Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amemaliza ngwe ya kwanza ya kampenzi zake za kuomba ridhaa ya Watanzania katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na Kusini mwa Tanzania kwa kupokelewa na umati katika mikutano yake iliyojaa hotuba zenye ahadi ya kuleta mabadiliko.
Llicha ya Dk. Magufuli kudhihirisha kukubalika na wengi waliojitokeza kwenye mikutano yake, CCM kitalazimika kufanya kazi ya ziada ili kuwanusuru wagombea ubunge katika baadhi ya majimbo yaliyo kwenye mikoa hiyo.
MAJIMBO MAGUMU
Majimbo yaliyo katika hali ngumu yalijidhihirisha wakati Dk. Magufuli aliyekuwa akishangiliwa muda wote kulazimika kutumia muda mwingi 'kuwabembelezea' kura wagombea ubunge.
Maeneo mengine Magufuli alilazimika kuwaombea msamaha kutokana na tuhuma mbalimbali dhidi ya wagombea hao. Maeneo mengine Dk. Magufuli alilazimika kuahidi ajira kwa waliobwagwa katika harakati za uteuzi wa wagombea ndani ya CCM ili kupoza makali ya mgawanyiko uliozaa makundi yanayotishia ushindi katika Uchaguzi Mkuu, Oktoba 25.Changamoto ilianza kujitokeza katika mkoa wa Rukwa Jimbo la Kalambo ambalo mgombea wake ni Josephat Kandege.
Dk. Magufuli alilazimika kutumia kipaji chake cha ushawishi kumnadi mgombea huyo huku akiahidi kutoa ajira kwa waliokuwa wamegombea naye na kukatwa katika mchakato wa kura za maoni ndani ya chama.
"Ndugu zangu, hatuchagui malaika bali binadamu mwenye mapungufu yake, naomba nimuombee msamaha mgombea huyu. Inawezekana yapo aliyowakosea, msameheni na mumpe kura za ndiyo. Nikiwa rais kazi zipo nyingi, alimradi uwe mchapakazi. Mliogombea naye msiwe na wasiwasi. Nitawapa nafasi, muungeni mkono CCM ishinde jimbo hili," alisema Magufuli katika moja ya hotuba zake.
Katika Jimbo la Kwela ambalo mgombea wake ni Ignus Malocha, Dk. Magufuli alilazimika kuzungumza kwa matamshi yenye sauti ya ushawishi wa hali ya juu kuomba radhi kwa niaba ya mgombea na kuwasihi wananchi kusahau ya zamani na kumchagua.
Katika mkutano uliofanyika eneo la Laela, kila mgombea aliposema "Malocha oyee...!", mwitikio ulikuwa hafifu lakini lilipotajwa jina la Magufuli, wananchi waliitika kwa shangwe kubwa.
Jimbo la Sumbawanga Mjini, lililomsimamisha Aeshi Hilaly, zinahitajika nguvu ya ziada licha ya mwitikio mkubwa wa wananachi walioujaza uwanja kumshangilia Dk. Magufuli kuliko mgombea ubunge.
Dk. Magufuli alikuwa na kibarua kizito chakumuombea kura mgombea huyo na kulazimika kutumia hekima za mahubiri ya kiroho kwa nia ya kuweka mambo sawa.
"Ndugu zangu Mungu anatutaka tusamehe saba mara sabini. Kila mmoja kwa imani ya dini yake amsamehe mgombea huyu kama kweli lipo alilokosea. Tukumbuke hatuchagui malaika bali binadamu mwenye mapungufu yake, nipeni huyu nitafanya naye kazi katika kuleta mabadiliko bora na siyo bora mabadiliko," alisema.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda, hakupokelewa vizuri na wananchi wa jimbo lake huku wakimshangalia zaidi Dk. Magufuli.
Baadhi ya wananchi wa Mbinga wanadai kuwa tangu mgombea huyo apate nafasi ya Ukamanda wa UVCCM, hakuwahi kurudi kwao na kushirikiana nao.
Mgombea wa Jimbo la Momba, Dk. Lucas Siyame aliyewahi kuwa waziri katika kipindi cha kwanza cha Rais Jakaya Kikwete, alikuwa katika wakati mgumu wa kutokubalika kwa wananchi hatua iliyomlazimu
Dk. Magufuli kutumia nguvu ya mvuto wake kumuombea msamaha huku akirudia kauli yake ya mara kwa mara kuwa 'hawachagui malaika bali binadamu mwenye mapungufu kama wao'.
Hata hivyo, katika kuonyesha umahiri wake kisiasa, Magufuli anayejulikana kama 'tingatinga' alifanya kazi ya kunadi sera zake huku akisistiza kuwa maendeleo hayana chama na akawaomba kura wafuasi wa Chadema na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF) ili aingie Ikulu kuleta mabadiliko bora na maendeleo yenye kuwajali maskini.
Jimbo la Lupa linalogombewa na Victor Mwambalaswa wananchi katika mikutano walionekana kumshangilia kwa nguvu Dk. Magufuli . Lilipotajwa jina la mgombea ubunge, baadhi waliguna na kumpinga.
Jimbo la Rungwe lililomsimamisha Sauli Amon linaonekana kuwa katika mvutano mkali wa chinichini baina ya mgombea huyo na aliyeshika nafasi ya pili katika kura za maoni CCM, Richard Kasesela. Licha ya kupanda jukwaani na kumuhakikishia Dk. Magufuli kuvunja makundi, bado hakuficha hisia zake kwa kutaka hatua zichukukiwe dhidi ya viongozi wa CCM wa wilaya na mkoa walioshiriki kuathiri mchakato wa uteuzi wa wagombea wa chama chao.
Dalili si nzuri katika Jimbo la Namtumbo kwa mgombea Injinia Edwin Ngonyani, ambaye wakati ananadiwa alipiga magoti kuomba kura, Dk. Magufuli alilazimika kuendelea na kazi yake ya kumuombea msamaha.
Jimbo la Lulindi lenye mgombea Jerome Mbwanahusi linatakiwa nguvu ya ziada kurudi kwa CCM kutokana na wananchi kuonyesha kutomkubali wakidai kutoridhishwa na maendeleo ya mradi wa maji.
MAJIMBO HAYA CCM INACHEKA
Tofauti na majimbo mengine yanayoonyesha ugumu kwa wagombea, majimbo ambayo CCM haitatumia nguvu katika kampeni la Ludewa mkoani Njombe, lililomsimamisha Deo Filikunjombe.
Mgombea huyo ambaye amefanya kazi nzuri na ya kuigwa katika jimbo na mara nyingi ameonekana akishiriki kazi za mikono za wananchi kuchimba barabara, kuweka nguzo za umeme kwenye maeneo ya vijiji.
Ujenzi wa shule, zahanati kwani mbali na kutoa fedha zake, za mfuko wa jimbo na nyingine za wahisani, ameshiriki kazi mbalimbali na wananchi hao bila kujali nafasi aliyonayo wala fedha alizonazo.
Kati ya mikutano iliyofanyika kwenye makao makuu ya wilaya na kufana kwa wananchi kuonyesha furaha zao kwa wagombea wa urais na ubunge, jimbo hilo ni mojawapo na mara zote alipojitokeza waliimba kwa kumshangalia “Mbunge!Mbunge!jembe! jembe”.
Jimbo jingine ambalo CCM iko vizuri ni Mtwara Mjini lililomsimamisha Husnen Murji, ambaye anaungwa mkono na wananchi wengi.
Murji amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa kipindi kilichopita na katika vurugu za sakata la gesi, Mtwara za mwaka 2013 alikuwa upande wa wananchi wake kwa kutaka ajira zinazotolewa kuwanufaisha wananchi wake badala ya wanaotoka mbali.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment