Na Jenerali Ulimwengu
WIKI iliyopita niliandika kusema kwamba Edward Lowassa kuhama kutoka chama kilichomlea ilikuwa ni hatua ya kushangaza kuliko kuhama kwa wanachama wengine waliowahi kuwa katika chama tawala na kisha wakahamia vyama vya upinzani.
Ukweli huu unatokana na ukweli kwamba amekuwa ni mtu wa kwanza aliyewahi kuwa na wadhifa aliokuwa nao Lowassa kuondoka na kuhamia upinzani. Isitoshe, hatua aliyochukua inaonekana kama hatua inayoweza kutangaza mwisho wa ukiritimba wa kisiasa wa Chama Cha Mapinduzi, au hata mwisho wa chama hicho kuwa madarakani.
Hii imetokea vipi? Nitajaribu kurejea baadhi ya mambo yaliyojitokeza, kwa mitazamo ya muda mrefu, mitazamo ya muda wa kati na mitazamo ya muda mfupi.
Mosi, Lowassa amedai kwamba alichotendewa Dodoma wakati wa mchujo wa majina yaliyojitokeza hakikuwa haki pale jina lake lilipoenguliwa bila kupigiwa kura. Madai hayo ni ya kweli kwa sababu hakupewa nafasi ya kujieleza wala kukata rufaa.
Sote tutakumbuka kwamba ofisa mwandamizi wa CCM, Nape Nnauye alikwisha kutahadharisha kabla ya mchujo huo kwamba wale ambao wangeenguliwa wasingekuwa na wasaa wa kukata rufaa.
Kwa maana hiyo, yeyote ambaye angekatwa angekuwa ndiyo amefikia mwisho wa safari yake ya kutafuta kuteuliwa kuwa mgombea wa urais.
Kutoka kwa Lowassa CCM na kujiunga na upinzani kunadhihirisha kwamba walichotaraji wenzake ndani ya CCM (kwamba kuenguliwa kwa jina lake ndio ulikuwa mwisho wa safari yake kwenda Ikulu) hakikuwa sahihi. Kwa kitendo chake peke yake aliweza kuwadhihirishia kwamba hesabu zao hazikuwa sahihi.
Pili, ni kwamba ingawa Lowassa hakutendewa haki, lakini hakuwa peke yake katika kutotendewa haki. Walikuwa wengi, na baadhi yao wamelalamikia kitendo hicho cha kunyimwa haki. Lakini si wote walionyimwa haki wamejitoa katika chama hicho ingawa ni sahihi kuhisi kuwa kokote waliko hawana moyo mkunjufu juu ya chama hicho na uongozi wake wa juu, ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa chama, Jakaya Kikwete. Hilo ni katika mtazamo wa muda mfupi, takriban mwezi mmoja tu uliopita.
Lakini, tukitaka kuambizana ukweli tutakumbushana kwamba kutendeana haki si utamaduni wa chama hiki, si miongoni mwa viongozi, si baina ya viongozi na wanachama wao, na wala si viongozi kwa nchi wanayoitawala. Tukichukua mtazamo wa muda mrefu kidogo tu, tutakumbuka kwamba katika chaguzi zote zilizopita tangu mwaka 1995 majina ya watu yamekuwa yakienguliwa mara kwa mara bila maelezo ya kuridhisha.
Mwaka 1995, jina la Lowassa lilifikishwa mbele ya halmashauri kuu ya chama chake, lakini halikupigiwa kura. Kisa? Liliondolewa kwenye orodha ya wagombea 16 kwa sababu Mwalimu Julius Nyerere, ambaye hakuwa mwenyekiti wa chama na wala hakuwa mjumbe wa halmashauri kuu, alitilia shaka uadilifu wa Lowassa.
Katika mchakato wa mwaka huo, jina la John Malecela wala halikufika mbele ya halmashauri kuu. Kisa? Nyerere aliwatisha wazee fulani ndani ya chama kwa kuwaambia kwamba jina la Malecela lingeendelea kuwamo ndani ya orodha yeye angerejea Butiama siku hiyo hiyo. Kwa hiyo hakumtaka Malecela hata kuwamo miongoni mwa majina yaliyofikishwa mbele ya halmashauri kuu, na akafanikiwa.
(Hapa naweka parandesi fupi ili tutafakari hali ninayoieleza hapa na tuelewane vyema. Kama nilivyosema hapo juu, wakati huo, Nyerere hakuwa mwenyekiti wa CCM kwa sababu alikwisha kung’atuka mwaka 1990, na wala hakuwa mjumbe wa kikao hicho, ila alijialika, lakini tukashitukia akikiongoza kikao hicho.
Kisa? CCM ilikwisha kujiweka katika hali ya kutishwa na nguvu ya Augustine Mrema, mwanasiasa iliyemtengeneza kutokana na upuuzi wa ndani ya chama chenyewe na serikali yake. Chama kilihitaji msaada wa Nyerere ili kumshinda Mrema, na Nyerere akatoa masharti yake: Mkitaka niwasaidieni, waondoeni nisiowataka)
Tatu, chama-tawala kilikwisha kujiweka katika mazingira magumu kwa kukataa kuruhusu jambo ambalo mantiki yoyote ile inaliona ni la msingi: haki ya mwananchi yeyote kugombea nafasi yoyote bila kulazimishwa kuwa mwanachama wa chama chochote. Hili ni sula ambalo wengine tulilipigania kwa nguvu zetu zote, ndani ya Bunge na ndani ya chama, lakini likashindikana kutokana na fikra za kipuuzi zilizotanda ndani ya chama hicho.
Hata Nyerere hakufanikiwa kuushinda upuuzi huo. Alijaribu kuwapa mfano wa Herman Sarwatt, aliyekuwa mwana-TANU aliyeenguliwa mwaka 1960 ingawa watu wake walimpenda, na akasimama kama mgombea huru, akaishinda TANU lakini akaendelea kuwa mwana-TANU ingawa kulikuwa na vyama vya upinzani.
Upuuzi huo wa CCM wa kukataa mgombea huru ndio uliomzaa mtu anayeitwa Wilbroad Slaa, (tena aliyetokea maeneo hayo hayo ya Sarwatt) kwa sababu alishinda kura za maoni lakini akaenguliwa, na hivyo akalizimika kujiunga na upinzani. Laiti Slaa angeruhusiwa kuwa mgombea huru ingewezekana hata leo akawa mwana-CCM.
Na hivyo ndivyo ingetokea kama Lowassa angekuwa na upenyo huo.
Nne, CCM inatafunwa na utamaduni unaokubali nakisi ya kutisha ya mijadala ndani yake. Ni kama vile chama hicho kinahofia mijadala na badala yake kinafurahia misimamo isiyo na uchambuzi inayotolewa mara kwa mara lakini haina uwiano baina yake.
Nne, CCM inatafunwa na utamaduni unaokubali nakisi ya kutisha ya mijadala ndani yake. Ni kama vile chama hicho kinahofia mijadala na badala yake kinafurahia misimamo isiyo na uchambuzi inayotolewa mara kwa mara lakini haina uwiano baina yake.
Ndiyo maana unaweza kusikia viongozi wake wakikemea udini mahali fulani lakini ukawasikia wakiwa wadini wa kutupa mahali pengine. Leo tunasikia kauli za kikabila kutoka kwa baadhi ya hao hao wanaokemea ukabila mahali pengine. Nilikwisha kusema kwamba hali ya kuachana na itikadi inatengeneza mazingira ya mikanganyiko ya kifikra, kila mmoja akijisemea anavyojihisi.
Kama chama hicho kingekuwa na utamaduni wa mijadala ni dhahiri kingemjadili Mrema mwaka 1995 na kubainisha ni kwa nini kilitaka kumzuia kuwania urais badala ya kuweka sharti la kijinga kama lile la kumtaka mgombea urais kwa tiketi ya CCM kuwa na shahada ya chuo kikuu. Kama chama hicho kingekuwa na mijadala ya ndani kingeacha mjadala kuhusu wote walioenguliwa uwe wa wazi na kila mmoja aelezwe upungufu wake.
Kwa utaratibu huo angalau wajumbe wa vikao muhimu vya juu wangechambua na kujiridhisha juu ya sababu za kuengua jina la Lowassa, lakini pia sababu za kumkataa makamu wa rais, waziri mkuu, waziri mkuu mstaafu, jaji mkuu mstaafu, wakuu wa ujasusi wastaafu wawili na watu kama hao.
Wajumbe pia wangepewa uelewa mkubwa zaidi ni kwa nini wanachama waandamizi kama hao waliachwa mapema na badala yake naibu waziri akawa miongoni mwa waliosonga mbele.
Tano, hali ya kisiasa nchini ilikwisha kufikia hatua ya hamasa kubwa na katikati ya hamasa hiyo alionekana Edward Lowassa kama kiini chake. Wako waliodai kwamba alitumia fedha kuwavuta watu. Inawezekana, lakini ni wangapi waliotumia fedha na bado hawakupata kuamsha hamasa kama ya Lowassa?
Hii ndiyo hali isiyokuwa ya kawaida, hali ya mwanasiasa ambaye amejijengea mazingira ya watu kumkubali, kwa sababu moja au nyingine, kiasi kwamba anaonekana ni mkubwa kuliko chama chake, ambacho ni chama kilicho madarakani, na akaweza kukitikisa hadi kwenye mizizi.
Kuhusu kutotendewa haki, nimekwisha kusema kwamba wote walioachwa hawakutendewa haki, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kuhama chama. Tulikotoka haki haikutendeka, ikiwa ni pamoja na alivyofanyiwa Lowassa mwenyewe mwaka 1995 pamoja na Malecela; alivyofanyiwa Malecela mwaka 2005; alivyofanyiwa Salim Ahmed Salim mwaka 2005. Lakini waliotendewa hivyo hawakuhama chama.
Tofauti safari hii ni kwamba imetokea fursa iliyo wazi kwa mtu anayeona kaonewa kuondoka na kujiunga na mkondo wenye nguvu na unaoonkeana kama unazo chembechembe za ushindi. Upande wa pili tunaikuta nguvu iliyomo katika harakati za kutaka kuchukua dola lakini imekuwa ikikosa “kiki” moja ya nguvu ya kuiwezesha kuking’oa chama kilichomo madarakani.
Hii ndiyo hali isiyo ya kawaida, na hatua tunazozishudia si za kawaida sana, lakini zinaelezeka.
Itaendelea
- See more at: http://raiamwema.co.tz/lowassa-hali-isiyo-ya-kawaida-huibua-hatua-zisizo-za-kawaida#sthash.DEyUwFLJ.dpuf
No comments :
Post a Comment