Kwarara Msikitini

airbnb

Dual Citizenship #2

Dual Citizenship #2

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

Mwanakwerekwe shops ad

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Wednesday, September 30, 2015

Polisi wasambaratisha utafiti wa wagombea urais mitaani!

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas.
By Mussa Juma
Arusha. Wakati tafiti za kienyeji zenye lengo la kupima kukubalika kwa wagombea urais, hasa Dk John Magufuli na Edward Lowassa zikizidi kuongezeka, polisi jijini hapa mwishoni mwa wiki walitumia nguvu kutawanya vijana waliokuwa wakiendesha kura za maoni kwenye stendi ndogo ya mabasi na soko kuu.
Tangu kutangazwa kwa matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi za Twaweza na Ipsos, vijana kwenye maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko, hasa sokoni na kwenye baa wamekuwa wakiendesha tafiti zao za kienyeji wakiwa na lengo la kuonyesha hali halisi ilivyo mitaani tofauti na matokeo ya tafiti hizo mbili.
Katika tafiti hizo za Ipsos na Twaweza, Dk Magufuli, ambaye anagombea urais kwa tiketi ya CCM, alikuwa mbele ya Lowassa anayegombea kwa tiketi ya Chadema na vyama vinavyounga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini matokeo hayo yamepingwa vikali na wadau mbalimbali, huku yakiamsha tafiti za kienyeji mitaani.
Katika tukio lililotokea mjini Arusha, vijana walikuwa wakiendesha utafiti wao kwenye soko kuu la Arusha na eneo la kituo kidogo cha mabasi, lakini polisi walifika na kuwatimua wakidai wanavunja sheria. Wafanyabiashara hao wa soko hilo na stendi ndogo, waliandaa maboksi mawili ya kura, moja likiwa limeandikwa “Magufuli” na jingine “Lowassa”.
Baadaye walialika watu kwenda kupiga kura.
Kila aliyepita katika eneo hilo alielezwa utaratibu wa kupiga kura na alitumbukiza karatasi yake katika boksi lililoandikwa jina la mgombea anayeona anafaa kuwa rais.
Utafiti wa stendi ndogo ulikamilika baada ya muda na ulionyesha matokeo ya wagombea hao (tunayo).
Wakati watu waliokuwa stendi ndogo wakiendelea kushangilia matokeo hayo, wafanyabiashara wenzao wa soko kuu walikuwa wakiendelea kupiga kura na ghafla polisi walipofika maeneo hayo na kuwatimua vijana waliokuwa wakikusanya kura.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema waliokuwa wanafanya utafiti huo walikiuka sheria na kwamba kitendo chao kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani kwa kuwa kulikuwa na watu wasioafikiana.
Aliwataka wakazi wa Arusha kuacha kufanya mambo ambayo hayana manufaa, badala yake wasubiri siku ya kupiga kura.
“Huo ni utafiti wa aina gani wa maboksi?” alihoji alipoulizwa kuhusu tukio hilo.
“Hizi ni vurugu za mitaani. Tunawaomba wananchi watulie, wasubiri siku ya uchaguzi wapige kura kwa amani.”
Hili ni tukio la pili la utafiti unaofanywa kienyeji mitaani baada ya wafanyabiashara wa Kariakoo, Dar es Salaam kuendesha utafiti wao kwa kuruhusu watu kumpigia kura mgombea wanayempenda kati ya Magufuli na Lowassa.
Mbali na utafiti huo wa wakazi wa Dar es Salaam, kwenye maeneo mengine nchini kumekuwapo na watu wanaoendesha tafiti kama hizo zenye lengo la kujua ni mgombea gani wa urais anakubalika zaidi.
Wakati vijana hao wakifanya tafiti za kienyeji mitaani, wadau mbalimbali wamekuwa na maoni tofauti kuhusu kushamiri kwa vitendo hivyo.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa na gazeti hili wamesema kuanzishwa kwa tafiti hizo kunasadia kupata matokeo halisi ya joto la uchaguzi katika maeneo husika, huku wataalamu wa tasnia hiyo wakieleza kuwa ni matokeo ya kufeli kwa mfumo rasmi wa ufanyaji tafiti za kisayansi kutokana na misukumo ya kisiasa.
Mkazi wa Tabata, Isaiah Salmon alisema kutokana na taasisi zilizoaminiwa na wananchi kutofanya kinachotakiwa, yupo tayari kujitokeza kushiriki tafiti za mitaani hata kama Serikali inazikataza.
Alisema inasikitisha kuona mashirika makubwa kama Twaweza yanatoa matokeo ambayo hayaendani na hali halisi katika mwenendo wa siasa nchini.
Salmon alisema anaona Dk Magufuli na Lowassa wanachuana katika kampeni zinavyoendelea, lakini matokeo ya utafiti wa taasisi hizo ni tofauti.
“Unakumbuka wakati wa uchaguzi kule Kenya tulikuwa tukipata matokeo ya tafiti zilizokuwa zikibainisha Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wanaachana kwa kiasi kidogo na ndivyo ilivyokuwa mitaani. Hata matokeo ya uchaguzi yalivyotoka yalionyesha kama tafiti zilivyosema,” alisema.
Pamoja na kuanza kushamiri kwa tafiti hizo, baadhi ya wananchi wanatatizika na masuala ya kisheria na kanuni za uchaguzi na pia kukosa imani na watu wanaoendesha tafiti hizo ambazo mara nyingi ni vijana wa maeneo yenye watu wengi kama sokoni au stendi.
Mjasiriamali, Telesphory Ndomba alisema yupo tayari kushiriki katika tafiti hizo, lakini hana uhakika na uhalali wa matokeo yanayotolewa na watu wanaoweka maboksi hayo kama ni kweli ya au yemetiwa chumvi.
“Tuna uhakika gani wale wanaochukua hayo maoni watawasilisha inavyotakiwa? Mimi sijajua iwapo taratibu na kanuni za uchaguzi zinaruhusu kufanya tafiti hizo za wananchi, lakini hata nikiziona na nikashiriki bado siwezi kujua kama taratibu hizo zimefuatwa na aliyetangazwa, kashinda kweli au la,” alisema.
Alisema pamoja na taasisi za kitafiti kuonekana zina upungufu katika kazi zao, bado wana uhalali wao na kwamba tafiti za mitaani zinafanyika kwa sababu wananchi wengi, akiwamo yeye, “wamechoshwa na ahadi hewa zisizotekelezeka hivyo wana hamu ya kufanya mabadiliko”.
Hata wakati baadhi wanaona kushiriki utafiti huo unaozidi kushamiri mtaani kama haki ya msingi, Emilia Masaka (29), alisema haoni kama kuna umuhimu wa kushiriki tafiti hizo.
“Binafsi utaratibu huo mimi sina kwa sababu nina kazi zangu nyingi za kufanya kwa sasa. Sina nafasi kabisa kushiriki hizo tafiti zao. Ila kama ningekuwa na nafasi ningekwenda tu kuwaangalia ila siyo kushiriki,” alisema Masaka anayefanya kazi katikati ya jiji.
Mtafiti kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Patience Mlowe alisema hatua ya wananchi kuanzisha kura zao maoni juu ya chama au mgombea atakayeshinda urais, ni ishara tosha kuwa hawana imani na tafiti zinazotolewa na mashirika mbalimbali wakati huu wa Uchaguzi Mkuu.
Mlowe alieleza kuwa tafiti nyingi zilizofanywa hivi karibuni zinaonekana kuwa na msukumo wa kisiasa kwa kuwa watafiti walitumia muda mwingi kuzielezea wakati kitaalamu inabidi mwananchi wa kawaida azielewe bila kufafanuliwa au kuachwa na maswali lukuki yasiyo na majibu.
“Hayo ni matokeo ya kuwa na tafiti zisizotoa hali halisi inayoendelea katika mchakato wa uchaguzi na wananchi hawakupata matokeo halisi, ndiyo maana wameanzisha tafiti zao.
“Tafiti za aina hii tuzitegemee tu katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuwa wananchi hawana imani na tafiti zinazotolewa,” alisema Mlowe.
Alisema iwapo watu wanaoshirikishwa katika tafiti hizo za wananchi ni wakazi wa maeneo husika na wana sifa za kupiga kura, hapana shaka kuwa matokeo yanayopatikana yatasadifu hali halisi siku ya kupiga kura ambayo ni Oktoba 25.
Pamoja na tafiti zinazofanywa na wananchi kutoonekana ni za kitaalamu bado huenda zikaendelea kufanywa zaidi nchini kwa kuwa zinasadifu hamu ya kupiga kura iliyopo miongoni mwa wananchi kama alivyoeleza, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Damian Shumbusho.
“Huu utaratibu wa wananchi kufanya tafiti zao kwa kupiga kura sokoni na vijiweni unaonyesha bayana wananchi wamepata mwamko wa kushiriki uchaguzi. Wanaona siku ya uchaguzi inacheleweshwa hivyo wanatafuta matokeo ya haraka haraka,” alisema Shumbusho kutoka Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.
Alisema tafiti za kupima kukubalika kwa vyama na wagombea zinaweza kuwakatisha tamaa au kuwaongezea mori wapiga kura wakati huu wa uchaguzi na hazitakiwi kutegemewa sana kwa kuwa muda zinaofanywa siyo sahihi na siasa zinabadilika mara kwa mara.
“Kitendo cha wananchi kusema hizo tafiti tupa kule ni sahihi kwa sababu zimechokoza wananchi walipopanga kupiga kura baada ya kusikia sera za wagombea,” alisema.
Ofisa habari wa Twaweza, Risha Chande alisema kitendo cha wananchi kufanya tafiti zao mitaani ni jambo jema kwa kuwa kinaonyesha wana hamu ya kushiriki katika tafiti mbalimbali za kitakwimu jambo ambalo halikuwapo hapo awali.
Chande alisema pamoja na wananchi hao kuonyesha hamasa ya maswala ya kitakwimu bado, methodolojia wanazotumia haziwezi kutoa matokeo halisi ukilinganisha na tafiti za kisayansi zinazohusisha uchaguzi makini wa sampuli za kutafiti.
“Lazima tufuate utamaduni wa kuangalia au kujihakikishia mambo hasa maswala ya kitakwimu na hilo ni jambo letu kama taasisi.
“Sasa kama ukiwa na ugomvi na kitu lazima utachukua hatua kama waliyofanya wananchi hao ila tutambue kuwa kuna tofauti nyingi baina ya utafiti wao na ule wa kwetu,” alisema.

No comments :

Post a Comment