa au kupona na kamwe siyo kijigambo cha mchezo. Mambo yanayotokea kwenye kinyanganyiro cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015 ni mwendelezo ya mapambano ya kihistoria ya Wazalendo ya kujitambua na falsafa yao dhidi ya mafisadi waporaji kwa hali, mali na uhai kwa zaidi ya karne kumi na mbili. Baada ya Wazalendo kurejesha uhuru, vyama vya siasa vya TANU/ASP/CCM vilipora na kumiliki Katiba ya kidemokrasia ya utawala wa Wananchi, wakajijengea falsafa ya kutinga Ikulu milele na kuingia ubia na falsafa ya mafisadi waporaji. Kimsingi, ubia wa wanasiasa wa U-EL ni kung’oa CCM na falsafa yao ni kuingia Ikulu kwanza na mengine yatafuata; yumkini pamoja na kujali Katiba Mpya. Kwa hali yeyote ile, wapiga kura ndio pekee wenye wajibu na jukumu la kuhakikisha wanapigia kura mgombea na chama chochote chenye utashi, mkataba na ratiba bora. Wapiga kura wajitambue, kushikamana na kuandamana kwa kudumu hadi uwepo wa Katiba Mpya yao. Katiba mpya ndio chambo pekee cha kujenga maisha bora ya wananchi hapa duniani; asemaye vinginevyo ni wa kupuuza. kwenye karne na milenia mpya; nchi Ukawa Asilia na Vyombo vya habari kila mmoja kwa nafasi, taaluma na ubunifu wake wana wajibu wa kutangulia na kuongoza wapiga kura kwenye safari yao ya Katiba mpya. Bila shaka itakuwa kama Wahenga wamelonga “wengi wape, usipowapa watachukua kwa nguvu”.
Mwandishi wa makala haya, Dk. Godfrey Swai anapatikana kwa simu +255658661616
- See more at: http://raiamwema.co.tz/je-ukawa-lowassa-watahakikisha-katiba-mpya#sthash.MPU1cOCj.dpuf
No comments :
Post a Comment