Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Tuesday, August 18, 2015

Sanaa ya kuhama vyama na mustakabali wa demokrasia


SANAA ya kuhama vyama vya kisiasa (the art of defection from one political party to another) imeanza karne nyingi sana zilizopita. Wenzetu walioanzisha sanaa hii wameipa majina mengi sana kwa mfano cross - carpeting, crossing the floor, decamping na kadhalika.
Licha ya majina mbalimbali wote wanakubaliana kitendo hiki ni sanaa (art) kama zilivyo fani nyingine za sanaa. Sanaa hii inaweza kutumika vizuri lakini pia inaweza kutumika vibaya.
Je sanaa hii huchagizwa na nini?
Kwa kawaida kuna vivutaji (pull) na visukumaji (push).
Mosi: Kwa kawaida chama cha siasa ni ushirika (association) unaoundwa kwa dhumuni moja kuu: kutwaa madaraka kwa mujibu wa sheria kwa nguvu zake chenyewe au kwa kushirikiana na chama au vyama vingine vya kisiasa. Chama cha siasa kikiona kwa nguvu zake chenyewe dhumuni hili haliwezi kufikiwa hujaribu kushawishi viongozi au wanachama walio katika chama au vyama vingine wahame huko walipo na wajiunge nacho
Ushawishi huu unawezekana kutekelezwa kwa njia za halali na njia za haramu pia. Kwa mfano njia halali ni pamoja na kuweka sera nzuri za kuvutia na kuboresha demokrasia ndani ya chama.

Njia za haramu ni pamoja na kuhonga vyeo au fedha, kuhujumu kazi za chama kingine hata kama zina manufaa kwa umma, kusema uongo, kuhadaa na kupotosha ukweli. Hili likitokea basi chagizo hapa ni aina ya kivutaji (pull factor).
Pili: Chama kinachokimbiwa kushindwa kudumisha demokrasia ndani yake au kushindwa kukidhi matarajio mema na/au maovu ya wanachama wanaotaka kuhama. Tuanze na hili la demokrasia.
Chama cha siasa ndio kioo cha demokrasia katika jamii hivyo basi ni lazima chama cha siasa kiisimike demokrasia ya kweli ndani yake au ndani ya mjumuiko wake na chama au vyama vingine. Kusimika demokrasia ni muhimu kwa kuwa kuna msemo wa kiingereza unasema ‘you cannot give what you do not have’!
Yaani huwezi kuwapa wengine kile usichokuwa nacho! Ikiwa wanachama wanaona ndani ya chama chao demokrasia haipo wataifuata huko ambapo akili yao inawaambia ipo.
Kwa kawaida wanachama wanaohama kutafuta demokrasia ya kweli huwa na chuki ya dhati dhidi ya chama wahamacho na mapenzi ya dhati kwa chama wanachohamia.
Ikiwa mwanachama anahama kwa kuwa chama hakina demokrasia ya kweli chama anachotoka kinapaswa kuingiwa hofu na chama ahamiacho kinapaswa kufurahi.
Lakini ikiwa mwanachama au wanachama wanahama chama ambacho demokrasia ya kweli imeshamiri basi chama kinachohamwa ni heri kimharakishe au kiwaharakishe wahame.
Ni mamluki hao. Chama kinachowapokea hakipaswi kukenua. Kinapokea mamluki wa kisiasa. Mara nyingi mhamo wa aina hii unashadidiwa na vivutaji (pull factor).
Tuangalie sasa suala la kushindwa kukidhi matarajio mema au maovu. Katika siasa kila mwanachama au kiongozi ana matarajio ya aina mbili: kama binadamu na kama mwanachama.
Hakuna mtu anaingia chama au kugombea uongozi kukidhi mahitaji ya chama tu. Ni kujidanganya. Lazima mtu atarajie kutimiziwa matarajio yake binafsi na ya chama. Tatizo ni pale mtu anapoweka matarajio yake binafsi kama kipaumbile.
Pia tatizo linakuwepo pale mwanachama anapotaka atekelezewe matarajio yake hata kwa mbinu chafu. Kwa hiyo chama cha siasa ni lazima kihakikishe kinawapatia wanachama wake matarajio yao kama binadamu na pia kama wanachama huku kikitoa kipaumbile kwa matarajio mapana ya chama na wanachama.
Ikitokea mwanachama au wanachama wakahama kwa kuwa tu matarajioyao binafsi hayakupewa kipaumbele au njia zao chafu hazikupewa nafasizifanye kazi chama kinachohamwa ni vyema kikawapatia visa haraka wasafiri! Ni wachumia tumbo hao.
Chama kinachowapokea kinapaswa kuchukua tahadhari kubwa mno. Wahamaji hao hawakawii kuambukiza wenyeji. Taratibu chama kilichowapokea kitakuta wanachama wake hata wale wa awali wanatukuza matarajio binafsi.
Tatu: kuna wakati nguvu za nje (external force) ya vyama vya siasa hutumika kuchagiza uhamaji. Mara nyingi nguvu hizi za nje zinatoka kwa makundi ya wafanyabiashara, wahalifu na serikali za nje ambao wanaona maslahi yao (mengi yenye athari mbaya kwa taifa) yatatimia kama watakipeleka chama fulani au mtu fulani kushika dola.
Dalili kuu ya kuwepo makundi haya katika uhamaji ni matumizi makubwa ya fedha katika kuhama au kugombea madaraka hasa kipindi cha uchaguzi mkuu. Ikitokea hivi chagizo zote mbili yaani visukuma (push) na vivuta (pull) vinakuwa kazini. Kama hutaki kuvutwa utasukumwa! La msingi ni utoke chama A kwenda chama B.
Ne: Ili wanachama na viongozi wawe kitu kimoja na wakae pamoja milele lazima pawepo na itikadi inayowagundisha (binding ideology). Ni sawa ndani ya ndoa kama mume anaamini katika uislam na mke katika ukristo ni nadra wawili hao kudumu pamoja.
Wakidumu pamoja ni kwa kujilazimisha. Vicheko na saa ingine hata watoto na wageni hupungua. Ni vigumu sana kujua itikadi ya hivi vyama vyetu. Hujui ni capitalist, labour, democrat, liberal, green, fashist, kingdom au socialist!
Maana yake wanachama wanajiunga bila kujua itikadi hasa ya chama ni nini? Sawa na kupanda basi Ubungo lakini abiria huyu anadhani linaenda Mbeya, aliyekaa siti pembeni anadhani linaenda Arusha, wa siti ya mwisho anadhani linaenda Handeni na dereva anadhani abiria wote ni wa Mwanza!
Mfano nzuri ni chama kinaitwa TLP (samahani msee babaangu)! Hii ni Tanzania Labour Party isiyo na agenda yoyote ya ki Labour au mahusiano yoyote na vyama vya wafanyakazi na shirikisho lao TUCTA!
Hebu waulize TLP ina agenda au mkakati gani wa kuhakikisha mikataba (conventions) za ILO (International Labour Office) zenye kusimamia viwango vya ajira (Labour Standards) zinaridhiwa (ratified) na kuingizwa kwenye sheria za nchi (domesticated)? Ndipo utajua hii ni labour party ya aina yake.
Waulize TUCTA hivi TLP ina mahusiano gani na nyie usikie maneno! Sasa hii Labour Party inawakilisha wafanyakazi na waajiri wa wapi?! Nimetolea mfano wa TLP lakini ni hali katika vyama vyote.
Chama kikikosa itikadi imara kinakosa gundi (super glue) ya kuwaweka wanachama wake pamoja. Kuhamwa ni rahisi. Wahamaji hawana itikadi ya kisiasa. Itikadi yao inageuka mtu au fedha au cheo! Alipo mtu, ilipo fedha au palipo na nafasi ya cheo inakuwa ndio itikadi!
Tunaona sasa jinsi wa itikadi hii wasivyo na haya! Mmoja kasema hadharani kabisa eti “mimi nimekaa cheo hicho hicho miaka wenzangu wamekuja wamenipita”! Akahama!
Huko alikoenda inabidi wasome somo! Hata wakimpa cheo wahakikishe hatakaa cheo hicho muda mrefu lazima apandishwe ngazi! Tena asipitwe hata na anayemzidi utendaji la sivyo patahamwa!
Napenda niweke wazi kuwa kuhama toka chama kimoja ni haki ya kikatiba (au sheria). Lakini mie si mtumwa wa Katiba! Ni katiba hiyo hiyo inalalamikiwa hata na wahamaji, wanaohamwa au wanaopokea wahamaji. Haki kuwepo kwenye katiba ni suala moja lakini kuwa haki hiyo ni halali ni swala lingine.
Si katiba yetu inaruhusu kunyonga mtu hadi kufa? Mbona kuna wengi tu hawakubali kuwa ni sahihi? Na kama wanaoshupalia kuwa haki ya kuhama chama ni ya kikatiba na lazima iheshimiwe tulipataje ujasiri wa kufanya jaribio la kuibadili kupitia BMK?
Kwangu mimi katiba lazima ikidhi mahitaji mapana ya jamii. Na sisemi katiba yetu ipige marufuku watu wasihame vyama! La hasha! Ninachopinga ni uhamaji huu usio na sababu za kidemokrasia au usimikaji wa haki.Uhamaji unaotokana na watu kuweka mbele maslahi binafsi au unaohatarisha mustakabali wa taifa tuukatae.
Kuna watakaodhani ‘aa anayeathirika sasa ni chama A acha watu wahame watakavyo’!. Inawezekana si chama A kitajachoathirika bali taifa zima. Na wala hakuna ajuae kuwa kabla na baada ya oktoba kuwa hatuwezi kuona hawa wanahama toka Mashariki kwenda Magharibi na wale wanatoka magharibi kwenda mashariki! Ikawa vurugu mechi hadi wanaodhani watanufaika wakawa ndio walalamikaji wakuu.
Tumeanza kuona watu walioamini kujumuika pamoja mambo yatanyookasasa mambo yanaanza kuvurugika. Tarajio lao la umoja wenye nguvu linaweza kuwatumbukia nyongo.
Hivi Mungu pishilia mbali mgombea urais wa chama B akiamua kutumia uhuru wa kuhama au akishawishiwa kuhama katikati ya kampeni itakuwaje? Bado watu watadai ni haki yake?
Lakini hatari kuu ni usalama na mustakabali wa taifa. Na ningependa kurejea tukio la wenzetu kule Nigeria. Wengi wetu tumeaminishwa kuwa kikundi cha Boko Haram kilianzia misikitini na madrasa. Ukweli ni kuwaBoko Haramu ilizaliwa na uhamaji vyama vya siasa.
Kule Nigeria almaarufu kwa jina decamping (kuhama kambi). Hata sasa Tanzania tunasoma vijana wakihimizana watu kuhama kambi! Ni hivi ilivyotokea: Chama cha PDP (PEOPLES DEMOCRATIC PARTY) kilichokuwa madarakani kilishindwa kusimamia demokrasia ndani ya chama.
Katiba ya Nigeria inaruhusu ugawaji wa ukuu wa nchi kwa ujimbo wao wanaita “zoning”. Rais Yar Dua (marehemu mungu amrehemu) alikuwa mwislam kwa kuwa kwa mtindo huu wa zoning ilikuwa zamu ya Waislam (Kaskazini) kutoa rais.
Akafariki kabla ya kumaliza kipindi chake na kwa mujibu wa katiba yao‘kipindi cha waislam’. Ndani ya chama Mkristo Goodluck Jonathan akaona bahati (goodluck) iliyoje! Akapoka urais. Waislam ndani ya PDP wakaamua kuhama na muda huohuo ikaanzishwa BOKO HARAM!
Boko Haram ni matokeo ya ukosefu wa demokrasia ndani ya chama! Hebu jiulize iweje Boko Haram wasumbue muda wote huu katika nchi yenye jeshi kubwa kabisa Afrika? Iweje Boko wapakie watoto kwenye convoy la malori na wasafiri zaidi ya kilomita 200 bila kuzuiwa?
Sasa sisi Tanzania tunaandaa mazingira mazuri ya kutengeneza maboko yetu. Na wanasiasa wetu na si waumini wa dini ndio watatuletea miboko! Kwenye chama tawala tumeshuhudia malalamiko kibao kuhusu rushwa kwenye michujo.
Watu wamepigana hadi wameungwa mkono na Naibu Spika! Ama kwa hakika CCM ina demokrasia ya hali ya juu ukilinganisha na wengine isipokuwa maksi hizo hupungua hadi - 0 (negative zero) wakati wa teuzi na uchaguzi!
Lakini vyama vya upinzani navyo vinaugua ugonjwa huu tena kwa kiwango cha kutisha. Hebu jiulize ni vipi mtu aliyetangazwa kiwanjani katika list of shame anapokewa na kupewa nafasi ya kugombea bila kushindanishwa na yeyote?
Hii ni demokrasia ya Sanya Juu au Iramba? Leo hii kiongozi aliyepigana kufa kupona hadi mkewe akatoka mimba amewekwa kando anaambiwa apumzike akiamua arudi! Hivi Mzee Slaa angekuwa na uwezo au utashi hawezi kuanzisha kiboko haramu chake?
Si tumesikia wenyewe wakidai mluteri kaingia mkatoliki out! Ndugu zangu wa CHADEMA nimewasikia mara kadhaa wakilaumu utaratibu wa bungeni wa kupiga kura kwa spika kuuliza wanaokubali waseme ndiooooo! Wengi tuliwaunga mkono.
Lakini kwenye mkutano wao mkuu pale Mlimani City ndio utaratibu ‘Spika’ wao aliotumia kuidhinisha wateule! Tena ‘Spika’ huyu nadhani ni baada ya kutonywa akatolea ufafanuzi utaratibu uliotumika!
Akadai ndio utaratibu wa chama! Nikajiuliza hivi kule bungeni hawajui ni utaratibu wa bunge?! Kuna mtu nyuma ya ukumbi alipiga kura ya ‘hapana’ mwenyekiti akasikika akisema kwa kufoka ‘anasemaje huyoo’!
Uvunjifu huu wa demokrasia ni hatari kwa mustakabali wa taifa. Hivi CDM na UKAWA watakuwa na udhu tena kule bungeni kupinga kupitisha miswada kwa kusema ndioooo?! Wenzao watawaambia “kule Mlimani City je?”
Nitoe mfano wa CUF! Kwenye ule mkutano Seif Hamad bila kuulizwa alitoa ufafanunuzi kuhusu habari kuwa Lipumba amejiuzulu. Alikanusha na kudai yeye ndiye Katibu Mkuu na jana yake alikuwa na Profesa hadi usiku saa nne.
Haikupita muda Lipumba akatangaza kuwa na mkutano na waandishi wahabari kesho yake! Hivi kwa picha hii kuna demokrasia ndani ya CUF? Katibu Mkuu anasema hili Mkiti anasema lile! Hatuoni hatari ya watu kuvamia ofisi kutaka kujua Mkiti wao anataka kuongea nini?! Hapawezi kuzaliwa kaboko siku moja?
Vyama vyetu hasa hivi vya upinzani vimegeuka kuwa Premji Manji and Sons Ltd! Au Msangi and Makande Enterprise Ltd ! Arawa and Mbeke Brothers Ltd! Vimegeuka kuwa mali binafsi! Hakika ndivyo vimeminya demokrasia kuliko hata chama tawala.
Nihitimishe makala hii kwa kutoa angalizo: kuhama chama ni haki ya kikatiba lakini si haki ya kuzaliwa. Haki hii itumike kukuza demokrasia na si kufifisha demokrasia, kuhatarisha usalama wa nchi au kukidhi mahitaji finyu ya mtu au kikundi cha watu.
Tusiruhusu maadui wa nje watumie haki hii kuliyumbisha taifa. Vyama vyote vya siasa vichukue hatua madhubuti kujenga uhamaji wenye mashiko. Uhamaji unaochochewa na itikadi na si ushabiki, uroho wa madaraka au cheo.
Asikiaye na asikie lakini naamini muda ni mwalimu mzuri.
Waasalam


- See more at: http://raiamwema.co.tz/sanaa-ya-kuhama-vyama-na-mustakabali-wa-demokrasia#sthash.tYXGCc6i.dpuf

No comments :

Post a Comment