STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 12 Septemba, 2015
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Vijana wasomi wametakiwa kuifahamu vyema na kuzingatia historia ili kuelewa sababu za kuanzisha mapambano ya uhuru dhidi ya wakoloni na hatimae waweze kujenga mustakabala endelevu wa nchi.
Wito huo umetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein wakati akizungumza na Wanafunzi wa Shirikisho la Vyuo Vikuu Zanzibar huko katika Ofisi Kuu ya CCM Zanzibar.
Aliwaeleza vijana hao kuwa historia ya Zanzibar inaonesha kuwa wananchi wake walijitawala wenyewe kabla ya kuja wakoloni hivyo Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa halali kwa kuwa yalirejesha uhuru wao wa kujitawala.
Aliwataka vijana hao kusambaza ujumbe wa kihistoria unaoeleza namna wazee walivyopambana na wakoloni hadi kulazimika kufanya Mapinduzi mwaka 1964.
Dk. Shein alisisitiza kuwa Mapinduzi ya mwaka 1964 yalikuwa halali na kuongeza kuwa Mapinduzi hayo yalifanyika kwa manufaa ya watu wote bila ya ubaguzi.
Katika mnasaba huo alieleza kuwa ndio maana mara baada ya kufanyika Rais wa Kwanza wa Zanzibar Sheikh Abeid Amani Karume alichukua hatua za haraka kuondosha ubaguzi ikiwemo kutoa elimu bure, matibabu bure pamoja na kutangaza ardhi kuwa mali ya serikali.
Alibainisha kuwa hata jumuiya ya vyuo kama ya vijana hao isingeweza kuwepo kwa kuwa sio tu kwa sababu elimu yenyewe ilikuwa ya kibaguzi lakini pia hata vyuo vyenyewe havikuwepo.
Aliwapongeza vijana hao zaidi 350 waliowakilisha wenzao wa vyuo vyuo 13 kwa kuandaa mpangomkakati madhubuti wa kukipatia ushindi Chama cha Mapinduzi na kueleza kufanya hivyo ni kutekeleza dhamira ya chama hicho kuwatumikia wananchi.
Dk. Shein ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, alisema chama hicho kiko tayari kwa uchaguzi na kina kila sababu ya kushinda kama ilivyofanya katika chaguzi zilizopita.
Aliongeza kuwa anaamini kuwa wananchi wa Zanzibar wamekiamini chama hicho na ndio maana wamekuwa wakiiunga mkono na kukipa ushindi mara zote.
Aliwataka vijana kwenda kila kona ya Zanzibar mijini na vijijini kufanya kampeni ili kukipa ushindi chama hicho na katika kufanya hivyo wasione aibu wala kuchoka kwani hata kura moja inaleta ushindi.
Katia riasla yao iliyosomwa na Katibu Mkuu wa shirikisho hilo Kassim Salum Abdi, vijana hao walieleza kuwa wamejiandaa vya kutosha kushiriki uchaguzi kwa kuhakikisha CCM inashinda.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Shirikisho hilo Kitaifa Bi Zainab Abdallah Issa alieleza kuwa vijana wa vyuo vikuu wana kila sababu za kumuunga mkono Dk. Shein kutokana na sifa zake na kwamba shirikisho limejipanga vilivyo kuendesha kampeni za nguvu hadi Dk. Shein na CCM ipate ushindi.
Postal Address: 2422 Tel.+255 776 613 015, Fax: 024 2231822
E-mail: saidameir@ikuluzanzibar.go.tz & sjka1960@hotmail.com
/ZanziNews
No comments :
Post a Comment