Mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amesema akiingia madarakani baada ya uchaguzi mkuu Jumapili ijayo atafuta misamaha yote ya kodi isiyokuwa na tija ili fedha zitakazopatikana zitumike kusomesha bure kila mtoto kuanzia chekechea hadi chuo kikuu.
Akizungumza katika mkutano wake wa kampeni uliovutia maelfu ya watu kwenye viwanja vya Luandanzovwe jijini Mbeya, jana, Lowassa anayeungwa mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chama cha Wananchi (CUF), NLD na NCCR-Mageuzi, alisema mwaka jana peke yake, serikali ilisamehe kodi yenye thamani ya zaidi ya Sh. trilioni 1.6 huku bajeti ya elimu nchini kote ikiwa ni Sh. trilioni 1.4.
Alisema akichaguliwa na kuingia madarakani, atahakikisha kodi hiyo inakusanywa na kutumika kwa maendeleo ya Watanzania.
"Serikali ikusanye hizo kodi halafu inipe mimi Sh. trilioni 1.4 ili niendeshe elimu nchini,"alisema.
Kadhalika, Lowassa alisema kupitia makusanyo mazuri ya kodi na pia kutumia vyema rasilimali zilizopo nchini, atazibadilisha hospitali za wilaya zote kuwa za rufaa ili kuboresha afya na pia kumaliza kero wanayoipata sasa kina mama kwa kutembea umbali mrefu kwa ajili ya kutafuta huduma hizo.
MAPOKEZI MAKUBWA
Kabla ya mkutano wake jijini Mbeya, Lowassa alipata mapokezi ya kifalme huku baadhi ya wananchi wakijitolea kufagia na kudeki barabara kama ilivyokuwa Musoma, mkoani Mara wiki iliyopita.
Msafara wa mgombea huyo ulianzia kwenye uwanja wa ndege wa zamani hadi kwenye viwanja vya Luandanzovwe vilivyopo Ilomba. Msafara huo wa Lowassa ulivutia maelfu ya watu na kusababisha barabara kuu itokayo Iringa hadi Mbeya kufungwa kwa muda huku polisi wakiwa na kazi kubwa ya kuwapanga vyema wananchi barabarani ili msafara huo upate nafasi ya kusogea.
Aidha, wakati mkutano wa Lowassa ukiendelea, zaidi ya watu 10 walionekana kuzimia kutokana na kukosa hewa na kusaidiwa na madaktari kadhaa, wakiwamo waliokuwa katika msafara wa Lowassa.
SUGU ATAKA MAJI, UMEME
Mgombea ubunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, alimuomba Lowassa kutatua suala la maji na umeme iwapo atachaguliwa kuwa rais. Pia, alisema Mbeya inahitaji hospitali yake kuwa na kipimo cha CT Scan ili wananchi wasihangaike kuifuata huduma hiyo mbali.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema iwapo serikali ya awamu ya tano itaingia madarakani, watahakikisha katiba mpya inayoridhiwa na Watanzania inapatikana baada ya serikali ya CCM kushindwa kutimiza dhamira hiyi.
Aidha, aliwataka wananchi kusimamia na kulinda kura zao kwa sababu tume ya uchaguzi iliyopo siyo huru na ya haki.
Alisema sheria nyingine zimepitwa na wakati kwa sababu vituo vingine vipo kwenye makazi ya wananchi.
Pia, aliwaomba askari na vyombo vya usalama kusimamia uchaguzi huo kwa amani.
"Askari wetu tunawapenda na kuwaheshimu, simamieni haki... na mimi nawaambia wananchi hakuna sababu ya kufanya fujo ila simamieni haki," alisema na kuongeza.
Alisema wizi wa kura unaanza kuanzia mkesha wa siku ya uchaguzi kwani CCM watakuwa wanazunguka mitaani kugawa fedha.
KINGUNGE
Aliyekuwa kada mkongwe wa CCM, Kingunge Ngombali Mwiru, alisema CCM aliyoshiriki yeye (Kingunge) kuiasisi siyo CCM ya sasa.
"Viongozi wa CCM wa sasa wamevunja katiba, hawaheshimu katiba yao wenyewe, hawaheshimu taratibu zao wenyewe, wameamua kubinafsisha chama chao wenyewe.
"Sasa hivi CCM imekuwa ni mali ya viongozi wachache, wanafanya wanayoyataka wenyewe, wanawadhalilisha wenzao,"alisema.
Alisema anaijua CCM na ameitumikia vya kutosha lakini ilibidi aachane nayo kwa sababu si chombo cha kuleta maendeleo kwa Watanzania kwani sasa imechoka.
"Unaposhindwa mzigo inabidi uwaachie wenye nguvu waubebe ambao ni Ukawa chini ya Lowassa,"alisema.
SUMAYE
Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye alisema CCM lazima iondoke madarakani kwa sababu imevunja mkataba na wananchi.
"CCM walitakiwa wajiulize kama wamewatimizia watanzania yale waliyowaahidi kuliko kuendeleea kupiga kelele,"alisema.
Alisema CCM wanatakiwa kujibu hoja na wala si kupanda majukwaani na kuanza kumtukana Lowassa.
Jana, Lowassa alifanya mikutano Mbarali, Chunya, Songwe na Mbeya mjini.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment