Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Friday, August 21, 2015

Kikwete amjibu Lowassa 'kimtindo'.

Rais Jakaya Kikwete.
Rais Jakaya Kikwete, amefunguka na kusema hatishwi wala hashtushwi na maneno ya watu wanaosema serikali yake kwa miaka 10 haijafanya kitu.
 
Badala yake amesema kitakachomshtusha ni taarifa zozote za uchochezi kwa kutumia kivuli cha dini ama ukabila kwa kuwa vitu hivyo ni hatari na vinaweza kuliingiza Taifa katika machafuko.
 
Rais Kikwete aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipotembelea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora  (THBUB) na kuzungumza na watumishi wake ambao walitumia nafasi hiyo kumuaga.
 
Alisema watu wanaobeza mafanikio ya serikali yake hawezi kuhangaika nao kwa kuwa anajua kuna mafanikio mengi yamepatikana katika kipindi cha miaka 10 mpaka sasa na wanao uhuru na kusema chochote wanachotaka.
 
“Kuna watu wanasema sana serikali yangu haijafanya chochote, lakini hawa sitahangaika nao kwa kuwa najua kuna mafanikio mengi yamefanyika katika uongozi wangu,” alisema  Rais Kikwete.

Alisema mtu atakayehangaika naye ni yule atakayetoa kauli za kuashiria uchochezi kwa kutumia dini na ukabila kwa kuwa vitu hivi ni hatari kwa amani ya nchi na kwamba kwa hilo atakuwa mkali.

“Kuna uhuru wa kutoa maoni na kama kuna mtu anataka kusema au kukosoa serikali yangu, mimi sina tatizo na yeye aende hata pale Jangwani aseme siku nzima sina tatizo naye, lakini atakayejaribu kuleta uchochezi kwa kutumia dini na ukabila, huyo tutashughulika naye," alisema.Ingawa Rais Kikwete hakumtaja mtu yeyote, Julai 29, mwaka huu, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, anayegombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alisema kuwa Serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kuwapatia wananchi maendeleo.
 
Lowassa baada ya kuchukua fomu za kuwania urais, akiwahutubia wafuasi wa Chadema na wananchi katika ofisi za chama hicho mtaa wa Ufipa, Kinondoni, Dar es Salaam pamoja na mambo mengine, alisema Serikali ya Rais Kikwete imeshindwa kusimamia uchumi kiasi cha bei za vitu kupanda kila uchao vikiwamo vibiriti, mafuta na vyakula.
 
Katika ziara zake za kutafuta wadhamini kwenye mikoa ya Mwanza, Arusha, Mbeya na Zamzibar, Lowassa alirudia kauli hiyo na kusema kuwa Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa, ilisimamia vizuri uchumi kuliko Serikali ya Awamu ya Nne.
 
MIGOGORO YA ARDHI
Kadhalika, Rais Kikwete  jana alisema migogoro mingi ya ardhi hapa nchini inachangiwa na viongozi wasiokuwa waaminifu ambao wanajihusisha na rushwa na kwamba tatizo hilo kwa sasa linawakumba wananchi wa vijijini.
 
Alisema viongozi katika ngazi za vijiji na wajanja wachache, wanatumia uelewa mdogo wa wananchi kuwadhulumu haki zao, jambo ambalo linaleta ugomvi kati ya wafugaji na wakulima.
 
Alisema migogoro ya ardhi imeongezeka na imefika vijijini, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma na kwa sasa inasababishwa na watumishi wa umma wanaopokea rushwa wakati wa utoaji wa hati miliki ya ardhi.
 
“Utakuta kiwanja kimoja wamepewa watu watatu na kinachofanyika hapo ni mtu mmojawapo kuwahi kumwaga mchanga na mawe ikiwezekana na kuanza kujenga haraka,” alisema.
 
Aliisifu Tume ya Haki za Binadamu kwa kutetea haki za wanyonge na kwamba lazima waendelee kufanya hivyo ili nchi na wananchi wake wafurahie kuishi na yeye ataisadia.
 
MAUAJI YA ALBINO
Kuhusu mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino), Rais Kikwete alisema ni dhana ya kijinga na kikatili kuumua  binadamu mwenzako kwa imani kwamba viungo vyake vitakuletea mafanikio.
 
“Vijijini ,wauzaji wa pombe wanaamini kwamba wakiweka nywele za albino chini ya pipa, pombe yake itauzika kwa haraka na wavuvi wanaamini kwamba viungo vya mwili vikifungwa kwenye mtumbwi, watapata samaki wengi,” alisema.
 
ADHABU YA KIFO 
Akizungumzia adhabu ya kifo, Rais Kikwete alisema mpaka sasa hawajawahi kusaini ili wafungwa wakiwamo wa mauaji ya albino wanyongwe na kwamba hatafanya hivyo kwa kuwa utekelezaji wake ni mgumu.
 
Rais Kikwete aliaidi kuisaidia tume hiyo kupata fedha zaidi kabla hajaondoka madarakani ili itekeleze majukumu yake kwa kuwa Watanzania wanahitaji kupata haki zao za msingi bila kunyanyasika.
 
KAULI YA MWENYEKITI WA  THBUB
Naye Mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyaduga, alisema tangu kuanzishwa hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, Tume ilipokea malalamiko 26,818 ya uvunjwaji wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora, kati ya hayo 19,508 sawa na asilimi 73, yameshatolewa uamuzi ama kupatiwa ufumbuzi.
 
Hata hivyo, alisema malalamiko 7,310 sawa na asilimia 27 yako katika hatua mbalimbali za kupatiwa ufumbuzi ikiwa ni pamoja na kufuatilia kesi 14 zilizoko mahakamani.
 
Mbali na hayo, Tume inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa bajeti inayotokana na bajeti yenye ukomo mdogo hasa kwa mwaka 2014/2015.

CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment