Maalim Seif alirejesha fomu hizo na kumkabidhi Mwenyekiti wa Zec, Jecha Salim Jecha.
Maalim Seif ambaye ni Katibu Mkuu wa CUF na Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK), aliwasili katika ofisi hizo za tume, saa nne asubuhi akiwa na msafara wake wa kawaida ukiongozwa na askari wa Jeshi la Polisi na Usalama wa Taifa.
Baada ya kukabidhi fomu hizo, mgombe huyo ambaye anaegombea nafasi hiyo kwa mara ya tano, alisema kuwa ni matumaini yake kuwa Zec itafanya kazi zake kwa uadilifu ili uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu uwe huru na haki.
“Matumaini yangu ni kuwa mtakuwa waadilifu katika suala hili la uchaguzi mkuu ili uwe huru, haki na uwazi,” alisema Maalim Seif mbele ya mwenyekiti na watendaji wa tume hiyo.
Maalim Seif ambaye aligombea nafasi hiyo mfululizo kuanzia mwaka 1995, 200, 2005, na 2010, alichukua muda usiozidi dakika kumi na kukamilisha taratibu zote za kuwasilisha fomu hizo kisha kuondoka katika ofisi za Zec.Miongoni mwa viongozi wachache wa CUF waliomsindikiza kiongozi huyo ni Mwakilishi wa Jimbo la Mjimkongwe, Ismail Jussa Ladhu; Mwakilishi wa Jimbo la Magogoni ambae pia ni Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdilahi Jihadi Hassan; Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Fereji; Naibu Wazi wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Zahra Ali Hamad na Afisa wa Uchaguzi wa CUF, Mhene Said Rashid.
Maalim Seif amekuwa mgombea wa kwanza wa urais kurejesha fomu kati ya wagombea 15 waliochukua fomu hizo.
Ikiwa mgombea huyo atapitishwa na Zec atachuana na wagombea kutoka vyama 14 vya siasa.
Wagombea hao ni pamoja na Rais wa sasa wa Zanzibar, Dk Ali Muhammed Shein, ambaye anatetea nafasi yake kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM); Hamad Rashid Mohammed (ADC); Mwajuma Ali Khamis (UPDP); Juma Ali Khatib (Tadea); Said Soud Said (AFP); Mohammed Masoud Rashid (Chauma) na Abdallah Kombo Khamis (DP).
Wengine ni Tabu Mussa Juma (Demokrasia Makini); Kassim Bakari Juma (Jahazi Asilia); Issa Mohammeed Zonga (Sau); Khamis Iddi Lila ACT - (Wazalendo); Seif Ali Iddi (NRA); Ali Khatib Ali (CCK) na Hafidh Hassa (TLP).
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment