Mbashiru Ngete akikaribishwa na ndugu zake katika uwanja wa ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jana baada ya kuwasili kutoka Mecca, Saudi Arabia.Picha na Omar Fungo
Dar es Salaam. Wakati kundi la kwanza la mahujaji 112 wa Tanzania likiwasili nchini jana kutoka Makka nchini Saudia Arabia walikokwenda kwenye Hijja, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa imetoa majina ya mahujaji 18 ambao hawajulikani walipo.
Hadi jana iliripotiwa kuwa jumla ya mahujaji waliokufa waliotoka katika nchi mbalimbali duniani walikuwa wamefikia 769 wakiwamo Watanzania watano na waliojeruhiwa ni 934.
Mahujaji hao 112 waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa mbili asubuhi kwa Shirika la Ndege la Qatar.
Wengi wa mahujaji na ndugu zao walionekana wakitokwa na machozi ya furaha wakifurahi kuungana tena na familia zao.
Kwa mujibu wa wizara hiyo kwa umma, majina ya mahujaji ni Abdul Iddi Hussein, Awadh Saleh Magram, Burhani Nzori Matata, Yussuf Ismail Yusuf, Saleh Mussa Said, Adam Abdul Adam, Archelaus Antory Rutayulungwa na Farida Khatun Abdulghani.
Wengine ni Rashida Adam Abdul, Hamida Ilyas Ibrahim, Rehema Ausi Rubaga, Faiza Ahmed Omar, Khadija Abdulkhalik Said, Shabinabanu Ismail Dinmohamed, Salama Rajabu Mwamba, Johari Mkesafiri Mwijage, Alwiya Sharrif Salehe Abdallah na Hafsa Sharrif Saleh Abdallah.
Wizara hiyo juzi ilisema inaendelea kufuatilia hatma ya mahujaji 32 wengine ambao hadi sasa hawajulikani walipo.
Ilisema kuwa wizara imepokea taarifa za kutambuliwa kwa mwili wa hujaji mmoja wa Tanzania, Hadija Shekali Mohamed wa kikundi cha Ahlu Daawa.
Taarifa ya wizara hiyo ilisema kuwa Serikali ya Saudi Arabia imetoa picha za maiti za mahujaji waliokufa Makka kwa ajili ya utambuzi.
Ubalozi wa Tanzania Saudi Arabia kwa kushirikiana na Tanzania Hajj Mission na vikundi vya mahujaji wanaendelea kuhakiki sura za kwenye picha hizo ili kubaini kama zinalingana na mahujaji waliopotea. Taarifa hiyo ilisema mamlaka ya Serikali ya Saudi Arabia imesema imechukua alama za vidole za mahujaji waliokufa ili wazilinganishe na zile walizozichukua uwanja wa ndege wakati wakiingia.
Mmoja wa mahujaji waliorejea jana, Bashiru Ali Ngete alisema siku ya hijja kulikuwa na joto na msongamano.
No comments :
Post a Comment