Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amesema kama wananchi watampa ridhaa atahakikisha serikali yake inatunga sera ya kuhakikisha nyumba za nyasi zinaondolewa nchi nzima.
Ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakazi wa mji wa Kigoma katika mkutano wa hadhara wa kampeni uliofanyika viwanja vya Community Center ikiwa ni siku ya sita tangu alipoanza ziara ya kuomba kura mikoani kwa wananchi.
Lowassa ameshafanya mikutano ya kampeni katika baadhi ya majimbo yaliyopo mikoa ya Iringa, Njombe, Ruvuma, Rukwa, Katavi na Kigoma na leo anaendelea na ziara yake katika mkoa wa Tabora.
Alisema iwapo wananchi watamchagua na kuwa Rais wa awamu ya tano suala la ujenzi wa nyumba bora litazingatiwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha nyumba zote za nyasi zinaondolewa ili Tanzania iweze kufanana na mataifa mengine.Kuhusu wakimbizi waliopo mkoani Kigoma, alisema wamepata taarifa kuwa wakimbizi hao wamepewa vistisho kwamba wasipoipigia kura CCM watanyang’anywa uraia wa Tanzania.
Alisema kutokana na hali hiyo wamemtuma aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha, afuatilie suala hilo.
“Hakuna serikali inayoweza kusema usiponichagua nitakunyang’anya uraia, mkinipata kura nitafanya mabadiliko katika nchi yetu ili kila mtanzania aone mabadiliko katika maisha yake,” alisema.
Lowassa alisema kama wananchi watamchagua serikali yake haitataka kusikia suala la michango katika shule na badala yake elimu itakuwa bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu.
Aliongeza kuwa ushuru wa mazao utaondolewa kwa wakulima na wataruhusiwa kuuza mazao yao nje ya nchi bila ya kuwekewa vikwazo vyovyote na kilimo cha umwagiliaji kitaboreshwa ili kuongeza ajira nchini.
Aliwaeleza wananchi wa Kigoma kuwa tatizo la usafiri katika Ziwa Tanganyika analifahamu hivyo serikali yake italipatia ufumbuzi haraka na uvuvi utaboreshwa uwe wa kisasa.
Lowassa aliahidi kujenga bandari ya kisasa mkoani Kigoma pamoja na kujenga reli ya kati na kwamba kama reli itakayojengwa na serikali ya sasa itakuwa haina viwango itachimbuliwa na kujengwa mpya.
Aidha, aliahidi kuwa serikali yake itajenga viwanda vya mawese ili kuwawezesha wakulima kupata soko la uhakika la zao hilo na hivyo kuongeza ajira.
DAVID KAFULILA
Kwa upande wake Mbunge wa Kigoma Kusini anayemaliza muda wake, David Kafulila alisema CCM hivi sasa kimekuwa ni chama ambacho hakikubaliki na maaskofu, masheikh na wapagani .
Alisema CCM imepoteza uhalali na ndiyo maana Serikali ya Marekani imezuia Dola za Marekani milioni 700 na Ulaya Dola za Marekani milioni 500 kwa ajili ya miradi ya Mileniaum Challenge (MCC) kwa kuhofia zitatafunwa.
Kafulila alisema Lowassa ana kila sababu ya kuwa rais wa awamu ya tano kwa kuwa ana uwezo wa kuwaunganisha wananchi wa dini zote.
Alisema kashfa ya Richmond ambayo CCM wanaitumia kama rungu la kumsema Lowassa kimsingi lilishafafanuliwa kwamba mhusika mkuu wa suala hilo anajulikana.
Aliwashangaa baadhi ya viongozi wa CCM ambao wanasema wana nyaraka za Richmond lakini kwanini hawakuzitoa tangu awali hadi wahubiri wakati wa uchaguzi mkuu.
Kafulila alisema hakuna mpinzani atakayeiondoa CCM nje ya Ukawa.
MBOWE
Naye Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, alisema bado siku 50 taifa hili liandike historia Watanzania watafanya maamuzi kuhusu ustawi wa taifa lao.
Alisema Kigoma ni miongoni mwa mikoa ambayo imepokea mageuzi toka mwaka 1993 na kutoa wabunge wa upinzani hivyo ushirika wa Ukawa utafanya maamuzi ya kufanya mabadiliko Oktoba 25, mwaka huu.
Mbowe alisema yeye kama Mwenyekiti amefanya kila jitihada kuviunganisha vyama vya upinzani ili viweze kuiondoa CCM madarakani ambayo imelifanya taifa kama la kilio.
Alisema Ukawa walipoamua kumchukua Lowassa baadhi ya watu walihoji suala hilo lakini lengo ni kutaka kuleta mabadiliko ambayo Watanzania wanayahitaji.
Aliongeza kuwa itakuwa ni haramu kwa mtu anayetumia nguvu kufifisha mabadiliko yanayohitajiwa na Watanzania wengi ambao wamechoshwa na serikali ya CCM.
“Kazi ya kuleta mabadiliko haiwezi kufanywa na Lowassa peke yake lakini kuna vikosi ambavyo vitapita mikoa yote nchi nzima mpaka kuhakikisha CCM inalala katika uchaguzi wa mwaka huu’’,alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment