Miongoni mwa waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa ambaye pia ni baba wa mgombea Ubunge wa Jimbo la Ukonga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Jerry Silaa.
Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, alisema jana kuwa Filikunjombe na watu wengine watatu waliokuwamo kwenye chopa hiyo wamepoteza maisha baada ya chopa waliyokuwa wakisafiria kuanguka na kuwaka moto.
Kamishna Chagonja alisema tukio hilo lilitokea jioni (juzi) katika mbuga ya Selous, eneo la Msolwa. Alisema muda kamili wa kutokea kwa tukio hilo bado haujafahamika kwakuwa iliangukia porini na eneo hilo halina mawasiliano, lakini watu walioshuhudia walisema ni jioni.Chagonja alisema timu ya upelelezi ya polisi kwa kushirikiana na mamlaka ya anga inafuatilia tukio hilo pamoja na kubaini majina kamili ya watu wawili. Alisema bado wanafuatilia zaidi kujua mmiliki wa chopa hiyo.
Taarifa nyingine zilizothibitishwa na Zitto Kabwe ambaye ni rafiki wa karibu wa marehemu Filikunjombe zilieleza kuwa miili ya marehemu iliwasili saa 12:00 jioni jana na kwamba, yote imepelekwa na kuhifadhiwa kwenye Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
Ilelezwa zaidi kuwa miili hiyo ilikuwa imeungua vibaya na hivyo haikuwa rahisi kuitambua, ingawa Filikunjombe alitambuliwa mapema kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni saa aliyokuwa ameivaa.
Kamishna Chagonja alisema taarifa zaidi kuhusiana na ajali hiyo zitatolewa leo baada ya kupokea ripoti kamili kutoka kwa wataalamu waliokwenda katika eneo la ajali.
NDUGU WAZUNGUMZA
Kadhalika, akizungumza na Nipashe jana, Msaidizi wa Jerry Silaa, alisema walipata taarifa za kutokea kwa kifo hicho jana majira ya saa 7:00 mchana.
“Jerry Silaa hawezi kuzungumza na simu kutona na hali iliyotokea. Taarifa ya kifo tumeipata kutoka kwa Kamishna Chagonja,” alisema msaidizi huyo wa Jerry Silaa.
Kaka wa Filikunjombe, Dominic Haule, aliiambia Nipashe jana kuwa taarifa za vifo hivyo, walizipata kutoka kwa Jerry Silaa.
“Taarifa tulizonazo hadi sasa ni za Jerry Silaa ambazo zimeenea mitandaoni. Walipata ajali wakiwa wanne na wote wamepoteza maisha.
Dominic aliongeza kuwa yeye alikuwa ni miongoni mwa abiria waliokuwa wasafiri na marehemu lakini alibanwa na kazi nyingine na hivyo akanusurika.
“Naomba uwaeleze watu kuwa mimi sijafariki dunia kwa sababu ni miongoni watu niliotakiwa kuwamo kwenye safari hiyo lakini nilibanwa na kazi nyingine mkoani Mwanza,” alisema Haule.
Alisema wanaodhaniwa kufa ni waliokuwa kwenye chopa hiyo ambao ni pamoja na kaka yao mkubwa, Casablanca Haule Filikunjombe, ambaye alisafiri badala yake. Alisema abiria mwingine alikuwa ni rafiki yao, Egid Mkwera, ambaye alikuwa ni Ofisa Mipango wa Musoma.
“Huyu rafiki yetu alitoka Musoma jana (juzi), akanifuata Mwanza nikamkatia tiketi ya ndege ili amuwahi Filikunjombe uwanja wa ndege na kweli alimkuta na kuanza kusafiri wote...naye amepoteza maisha,” alisema Haule.
Alimtaja abiria mwingine aliyetakiwa kusafiri na Filikunjombe kuwa ni Tonny Kebeda, ambaye alichelewa helikopta na hivyo kuachwa.
“Filikunjombe na kaka yetu pamoja na huyu rafiki yetu, walimsubiri kwa nusu saa huyu Kebeda na walipoona anachelewa, wakaamua kuruka na kumuacha. Ilibidi wawahi kwenda Ludewa kwa sababu leo (jana) walikuwa wafanye mkutano wa kampeni kwenye Kijiji cha Lupingu” alisema Dominic.
Akizungumza muda waliosafiri, alisema waliruka kutoka uwanja wa ndege majira ya saa 10:00 jioni wakielekea Ludewa na kwamba, ilipofika saa 12:00 jioni, Katibu Mwenezi wa CCM ludewa, alimpigia simu kumuuliza sababu za chopa hiyo kuchelewa kutua. Alisema aliamua kuwasiliana na watu mbalimbali kuulizia chopa hiyo imekwama wapi bila ya mafanikio.
“Taarifa tuliyopata ni kuwa helkopta hiyo ilianguka mida ya saa 12:00 jioni, lakini taarifa ya kutokea vifo hivyo tumeipata leo,” alisema Dominic.
Akizungumzia taratibu za msiba, alisema marehemu alikuwa na nyumba Kijichi jijini Dar es Salaam na ndipo msiba huo utakuwapo kabla ya kusafirishwa kupelekwa jimboni mwake, Ludewa mkoani Njombe.
“Niko njiani natokea Mwanza kuelekea nyumbani Kijichi. Taratibu zote zitakuwa nyumbani hapo Dar es Salaam na baadaye kwenda Ludewa,” alisema.
MENEJA MBUGA YA SELOUS
Meneja wa Pori la Akiba la Selous, Benson Kibonde, akizungumza na Nipashe, alisema taarifa za kutokea kwa ajali hiyo saa 11:00 juzi alizipata kutoka kwa Deogratius Sanga, ambaye ni mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ya Forward Venture inayomiliki kitalu cha uwindaji cha R2.
Alisema wakati Sanga na wenzake wakiendelea na shughuli za uwindaji katika kitalu hicho, ghafla waliona helikopta hiyo ikianguka na muda mfupi kutoa kishindo kikubwa katika eneo la kitalu cha R3.
Kibonde alisema baada ya kupata taarifa hizo, jiihada za kujulisha ofisi ya Bunge na uwanja wa ndege zilifanyika lakini kufika eneo la tukio ilikuwa si kazi rahisi kwani ni ndani kabisa ya msitu.
MAGUFULI AMLILIA
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema amepokea kwa mshtuko na na kupatawa na huzuni kubwa kutokana na taarifa ya kifo cha Filikunjombe pamoja na watu wengine watatu akiwamo Kapteni Silaa.
Dk. Magufuli alituma salamu za rambirambi kwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Njombe, Deo Sanga, Meya wa Manispaa ya Ilala, Mstahiki Jerry Silaa na familia za wafiwa.
“Kwa hakika, nimeshtushwa na kuhuzunishwa mno na taarifa za vifo vya Filikunjombe na Silaa ambavyo nimetaarifiwa kuwa vimetokea kwa ajali ya helkopta aliyokuwa akiitumia Ndugu Filikunjombe kwa kampeni zake za ubunge katika jimbo hilo la Ludewa,” ilisema sehemu ya taarifa ya Magufuli.
Aliongezea kuwa, “Kama unavyojua, namfahamu vizuri Filikunjombe. Alikuwa mbunge mwenzangu katika Bunge lililomaliza muda wake mwaka huu. Nimefanya kazi naye kwa karibu na kwa miaka mitano ndani ya bunge letu. Alikuwa mtumishi hodari, mtumishi mwaminifu na mwadilifu kwa wananchi wa Tanzania, na hasa wananchi wa Jimbo la Ludewa, ambao aliwawakilisha vyema,”
Katika taarifa hiyo, Dk. Magufuli alieleza kuwa alivyofanya ziara katika Jimbo la Ludewa mwezi uliopita alikuwa akilala nyumbani kwake, na hiyo inadhihirisha namna alivyokuwa karibu naye.
Pia alituma salamu zake za rambirambi kwa Mstahiki Meya Silaa kwa kufiwa na baba yake kwani ni tukio lisilozoeleka, na pia wafiwa wengine.
“Nawapa pole kwa wanandugu wengine waliopoteza ndugu zao katika tukio hilo... wawe na subira katika kipindi hiki kigumu,” ilisema taarifa hiyo ya Magufuli.
Kadhalika alituma salumu nyingine za rambi rambi kwa Spika wa Anna Makinda na Wabunge wote kwa kuondokewa na mwenzao.
Dk. Magufuli aliongezea “Nakuomba pia unifikishe salamu zangu za rambirambi kwa wananchi wa Jimbo na Wilaya ya Ludewa ambao wamepoteza Mbunge wao aliyewatumikia kwa ustadi mkubwa kwa kipindi chote kwa kujali maslahi ya wananchi wake,”
LOWASSA ASHTUSHWA
Mgombea urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa ameelezea kustushwa kwake na taarifa za kifo cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe, aliyefariki dunia juzi jioni baada ya helikopta aliyokuwa akisafiria kuanguka kabla ya kushika moto katika maeneo ya Mbuga ya Selous mkoani Morogoro.
Katika taarifa yake alaiyoituma kwa vyombo vya habari jana, Lowassa anayewakilisha pia muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na NLD, alisema kifo cha mgombea huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) aliyekuwa mahiri na imara katika kutetea jimbo lake na Watanzania, ni pigo jingine kubwa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Oktoba 25.
"Ni pigo lingine kubwa ambalo katika kipindi kifupi taifa limepata, huku bado tukiwa na kidonda cha kuondokewa na wanasiasa wengine mahiri, marehemu Celina Kombani, Dk. Abdallah Kigoda na Dk. Emmanuel Makaidi aliyefariki jana (juzi)," inasema sehemu ya taarifa ya Lowassa kwenda kwa vyombo vya habari jana.
Kombani aliyekuwa akigombea ubunge Jimbo la Ulanga Mashariki (CCM) na Dk. Kigoda wa Handeni (CCM) walifariki dunia wakati wakitibiwa nchini India huku Dk. Makaidi wa NLD aliyekuwa akiwakilisha Ukawa Jimbo la Masasi akifariki dunia juzi mchana wakati akitibiwa katika Hospitali ya Nyangao mkoani Lindi.
Wagombea ubunge wengine waliofariki dunia katika kipindi hiki cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu ni Mohamed Mtoi wa Chadema aliyekuwa akiwakilisha Ukawa katika Jimbo la Lushoto na Estomiah Mallah, aliyekuwa akiwania ubunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya ACT - Wazalendo.
"Filikonjombe alikuwa ni mbunge mahiri, aliyesimama imara kutetea maslahi ya wananchi wa jimbo lake la Ludewa na pia Watanzania kwa ujumla. Ni taarifa ya kushtusha sana ya msiba wa mwanasiasa chipukizi na jasiri, Deo Filikonjombe," iliongeza taarifa hiyo.
Kadhalika, Lowassa alimuelezea Filikunjombe kuwa ni mbunge aliyekuwa mwiba kwa serikali ya chama chake (CCM) wakati akitetea maslahi ya nchi, akitolea mfano katika kashfa ya Escrow ambayo alikuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati iliyochunguza kashfa hiyo na kufanya kazi nzuri kwa manufaa ya taifa.
"Mwenyezimungu awape moyo wa subira familia, jamaa, marafiki na wananchi wa Ludewa katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na mpendwa wao," alisema Lowassa.
Mbali na Filikunjombe, wengine waliokuwamo na kufariki dunia katika helikopta hiyo aliyokuwa akienda kwenye shughuli za kampeni za chama chake kwenye Jimbo la Ludewa kwa ajili ya uchaguzi mkuu ni pamoja na rubani wa chopa hiyo, Kapteni William Silaa, ambaye ni baba wa mgombea ubunge wa Jimbo la Ukonga na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Jerry Silaa.
KATIBU WA BUNGE
Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila alisema kifo cha kiongozi huyo kimewashtua na kimewapa majonzi kwa kumpoteza mtu ambaye alikuwa ni mahiri na mwadilifu katika kutekeleza majukumu yake.
“Filikunjombe ni kiongozi ambaye ana misimamo yake. Tumempoteza mtu muhimu sana. Mara zote alikuwa anasimamia kitu anachokiamini,” alisema Dk. Kashilila, akiongeza kuwa Filikunjombe ni kiongozi mwenye uwezo mkubwa wa kufikiri na kutoa maamuzi sahihi na kwa wakati.
Kuhusiana na msiba huo, alisema ofisi yake itatoa taarifa zaidi baadaye.
SIMANZI LUDEWA
Habari kutoka Ludewa hadi jana jioni zilieleza kuwa, mamia ya wananchi walifurika nyumbani kwa marehemu Filikunjombe huku wengine wakizimia huku vilio vikitanda eneo hilo.
Taarifa hizo zilieleza kuwa, wananchi walianza kufurika nyumbani hapo majira ya saa 7:30 mchana, baada ya kupata taarifa za Filikunjombe kufariki kutoka kwa ndugu walioko jijini Dar es Salaam na vyombo vya habari.
Aidha taarifa zilieleza kuwa, nyumbani hapo walikuwapo mama mzazi wa Filikunjombe na mjomba wake.
Pia watu walifurika nyumbani kwake na kusababisha kukosekana wa eneo la kukaa na wengine kukaa kwenye nyumba yake mpya aliyokuwa akijenga jirani na hapo.
Umati huo uliwalazimu badhi ya askari wa Jeshi la Polisi kufika nyumbani hapo kwa nia ya kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa.
DC: HAKUNA KAMA FILIKUNJOMBE
Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Anatory Choya, akizungumza na Nipashe jana, alisema hakuwahi kumuona mbunge shupavu kama Filikunjombe katika kipindi cha maisha yake ya uongozi serikalini.
“Kifo hiki tumekipokea kwa mshituko mkubwa, majonzi, vilio na sintofahamu zimetawala kwa wananchi wa Ludewa. Nimefanya kazi serikalini miaka mingi, nimekuwa mkuu wa wilaya niliyeishi na
wabunge wengi, lakini ukweli ni kwamba Filikunjombe ni wa tofauti sana... sijawahi kuona kama yeye,” alisema
CCM, LUDEWA WAOMBOLEZA
Mwenyekiti wa CCM wilaya hiyo, Stanley Kolimba, alisema Filikunjombe ndiye mtu aliyepeleka maendeleo Ludewa na alikuwa mbunge wa watu wote.
Alisema Filikunjombe alijitahidi kufika kila kona ya wilaya hiyo kushughulikia matatizo ya wananchi bila kujali jambo lolote.
“Mpaka sasa napokea simu kutoka kila kona ya Ludewa, wengi wakimlilia... tumepoteza mwakilishi wetu shupavu, mpambanaji, hodari mpenda haki na msaada mkubwa kwa wana Ludewa,” alisema Kolimba.
MAMLAKA YA ANGA
Msemaji wa Mamlaka ya Anga Tanzania, Bestina Magutu, alisema jana asubuhi walituma timu maalum ili mwishowe watoe taarifa kamili ya kitaalam kuhusiana na tukio hilo.
“Ni kweli hiyo helkopta jana ilipata ajali na tayari tumeshatuma wataalamu wetu kwenda eneo la tukio ...mara baada ya kuchukua taarifa hizo watatutaarifu nasi tutawapatia taarifa kamili,” alisema Magutu.
RUBANI SILAA
Kabla ya ajali hiyo ya juzi, inaelezwa kuwa marehemu Kapteni Silaa, aliwahi kukumbana pia na ajali nyingine ya chopa Julai 8 mwaka huu wakati akiwa Arumeru na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na abiria wengine wawili.
Katika tukio hilo lililotokea Arumeru wakati wakiwa njiani kuelekea kwenye mkutano wa hadhara katika maeneo ya Ndoombo na Ngureserosambu.
Wakati akisimulia tukio hilo na namna walivyonusurika, Nassari alisema hali ya hewa ilikuwa mbaya, kulitokea wingu zito lakini mwishowe walipona kutokana na ustadi mkubwa ulioonyeshwa na Kapteni Silaa.
CHOPA 5Y-DKK
Kwa mujibu wa mtandao wa Rotorspot, chopa 5Y-DKK inayotajwa kupata ajali iliyowaua Filikunjombe na Kapteni Silaa ni miongoni mwa 58 zilizopo katika orodha ya usajili nchini Kenya baada ya kuziondoa kwenye orodha zile zisizofanya kazi. Hata hivyo, Nipashe haikuweza kuthibitisha moja kwa moja juu ya uhakika wa taarifa kwenye mtandao huo.
Kadhalika, inaonekana kuwa chopa hiyo ni aina ya Aerospatiale 350B3 Ecureuil (AS350 B3E) na aina hiyo ya chopa ilianza kutengenezwa nchini Ufaransa. Hivi sasa zinatengenezwa kwingineko pia ikiwamo Marekani.
Toleo la chopa hizo linaelezewa kuwa ni madhubuti na imara na kwamba, ndiyo chopa ya kwanza kuwahi kutua kwenye kilele cha mlima mrefu kuliko yote duniani wa Everest. Baadhi ya rejea zinaeleza kuwa chopa za toleo hili zilianza kutengenezwa mwishoni mwa mwaka 2011 na zina uwezo wa kuruka hewani na uzito wa hadi Kilogram 2,370.
CHOPA KAMA HII ILIMUUA SAITOTI
Katika mitandao mbalimbali ya masuala ya usafiri anga, yanaonekena kuwa chopa aina hii licha ya kusifiwa kwa ubora na kuaminiwa na taasisi mbalimbali maarufu duniani, lakini pia zimewahi kukumbwa na matukio mbalimbali ya ajali.
Mojawapo iliyo maarufu katika ukanda wa Afrika Mashariki ni ile iliyotokea nchini Kenya Juni 10, 2012. Chopa hiyo AS350 B3e), iliyokuwa mali ya Jeshi la Polisi la Kenya, ilianguka katika maeneo ya Kibiku, kwenye msitu wa Ngong, magharibi mwa Nairobi, Kenya na kusababisha vifo vya watu sita, akiwamo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, George Saitoti na naibu waziri wake, Orwa Ojode.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment