Tukio hilo lilimlazimisha mgombea urais wa Zanzibar kupitia Cuf, Maalim Seif Shariff Hamad, kukatisha hotuba yake na kuwatuliza wafuasi wake waliokuwa wakiwazomea wafuasi wa CCM wakati wakitangaza matangazo hayo.
Kufuatia tukio hilo, mkutano huo ulikatishwa na kusababisha wafuasi na wananchi waliiohudhuria mkutano huo kuondoka kwa kuhofia usalama wao.
Mapema, mgombea huyo alisema endapo atakuwa rais wa Zanzibar ataimarisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema serikali hiyo itakuwa na uwiano wa uongozi kati ya vyama viwili vitakavyoiunda kuanzia ngazi ya juu hadi chini zikiwemo nafasi ya masheha (viongozi wa mitaa).
Aidha, alisema viongozi wa serikali kama makatibu wakuu hawataruhusiwa kuingia katika siasa kama ilivyo sasa.
Alisema serikali atakayoiongoza, itatenda haki kwa watu wote bila kujali dini, rangi, ukabila na itikadi za kivyama na kudumisha amani ya nchi ili kuleta maendeleo.
“Chini ya serikali nitakayoiongoza nitahakikisha najenga umoja na kutenda haki sawa kwa watu wote bila ya upendeleo,” alisema.
Alisema hatomvumilia mtu yeyote atakayejaribu kutaka kuvunja mariadhano ya serikali ya umoja wa kitaifa na anakae thubutu kufanya hivyo atakiona cha moto.
Naye Mkurugenzi wa mawasiliano wa timu ya ushindi ya chama hicho, Ismail Jussa Ladhu, akizungumza na waandishi wa habari jana, alilaani kitendo kilichofanywa na wafuasi wa CCM cha kukatisha hotuba ya mgombea urais wa Cuf wakati akiwa katika mkutano huo.
Alisema kuwa kitendo hicho cha wafuasi wa CCM kupitia katika eneo hilo la mkutano na kutoa matangazo ya uzinduzi wa kampeni wa CCM alikiita ni kitendo cha uchochezi.
“Wamefanya makusudi inakuaje wapite tulipo sisi na kutoa matangazo yao wakati njia zipo nyingi za kupita hiki tunakiita ni kitendo cha hujuma na uchochezi,” alisema.
Aidha, alisema kitendo hicho kilichofanywa na CCM ni kukiuka maadili ya uchaguzi ambayo walikubaliana na kuyasaini mbele ya tume ya uchaguzi.
Alisema muongozo wa maadili ya uchaguzi umeweka bayana kwa vyama vya siasa kuacha kufanya vitendo vya uchochezi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment