Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, akikagua sehemu ya Mtambo wa kuchakata gesi asilia wa Madimba – Mtwara hivi karibuni. Picha na Blog ya Hivisasa.
Dar es Salaam. Utafiti mpya umeonyesha kuwa asilimia 80 ya wananchi wanataka mapato yatakayopatikana kwenye mauzo ya gesi asilia yatumike kwa ajili ya kuboresha huduma za afya na elimu.
Matokeo ya utafiti huo uliolenga kujua msimamo wa Watanzania kuhusu matumizi ya gesi asilia, uliofanywa na Taasisi ya Repoa kwa ushirikiano na Kituo cha Maendeleo Duniani (CGD) umeonyesha pia kuwa wananchi wanataka uwazi kwenye mikataba inayohusu rasilimali hiyo.
Rais wa CGD, Nacy Birdsall alisema utafiti huo uliowahoji watu 2,000 kutoka wilaya zote nchini kati ya mwaka jana hadi June mwaka huu, umeonyesha wananchi wanataka fedha zitakazopatikana zitumike kuboresha huduma muhimu na zitakazobaki zihifadhiwe.
“Wananchi wangependa kuona baadhi ya fedha zinahifadhiwa, serikali isianze kukopa ikitegemea kulipa madeni kutokana na fedha zitakazotokana na gesi asilia,” alisema Birdsall.
Mtafiti kutoka CGD, Mujobu Moyo aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wamesema ni vyema gesi hiyo ikachimbwa kuliko kuendelea kukaa ardhini na kupongeza uamuzi wa serikali uliochukuliwa.
Aliongeza kuwa taasisi hizo ziliwakusanya wananchi 400 jiji hapa kwa ajili ya kufanya mahojiano kuhusu gesi asilia ambapo pia walikutana na watunga sera.
Kwa upande wake Mwanauchumi nguli nchini, Profesa Ibrahim Lipumba aliyeshiriki mkutano huo, alisema wananchi wanapenda mikataba ya gesi asilia iwe wazi ili wakitaka kuisoma wapewe fursa hiyo.
“Wanataka kujua serikali imekubaliana nini na kampuni za nje,” alisema Profesa Lipumba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Profesa Samuel Wangwe alisema funzo kubwa lililopatikana katika utafiti huo ni kuwa wananchi wanapenda kuhusishwa katika mambo mbalimbali yanayowahusu.
No comments :
Post a Comment