WIKI iliyopita, Rais Jakaya Kikwete alifanya ziara ya kiserikali ya siku nne nchini Australia kwa mwaliko wa viongozi wa nchi hiyo. Mhariri wa Raia Mwema, Ezekiel Kamwaga, alipata fursa ya kufanya mahojiano naye kuhusu ziara hiyo na umuhimu wake kwa Tanzania. Endelea
RAIA MWEMA: Leo ndiyo umemaliza ziara yako ya kikazi ya siku nne hapa Australia. Je, kwa ufupi, unadhani umetimiza malengo uliyojiwekea kuyafanikisha katika ziara hii?KIKWETE: Ziara yangu hapa Australia ilikuwa nzuri na kwa kweli naweza kusema kwamba yote niliyotarajia kuyafanya nimeyakamilisha kwa asilimia 100. Nilikuja hapa kwa shughuli mbili kubwa; mosi kuitikia wito wa Gavana Mkuu wa nchi hiyo, Peter Cosgrove, aliyenipa mwaliko wa kiserikali kufanya ziara hapa na pili kupokea Shahada ya Heshima ya Uzamivu niliyotunukiwa na Chuo Kikuu cha Newcastle nchini hapa.
Kwa hiyo kwanza ziara hiyo imefanyika na pili nimeweza kutunukiwa tuzo yangu. Kwenye ziara hiyo nimekutana na Gavana Cosgrove na pia Waziri Mkuu, Tony Abbot pamoja na watu wa kambi rasmi ya upinzani nchini Australia.
Tanzania na Australia zina uhusiano wa muda mrefu na umetapakaa katika Nyanja nyingi.
Kwanza sisi sote ni wanachama katika Jumuiya ya Madola na pia tupo katika Umoja wa Nchi zilizo kwenye Kingo ya Bahari Kuu ya Hindi. Kwa sababu hii, tunashirikiana katika mambo mengi.
Tuko pamoja katika mapambano dhidi ya uharamia na ugaidi katika bahari yetu hiyo. Nchi hii pia inatusaidia sana katika kutoa mafunzo ya juu kwa vijana wetu kielimu. Kati ya mwaka 2007 na sasa, zaidi ya vijana wetu 230 wamepata ufadhili wa kusoma katika vyuo mbalimbali nchini hapa.
Aprili mwaka huu, vikosi vya baharini vya Australia vilikamata kilo 800 za madawa ya kulevya yaliyokuwa yakija Tanzania na wakatupa taarifa. Walipokamata waliyamwaga yote baharini na kiasi kile ni kikubwa na kama kingefanikiwa kufika nchini maana yake vijana wetu wangezidi kuharibikiwa na dawa hizo.
Lakini, Australia pia ina wawekezaji hapa nchini katika masuala mbalimbali kama ya gesi na mafuta na kwa sababu ni nchi tajiri, bado ina fursa ya kuleta wawekezaji wengi zaidi kwa ajili ya kuchochea uchumi wetu.
Hivyo, katika mazungumzo yangu na Gavana na Abbott, tuliyazungumza yote hayo; masuala ya uwekezaji, vita dhidi ya ugaidi na uharamia, elimu kwa maana ya vijana wetu na mambo mengine muhimu kwa ajili ya nchi zetu hizi mbili na namna ya kuboresha zaidi uhusiano wetu huo.
Kwenye suala la shahada ya heshima, kwa kweli niliwaeleza wakuu wa chuo kwamba nilipopata barua kutoka kwao ya kusema wamenipa heshima hiyo, nilishangaa sana. Australia ni nchi ya mbali sana kutoka kwetu Tanzania lakini mpaka wakajua kwamba tupo na kuna mambo mazuri tunafanya, maana yake ni kuwa wanatufuatilia.
Chuo Kikuu cha Newcastle ni kichanga kwa vile ndiyo kwanza kina umri wa miaka 50 lakini ni miongoni mwa vyuo vikuu 10 bora nchini hapa. Kinaheshimika kimataifa kwa tafiti na kwa vyovyote vile kuna jambo wameliona na ndiyo maana wakaamua kufanya walivyofanya kunitunuku.
Niliwaambia kuwa heshima ile waliyonipa si yangu, ni ya Watanzania wote. Haya mambo unaweza ukapewa wewe sifa lakini ukweli ni kuwa hufanyi mambo peke yako. Ni ushirikiano wa watu mbalimbali kwa ujumla na ndiyo maana nimesema naitoa heshima ile kwa Watanzania wote.
Tumezungumza kuhusu ushirikiano baina ya vyuo vikuu vya Australia na Tanzania katika masuala ya elimu na utafiti kwa sababu wenzetu wako mbali katika eneo hilo. Nikirudi nyumbani nitaandika barua ya kuwashukuru lakini nitasisitiza na kukumbusha kuhusu ushirikiano huo na Wizara ya Elimu sasa itatakiwa kufuatilia zaidi kuhusu huu uhusiano.
RAIA MWEMA: Hakukuwa na ajenda nyingine zaidi ya zile zilizo rasmi?
KIKWETE: Hahahahaa (anacheka), ajenda nyingine ilikuwa ni kuaga. Niliwaambia kwamba mwezi wa kumi mwaka huu kutakuwa na uchaguzi nchini kwetu na mimi nitaacha madaraka kwa mtu atakayechaguliwa na Watanzania.
Kama ningekuwa mcheza mpira, ningesema nakaribia kutundika daluga au kuweka viatu mchagoni. Nilichowaambia wenzetu hawa, kama ambavyo nimewaambia wengine nilikopita, ni kwamba mimi naondoka lakini natamani uhusiano na ushirikiano uliokuwepo wakati wangu uendelee pia kwa mrithi wangu.
Mimi nimepokea uhusiano huu mzuri kwa sababu ulianzishwa na watangulizi wangu; Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa. Wao wakaniambia kuwa rafiki yao ni Tanzania na hivyo uhusiano huu utaendelezwa kama kawaida.
Waliniuliza kidogo kwanini Tanzania imekuwa rahisi kubadilishana uongozi wakati wengine wanagombana kwa sababu hiyo lakini nikawaambia sisi tumekubaliana hivyo na kama wenzetu nao wamekubaliana kwenye mifumo yao, sisi hatuwezi kuwaingilia. Kila nchi ina utaratibu wake na wetu sisi ni wa kupokezana vijiti.
Cha msingi ni kwamba tumeona uhusiano wa nchi hizi mbili uko imara na atakayekuja baada yangu ataendelea pale nilipoishia mimi.
RAIA MWEMA: Ukisoma magazeti ya hapa inaonekana kama Australia inapita katika kipindi kigumu kiuchumi na mwelekeo wa serikali yao sasa uko katika kupunguza misaada na badala yake kujielekeza katika uhusiano wa kiuchumi. Je, tumejiandaaje na mabadiliko haya ya Australia?
KIKWETE: Kwenye uchumi, Tanzania inahitaji vitu vikubwa vitatu kwenye uhusiano wake na nchi zilizoendelea kama Australia. Tunahitaji wawekezaji, masoko ya kuuzia bidhaa zetu na teknolojia mpya katika uzalishaji. Haya ndiyo mambo ya msingi.
Mtu akikwambia kwamba uwezo wake wa kukusaidia umepungua, huwezi kumlazimisha akupe kilekile alichokuwa anakupa zamani. Hilo ni jambo ambalo haliwezekani. Maadamu wao wameamua kuwa na uelekeo mpya, la muhimu kwetu ni kuhakikisha kwamba tunafaidika pia na mabadiliko hayo.
Ndiyo maana kwenye ziara yangu ya hapa nimefuatana na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Dk. James Mataragio na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Juliet Kairuki kwa lengo la kuvutia wawekezaji zaidi katika maeneo mengine na pia kwenye gesi na mafuta.
Mingi ya misaada tunayopata inasaidia katika maeneo yasiyo ya ukuzaji uchumi. Mambo kama afya, elimu ni muhimu lakini hayakuzi uchumi na kuongeza ajira mara moja. Lakini, unapopata mwekezaji, kama ilivyokuwa kule Ngaka ambako kuna wawekezaji kutoka Australia, ajira zinaongezeka.
Kinachozalishwa kinauzwa na nchi inapata mapato yake kupitia kodi. Na yule anayenunua naye analipa. Sasa ukipata miradi mingi mikubwa, maana yake mapato yanaongezeka na tatizo la ajira pia linapungua kwa sababu wawekezaji wanahitaji watu ili wafanye shughuli zao.
Kwa ujumla, uwekezaji una faida nyingi zaidi kiuchumi kuliko misaada na sisi tumeliona hili na ndiyo tumeamua kuongeza nguvu katika kutafuta wawekezaji wa kimkakati ili tuweze kukuza uchumi wetu.
RAIA MWEMA: Kwenye mazungumzo yako na Waziri Mkuu Abbott mlizungumza pia kuhusu umuhimu wa mikataba inayonufaisha pande zote; kwa maana ya nchi husika na wawekezaji. Unadhani ni kwanini hili suala ni muhimu?
KIKWETE: Ndiyo tulizungumza lakini haya ni mambo ambayo yako kama mila kwenye masuala ya uwekezaji. Kuna mikataba ambayo ipo ambako watu wanakubaliana, kwa mfano, kwamba kama mwekezaji yuko katika nchi yako basi asitozwe kodi mara mbili. Yaani kule alikotoka na anakofanya shughuli zake.
Lakini kuna mikataba pia ambayo inahusu ukuzaji wa uwekezaji na ulinzi wa mali ya mwekezaji. Kwamba mnakubaliana kuwa kama mwekezaji wa nchi A akienda nchi B, ana uhakika wa kupata mambo kadhaa wa kadhaa na yanalindwa kwa mujibu wa sheria.
Haya ni baadhi ya mambo ambayo tuliyazungumza lakini ni ya kawaida na yanafahamika katika masuala haya ya uwekezaji.
RAIA MWEMA: Umeweka historia mbili za kipekee katika ziara yako hii ya hapa Australia. Kwanza umekuwa kiongozi wa kwanza wa bara la Afrika kualikwa kutembelea nchi hii tangu serikali ya Abbott iingie madarakani mwaka 2013 na pili umekuwa Mkuu wa Kwanza wa Nchi duniani kutunukiwa shahada hiyo ya heshima ya uzamivu na Chuo Kikuu cha Newcastle.
Je, matukio haya mawili yana maana gani kwako binafsi na kwa nchi yetu ya Tanzania?
KIKWETE: Hilo la kuwa kiongozi wa kwanza kutoka Afrika kualikwa na serikali ya Waziri Mkuu Abbott tangu aingie madarakani sikulijua mpaka nilipofika hapa. Sasa wao wenyewe watakuwa wanajua kwanini wameanialika mimi na si kiongozi mwingine kutoka katika bara letu.
Lakini, kwetu sisi hii ni sifa na heshima kubwa. Nchi yetu, tangu zamani, pamoja na umasikini wetu tumekuwa na heshima kubwa katika medani ya kimataifa. Kwenye lugha ya Kiingereza ningeweza kusema we have been punching way above our weight.
Kwenye miaka ya karibuni hapa, tumepokea viongozi wakubwa sana kimataifa kwenye ardhi yetu na kupata fursa ya kuongoza tukipewa nafasi za juu kwenye taasisi za kimataifa. Tunashindana na mataifa yanayotuzidi kwa mbali sana kiuchumi na kijeshi lakini siku zote tunabaki kuwa juu.
Haya ni mafanikio na mambo ambayo tunahitaji kuendelea kuwa nayo. Huku nje watu wanaiheshimu sana Tanzania, kila taifa kwa sababu zake binafsi na hili tupate maendeleo tunayoyataka ni lazima tuendeleze ushawishi wetu huu.
Kuhusu ile shahada, kama nilivyosema mimi sikuwa hata nakijua hiki chuo wakati nilipopokea barua ya kuniomba kukubali heshima waliyonipa. Wao pia ndiyo wanaojua hasa kwa nini waliamua kunipa mimi heshima hiyo; kiongozi kutoka katika taifa la Afrika na lililo mbali kutoka kwao.
Ni wazi, inaonekana kuna mambo tunayafanya vizuri. Ni matumaini yangu kwamba heshima niliyopewa na chuo hicho sasa itafungua milango kwa viongozi wengine duniani nao kupewa heshima hiyo kama ilivyokuwa kwangu.
RAIA MWEMA: Baada ya ziara yako hii na kwa mazungumzo ya kiuwekezaji ambayo umeyafanya ukiwa hapa, una ujumbe gani kwa sekta binafsi ya Tanzania?
KIKWETE: Wachangamke tu. Kuna fursa nyingi hapa Australia na kuna fursa nyingi zaidi nchini Tanzania. Ni matumaini yangu kwamba Kairuki atarudi Tanzania na kuwaambia wawekezaji kule kwamba kuna fursa za kibiashara na watu wa Australia.
Kama Mtanzania akipatana na mwekezaji kutoka Australia na wakakubaliana kwenye mambo ya msingi, maana yake ni kwamba wote watapata. Hii ndiyo aina ya uwekezaji tunaoutaka kuwa aliyeleta mtaji kutoka nje anafaidika na mwekezaji wa nyumbani naye anaondoka na kitu.
RAIA MWEMA: Umesema kwamba umetumia ziara hii kuaga kwa vile unamaliza muda wako wa uongozi katika kipindi cha miezi miwili ijayo. Je, una mpango wa kufanya nini ukistaafu?
KIKWETE: La kwanza kabisa nitakalofanya ni kupumzika. Muda ukifika na nikimwachia madaraka anayekuja, nitakwenda zangu kijijini kwetu Msoga kupumzika. Unajua hii kazi si rahisi, ni ngumu sana na inatumia muda, nguvu na akili yako yote.
Kuna watu wanafikiri pengine hii kazi ni rahisi lakini kama unawapenda watu wako na unaumizwa na hali yao na unapenda uwavushe, hii si kazi rahisi. Umekuja huku nje ya nchi na umeona mchakamchaka wa mikutano. Usiku wa kuamkia leo nimepata usingizi saa 11 alfajiri na sasa nazungumza nawe (saa tano usiku) na bado nina mambo mengine ya kufanya usiku huu. Ni lazima tu nipumzike kwanza.
Sasa nikishapumzika vya kutosha, naweza kuamua kufanya mambo mengine ya kusaidia nchi yangu. Nafikiri kwa uzoefu wa uongozi nilioupata na watu ambao nimekutana nao kwenye maisha yangu, bado naweza kutoa mchango kwa nchi yangu.
Nimepanga kuanzisha taasisi isiyo ya kiserikali itakayokuwa na kazi ya kushughulikia masuala ya watoto na kinamama. Inaweza pia kujihusisha na mambo mengine ya kimaendeleo lakini suala la utatuzi wa migogoro halitakuwepo kwenye ajenda za taasisi hiyo.
Kazi ya kusuluhisha migogoro naifananisha na watu wanaofanya kazi ya kuchonga majeneza. Mchonga majeneza, ili apate riziki, ni lazima watu wafe. Watu wasipokufa kwake inakuwa balaa. Ni sawasawa na kuwa na taasisi ya kutatua migogoro, kwa sababu kama migogoro haipo, basi na wewe huna kazi.
Ndiyo maana mimi sitaki kuwa na taasisi ya namna hiyo. Hata hivyo, kama kutatokea tatizo na watu wakaona pengine mimi naweza kusaidia kulitatua, na wakaniomba nifanye hivyo, nitasaidia. Hakutakuwa na tatizo lakini siwezi kukaa na kusema kazi yangu itakuwa kutatua migogoro.
Kwenye mkutano wa hivi karibu wa wakuu wa nchi za Afrika uliofanyika Afrika Kusini, mmoja wa viongozi wakubwa duniani alinifuata na kuniuliza, sasa ukistaafu utafanya kazi gani? Nikamwambia mimi nitapumzika tu.
Hapa duniani, hakuna kazi ya juu zaidi kama ya urais ambayo mimi nimeshaifanya. Siwezi tena kuandika barua ya kuomba kazi sehemu nyingine. Nadhani zaidi ya kazi za hiyo taasisi, pengine nitalima na kufuga kama ambavyo wanakijiji wenzangu wa Msoga wanafanya.
- See more at: http://raiamwema.co.tz/kikwete-sitaki-kuwa-mchonga-majeneza#sthash.OQi3YM8X.dpuf
No comments :
Post a Comment