Alitoa ahadi hiyo jana katika viwanja vya CCM, Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu wakati wa mwendelezo wa mikutano yake ya kampeni mkoani.
Alisema iwapo ataingia Ikulu serikali yake itajitahidi kutengeneza mazingira mazuri kwa wafanyakazi ili watulie ofisini na kuwatumikia Watanzania.
“Nataka watu wakae maofisini wafanye kazi ya kuwatumikia watanzania badala ya kwenda kuangalia miradi yao kutokana na hali ngumu ya maisha," alisema.
Alisema ataboresha maslahi ya askari polisi, wanajeshi na walimu kwa kulipa malimbikizo na marupurupu yao ili waweze kuishi maisha mazuri kama watumishi wa kada zingine.
Dk. Magufuli alihidi kuwa serikali yake itahakikisha inashusha bei ya vifaa vya ujenzi kama bati, saruji, nondo ili wananchi wa kawaida wamudu kununua na kuendesha shughuli zao.
Alisema atahakikisha serikali yake inaondoa ushuru ambao umekuwa kero kwa wafanyabiashara wadogo hasa mamalishe na watu wa bodaboda ambao kila kukicha wanahangaishwa.
“Nitashusha ushuru wote ambao si rafiki kwa watanzania maana haiwezekani mamalishe kaweka chakula chake pale anahangaishwa hangaishwa, mtu amekata miwa yake anaenda kuuza anakamatwa kamatwa bila sababu za msingi, mimi sitakubali uonevu mnichague ili niwaondolee kero hiyo,” alisema Dk. Magufuli.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Taifa (CCM), Abdalah Bulembo, alimwelezea mgombea huyo kuwa ni mtu mwadilifu ambaye hajawahi kuwa na kashfa yoyote ya ufisadi.
Bulembo alisema Dk. Magufuli ni mtoto wa mkulima ambaye anajua shida za watanzania hivyo wamchague kwa kura nyingi za ndiyo ili aweze kutatua kero zao.
Akiwaomba kura wananchi wa Lamadi, mkoani Simiyu, Dk. Magufuli, aliwataka watumishi wazembe serikalini wanaochelewesha na kukwamisha maendeleo ya wananchi waanze kutubu kabla hajaingia Ikulu.
Alisema anataka matatizo ya wananchi yatatuliwe kwa wakati, hivyo serikali yake haitavumilia utaratibu wa njoo kesho na kwamba watumishi ambao wamezoea kufanyakazi kwa mazoea wajipange upya.
Dk. Magufuli aliyasema hayo baada ya kuelezwa na mgombea ubunge jimbo la Busega (CCM), Dk. Raphael Chegeni, kuwa kuna mradi mkubwa wa maji kwenye mji huo wa Lamadi ambao umekwama kutokana na ukosefu wa Sh. milioni 100.
Alisema haiwezekani halmashauri ya wilaya hiyo ikakosa kiasi hicho cha fedha ili kutatua kero ya maji na kumtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo kutafuta fedha hizo haraka ili kukamilisha mradi huo.
“Leo hii nakuomba mkurugenzi lakini nikija tena nikiwa rais sitakuomba nitakuagiza na nadhani mnajua mimi nikiagiza huwa naagiza kwa namna gani maana nikisema nimesema sitakagi kubabaisha,” alisema.
Mgombea ubunge wa jimbo la Busega (CCM), Dk. Chegeni alisema wananchi wa Lamadi wanateseka muda mrefu kutafuta maji wakati kuna mradi mkubwa ambao umekwama kutokana na kukosekana Sh milioni 100.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment