Leo naandika kujibu swali alilouliza Dk. Kigwangalla “Je, wao (wapinzani) wakiingia madarakani wanalo jipya?” akaendelea kuhoji ‘‘Kutoka wapi kwa mfano?”. Jibu ndiyo, kama tusingekuwa na jipya tusingeshawishi maelfu ya Watanzania wanaokuja kutusikiliza kwenye mikutano au mamilioni ya Watanzania wanaosubiri kwa hamu siku ya uchaguzi Oktoba 25, 2015 wapige kura ya kumuingiza madarakani kwa kishindo mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama washirika wa Ukawa yaani CUF, NLD na NCCR-Mageuzi.
Ni kupitia fikra hizi mpya tunaendelea kuwashawishi Watanzania wachague upinzani na kupuuza upotoshaji unaofanywa na makada wa CCM na hata ripoti za kupika za Synovate kama walivyopuuzwa na wapiga kura wa Ghana, baada ya mwaka 2011 kutabiri kuwa Nana Akuffo-Addo wa NPP angemshinda Evans Atta Mills, ikawa kinyume chake. Kama Wazambia walivyowapuuza baada ya kutoa matokeo ya kuonyesha Michael Satta wa chama cha upinzani cha PF angeshindwa na chama tawala cha MMD, chini ya Rupia Banda, ikawa kinyume chake, kama ilivyotokea Nigeria na Kenya pia ambako hatimaye Uhuru Kenyatta alimwangusha Raila Odinga.Kabla sijaanza kujenga hoja kujibu swali la msomi huyu aliyekuwa akiutaka urais wa Tanzania kwa kushiriki mchakato wa kura ya maoni ndani ya chama chake, naomba kwanza wapenzi wasomaji wangu tukubaliane kwamba uchaguzi huu wa Oktoba 25, utakuwa uchaguzi wa kuamua hatma ya Tanzania mpya yenye maono, yenye ari mpya katika kujipambanua sio katika nafasi yake kwenye ukanda huu tu bali ulimwenguni kote.
Uamuzi wa kuingiza serikali mpya madarakani kupitia sanduku la kura utazingatia sera, maono ya vyama na wagombea wao badala ya kashfa, matusi, kukata viuno majukwaani na “pushups”. Tanzania mpya itajengwa kwa fikra mbadala. Mataifa yote yaliyopiga hatua za kimaendeleo yaliongozwa na viongozi wenye maono, majasiri katika kufanya uamuzi, naam uamuzi sahihi badala ya kutumia nguvu.
Ni rahisi sana katika mazingira ya sasa mgombea kusakata rumba majukwaani, kutikisa nyonga au kupiga pushups kama vile Tanzania itajengwa kwa misuli ya mabaunsa lakini akiinuka hapo ukimuuliza kwa nini taifa hili ni masikini ataishia kujibu “…nitawavusha, sitawaangusha”. Hajui ni kwa nini elimu ya Tanzania imeshuka, hajui ni kwani deni la taifa linafikia shilingi trilioni 40 lakini bado Tanzania ni ombaomba wa kutupwa.
Mgombea wa aina hii hawezi kujibu maswali haya pamoja na ubaunsa wake wa misuli iliyotuna kutokana na “pushups”. Mama aliyelala chini ndani ya wodi ya wazazi iliyokosa vitanda na dawa kule Ndanda hawezi kupata suluhisho la matatizo kupitia ubaunsa wa misuli wa kiongozi wa nchi. Mzee anayenyanyaswa kwa michango ya maabara kule Katangara-Mrere hawezi kupata ahueni na kufarijika eti kwa vile Rais wake ni baunsa wa misuli.
Kwa hiyo tunahitaji mabaunsa wa fikra na sio watunisha misuli ambayo haina tija kwa taifa la sasa na la baadaye. Hachaguliwi Rais wa Sungusungu bali Rais wa taifa lenye kiu ya kuwa taifa kubwa zaidi kiuchumi si tu Afrika bali duniani. Rais wa nchi ambayo ukubwa wake ni sawa na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya kwa pamoja. Tunahitaji Rais mwenye kiu na ndoto (ambitions) za kuleta maendeleo kwa wananchi wake na pia kuiweka Tanzania katika nafasi yake inayostahili katika ramani ya dunia. Tanzania ni sawa na Simba aliyelala (Sleeping Lion). Simba huyu amelala kwa sababu ya uchovu, kiu na njaa, yaani Tanzania imekosa viongozi wenye dira, falsafa na mkakati thabiti .
Miaka 10 iliyopita yaani 2005 wakati kama huu kulikuwa na mbwembwe nyingi, mgombea urais wa CCM Jakaya Kikwete akawa anajinadi kwa kunengua na kutungiwa majina mengi kama Handsome Boy (Mtanashati) badala ya kuonyesha dira na mwelekeo wa serikali yake mpya, matokeo yake akwa Rais ambaye alikuja kukiri hadharani kuwa hajui ni kwa nini Tanzania ni masikini.
Ni huyo huyo aliyevunja rekodi ya kuzunguzunguka duniani kwa kufanya safari zaidi ya 410 hadi sasa, yaani ukipiga hesabu utakuta kwamba Rais alikaa nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka moja kwa kisingizio cha kutafuta wawekezaji kutoka nje (FDI). Lakini kuna nchi kama Kenya na Rwanda ambako marais, Uhuru Kenyatta na Kagame, hawasafiri kwa kiwango hicho lakini bado ripoti ya Shirika la Fedha Duniani (IMF) inaonyesha kuwa wametupita katika kuvutia uwekezaji.
Rais anayefikiria kuzungukazunguka kwa kisingizio cha kutafuta wawekezaji (utadhani hatuna mabalozi nje ya nchi) anawezaje kufikiria kuwavuta wawekezaji katika nchi iliyojaa urasimu, hakuna nishati ya uhakika yaani hadi mwekezaji asafiri na majenereta? Je, mbwembe za majukwaani kipindi cha kampeni kwa sifa za utanashati ziliweza kuvuta wawekezaji baada ya safari 410?
Ni huyo huyo aliyeingia madarakani na kuanza kugawa bilioni 26 kama mkopo kwa wananchi na hadi sasa hakuna taarifa ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG). Mgombea urais wa CCM mwaka huu na mgombea mwenza wake wamerudia yale yale na sasa wamefikia kutoa ahadi ya kutoa shilingi milioni 50 kwa kila kijiji. Yaani katika vijiji 12,000 atagawa zaidi ya shilingi bilioni 600. Je, hayo si mazingira ya kifisadi yanayoandaliwa katika eneo kubwa (large scale)? Haya ndiyo mabadiliko anayohubiri Dk. Kigwangalla ndani ya mfumo?
Kuna mwanafalsafa mmoja aliwahi kutamka kuwa siasa na aina ya uongozi huathiri namna ya kufikiri kwa watu wa jamii husika.
Ni kupitia uchaguzi huu tu ambapo Watanzania watajiandikia historia mpya kupitia sanduku la kura kwa kubadili uongozi uliopo madarakani kwa kuwa hakuna namna ya kuibadili Tanzania bila ya kukiondoa chama tawala madarakani, ili Tanzania mpya ijengwe kulingana na mtiririko wa maono kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Chadema inayoungwa mkono na umoja wa vyama washirika wa Ukawa.
Siasa na uongozi zinapaswa kuwa ni mfumo wenye mtiririko ambapo ama jamii kwa ushiriki wa kila siku au kwa dhamana ya mtu, watu au chama wanapaswa kuyaweka na kuyapa kipaumbele ili kufikia lengo maalumu.
Watanzania wengi wanajifahamu kuwa wao na hata nchi yao ni masikini, wanyonge na ni ombaomba. Kwa kujikagua tunatambua tuna matatizo ya elimu duni, mfumo dhaifu wa uzalishaji wa kilimo na viwanda, mapato hafifu, kutapeliwa ama kwa hiari kupitia mikataba ya kiuchumi na mashirika ya nje na nchi za nje au hujuma za ndani ya nchi zinazotukosesha mapato ya kutuhudumia kwa kila tunachokitaka.
Je, pamoja na ufahamu huu, tufanye nini kurekebisha kasoro (fix and correct the deficiencies and inefficiency/ineffectiveness) ambazo tumezilea miaka nenda rudi kwa kutoa imani na dhamana kwa chama tawala na viongozi wake ambao uwezo wao na maono yao hayawezi kutupeleka tena mahali popote?
Watanzania tulitoa imani yetu kwa watu tuliowaamini kwa dhati kuwa wanatufaa kuwa viongozi, tukajisalimisha haki zetu za upeo wa mawazo na fikra na kuwapa mamlaka kamili watuundie falsafa za kisiasa na kiutendaji katika azma yao ya kuongoza nchi kama vile dereva anavyopewa imani na abiria wake lakini matokeo yake tumejikuta katika mtaro mrefu wa majitaka ya umaskini, ujinga, maradhi na wadudu hatarishi wenye sumu kali kama ufisadi, uzembe, chuki na unyama usiofaa mbele ya jamii yoyote iliyostaarabika.
Mbele ya jamii iliyostaarabika na yenye uongozi shupavu huwezi kukuta mambo ya aibu kama mauaji ya albino, unyama na ukandamizaji wa haki za kiraia unaofanywa na vyombo vya dola, ukosefu wa uwajibikaji kwa viongozi, viongozi wakuu kuwalea mafisadi huku akina mama wakijifungulia chini na watoto wao wakisomea chini ya miti iwe kipindi cha masika au kiangazi mvua na jua ni lao, haiwezi kuvumilia uongozi unaotumia vyombo vya dola kukandamizi wanafunzi wanapodai haki zao na pia kunyimwa haki zao za kiraia kama vile kupiga kura, haiwezi kuvumilia watawala wakila njama na mataifa ya nje kwa maslahi yao binafsi na kugeuka madalali wa rasilimali za jamii husika walizojaaliwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa hayo machache Tanzania imefikishwa hapo kutokana na uongozi wa nchi kufanya kazi kama genge lisilokuwa na nidhamu.
Chadema na Ukawa kwa kutambua udhaifu uliotokana na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani tangu tupate uhuru, tunatambua umuhimu wa kutengeneza mtiririko wa kiutendaji ili tuijenge Tanzania kwa kusimama juu ya misingi ya kifalsafa, kiitikadi na pia kiutendaji kwa kuwa na (maono ya mbali - vision), malengo na makusudio (goals and objectives) kisha itikadi/imani (ideology), kisha ilani (manifesto) inayokwenda sambamba na sera/mipango (policies) tukitoka hapo tunatunga miswaada/sheria (bill/laws) na kujenga kanuni The Governing Principles), mipango (planning), upashanaji wa habari (communication) na kazi ya kwanza itaanza utekelezaji/uzalishaji (implementation/production).
Katika maisha ya dira (vision life cycle) kuna ukaguzi, ufuatiliaji (checks and balances), kuna mambo ambayo tunayaweka kama vigezo (criteria) vya kuhakikisha kazi inafanyika vizuri yaani vitendea kazi (resources) majukumu (responsibilities) umakini (thoroughness), ufanisi (efficiency), uimara (sustainability) uwajibikaji (accountability), uadilifu (integrity), usimamizi/ufuatiliaji (supervision and follow up), ukaguzi (quality check), juhudi na tija (efforts) maarifa (expertise/knowledge) kupima (measuring) maoni (feed back) na matokeo (results-end product).
Haya yote ni mambo mapya ambayo yalikosekana katika uongozi wa CCM madarakani na ndiyo yaliyolifikisha taifa letu hapa tulipo. Ili Tanzania mpya tunayoielezea kupitia maudhui ya ilani yetu yatimie ni lazima tufuate mtiririko huo katika kuongoza taifa.
Ninapoandika makala haya napenda nimkumbushe Dk. Hamisi Kigwangalla kuwa miaka 50 na ushee ni miaka ambayo sisi kama taifa tunapaswa kujitafakari tulikotoka na tunakokwenda na hakuna mwenye uwezo wa kupumbaza akili za Watanzania tena na kuwafanya waridhike na hali iliyopo (status quo).
Taifa la Singapore lilipojitenga kutoka Malaysia miaka minne baada ya Tanganyika yetu kupata Uhuru, Waziri Mkuu wake, Lee Kuwan Yew, alianza kuiongoza nchi isiyokuwa na rasilimali kabisa tena iliyokuwa katika orodha ya nchi za dunia ya tatu.
Lakini kwa miaka 10 tu aliweza kuijenga Singapore baada ya kuweka malengo juu ya misingi ya kiitikadi, kifalsafa na kimaono na hatimaye kupata jamii isiyo na rushwa na inayowajibika (Corruption-free society and accountability). Alifanya hivyo kwa kupambana na mfumo uliokuwa umejengeka awali uliokuwa ukilea uzembe, ufisadi na uliochochea nakisi ya udilifu.
Yeye Lee hakuamini katika mapambano na sura za watu bali mfumo kwa kutumia mtiririko nilioueleza hapo juu tofauti na ambavyo CCM imekuwa ikifanya katika uongozi wa nchi kwa kutojenga taasisi za uwajibikaji au mfumo thabiti wa kiuwajibikaji badala yake wamejenga na bado wanaendelea kujenga tabia ya kupambana na watu kama ambavyo Dk. Kigwangalla amekuwa akifanya mwenyewe.
Unasikia mara Lowassa fisadi mara hivi mara vile. Haelezi kwa nini Lowassa asifikishwe mahamakani. Haelezi kwa nini waliotajwa kwa ushahidi kwenye ufisadi wa Escrow kama akina Andrew Chenge na Profesa Anna Tibaijuka wameendelea kukabidhiwa dhamana ya kupeperusha Chama Cha Mapinduzi kwenye Uchaguzi Mkuu, katika ngazi ya ubunge.
Naamini atakubaliana nami kwamba chama tawala ndiko ambako mafisadi wamejichimbia na chama husika kupanda mizizi ya ufisadi na mmomonyoko wa maadili. Badala ya kujadili watu tufikie mahala tujadili masuala (issues) yatakayoijenga Tanzania adilifu, uwajibikaji na inayojitambua.
Miaka 25 ya mwanzo tangu tupate Uhuru tulikuwa tunajenga uwezo, vyanzo vya nishati, elimu, huduma za msingi za afya na elimu. Tuliweza kujenga viwanda vya viberiti, nyembe, ndala na khanga kuelekea katika ujenzi wa viwanda zaidi. Maono (vision) ya Mwalimu Julius Nyerere wakati huo ilikuwa kujenga uwezo, na kuona mbali tatizo la ajira kwa vijana ndani ya miaka 50 tuliyopo.
Miaka 25 tumesomewa ilani na sera zile zile za CCM zilizotumika miaka 50. Tena kwa upungufu mkubwa maana mgombea wa CCM anapozungumzia kufufua viwanda utashangaa. Labda Dk. Kigwangalla angetuambia viwanda hivyo viliuawa na serikali ya chama gani iliyokuwepo madarakani hapo kabla hadi mgombea wa CCM sasa atumie lugha ya “kufufua.”
Kama kwa miaka zaidi ya 50 sera zile zile zimeshindwa, leo hii mwaka 2015 -2020 wataweza? Yaani kilichowashinda kwa miaka 50 watakiweza kwa miaka mitano? Bila itikadi, bila falsafa na bila maono kwa kufuata mtiririko nilioueleza hapo awali? Hili sio jaribio lingine la kuwakejeli Watanzania?
Serikali ya Ukawa kwa kuzingatia mtiririko nilioueleza, katika utendaji wake imeandaa mkakati mpya wa kuondoa umasikini ambao utakuwa na nguzo tano ambazo ni pamoja na kupunguza matumizi ya serikali na mashirika yake na kuimarisha utendaji na uwajibikaji, kukuza pato la serikali kwa kudhibiti ukwepaji na misamaha ya kodi holela na kuhakikisha nchi inawekeza katika sekta muhimu na inapata gawio halisia kutoka wawekezaji, kukuza uchumi kwa sera na sheria endelevu ikiwa ni pamoja na kukuza biashara na uwekezaji hasa katika sekta za madini, kilimo, viwanda, ufugaji na uvuvi na kuondoa kodi kwa wanyonge, kuimarisha huduma za umma kama elimu, afya, maji na makazi, na mazingira, kuimarisha utawala bora na mfumo wa haki na sheria chini ya Katiba ya Wananchi.
Chini ya misingi hii na ili kufanikisha mkakati wa kuondoa umasikini, serikali itakayoundwa na Ukawa chini ya Edward Lowassa itatoa kipaumbele katika elimu itatayogharimiwa na serikali kwa kila Mtanzania kutoka elimu ya msingi hadi chuo kikuu na pia, kuimarisha elimu ya teknolojia, ustadi na ufundi inayojenga uwezo wa kujiajiri na ushindani katika soko la ajira, ujenzi na uimarishaji wa miundombinu ya elimu ikiwa ni pamoja na shule za kata, kusimamia ubora wa viwango vya elimu kote nchini, kuimarisha taaluma na mitaala katika shule, kuondoa utoro darasani, na kuboresha afya za wanafunzi, kuboresha maslahi na vitendea kazi kwa walimu ikiwa ni pamoja na nyumba, posho ya kufundishia, usafiri na zana za teknolojia na kufuta michango ya maabara ya shule za kata.
Nchi za Brazili, Mauritius na Sri-Lanka zimepiga hatua kubwa kimaendeleo kwa haraka baada ya kuwekeza kwenye elimu na kuweka mazingira bora ya kumpunguzia mzazi mzigo ili pia kujenga taifa lenye raslimali watu yenye ujuzi wa kutosha.
Bajeti ya Wizara ya Elimu nchini ni takribani shilingi bilioni 794 wakati ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa sekta ya madini pekee inalipotezea taifa shilingi trilioni 2.5 kwa ukwepaji kodi na misamaha holela ya kodi kwa mwaka. Hivi fedha hizi shilingi 2,500,000,000,000 haziwezi kuingizwa katika bajeti ya elimu kusomesha watoto na wadogo zetu? Serikali ya CCM imechoka kufikiri na haiwezekani kuleta mabadiliko ndani ya mfumo wa chama tawala bali ili kulinusuru taifa ni kutafuta mabadiliko nje ya CCM kama alivyotoa wosia Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, kuwa Watanzania mkifikia hatua hii ya kuhitaji mabadiliko na mkawa hamuyaoni ndani ya CCM ni vyema na salama zaidi kuyatafuta nje ya CCM.
Utafiti ulioendeshwa na shirika lisilo la kiserikali la UWEZO mwaka 2012, ulionyesha kuna tofauti ndogo sana ya ufaulu kati ya shule binafsi za Tanzania na zile za umma za nchini Kenya, ikiwa kiwango cha ufaulu wa asilimia 71 na asilimia 75. Hii maana yake, shule binafsi za nchini Tanzania zinatofauti ndogo sana kwa kiwango cha ufaulu (na ubora) kulinganisha na zile shule za umma kwa nchini Kenya licha ya kuwa kwa upande wa Tanzania, wazazi na walezi wanawajibika kulipa gharama kubwa sana wakati nchini Kenya katika shule za umma gharama ni nafuu. Hivyo kumbe inawezekana kabisa kuwa na shule za umma zenye elimu bora.
Kazi kubwa bado inatakiwa kufanyika ili watoto walio kwenye shule na taasisi mbalimbali za elimu nchini wajifunze na kuelimika kweli. Katika hili, serikali inapaswa kulipa suala la ubora wa elimu umuhimu mkubwa. Ukiacha hiyo ngazi ya kielimu, kuna elimu inayotolewa na vyuo vya ufundi kama VETA ambayo nayo inabidi iwekewe mkazo na isionekane ni elimu ya wanaoshindwa kuingia kidato cha kwanza au kuendelea na kidato cha tano.
Serikali ya chama tawala kwa miaka yote imeshindwa kulipa uzito stahiki au imefilisika kisera katika suala la elimu. Sekta ya elimu inapopuuzwa sekta nyingine zote haziwezi kuwa thabiti na hivyo kuathiri mfumo wote wa kiutendaji na maisha ya Watanzania kwa ujumla.
Serikali inayohadaa wananchi kuwa inaimarisha elimu kwa kushusha madaraja na alama za ufaulu inafanya mzaha wa gharama kubwa kwa kizazi cha sasa na vya baadaye.
Kwa haraka haraka, utaona kwa kuangalia suala la elimu pekee, kuna masuala ya afya, lishe, nyumba, maji, fedha (mikopo) na mengine mengi yanayoingiliana ili tupate kuwa na mfumo mzuri wa elimu utakaozalisha wahitimu (si kufaulu mitihani pekee) wenye uwezo wa kuinua katika uzalishaji ama kwa kujiajiri au kuajiriwa.
Tulipopata uhuru, tuliweka umuhimu katika sera ya elimu katika kujua kusoma, kuandika na kuhesabu. Hivi vitatu vilikuwa ni vitu vya msingi, tukapanua wigo kwa kutaifisha shule ziwe mali ya umma kutoa nafasi sawa kwa wananchi, tukatoa elimu ya UPE na elimu ya watu wazima.
Tukafungua shule za ufundi, vyuo vya waganga, mabwana shamba, mifugo, uvuvi, ualimu na fani nyingine ili kupanua uwezo wa kielimu na kutoa nafasi/fursa kwa wananchi kujichagulia fani wanazozitaka ili kushiriki uzalishaji mali.
Lakini katika utekelezaji wa sera, tukasahau vitu vingi na badala ya kurudi kwenye ubao na kuandika upya na kuhoji kila kifungu cha sera hizo za elimu, tukaanzisha sera mpya mpya zenye malengo ya kutoa matunda ya haraka haraka, kukawa na “compound effects” kama nyumba za walimu, ada, vitabu na utitiri wa mambo mengi ambayo yamefanya mfumo wetu wa elimu kuzorota.
Hivyo kwa kushindwa kuwa na umakini, kushindwa kukaa chini na kuangalia mfumo wa elimu kwa mapana, tuliona kuwa tukiongeza majengo na kutoa fursa za kila mtoto kuvaa sare ya shule, kwenda akiwa na kidaftari kimoja, kalamu, dumu la maji na ufagio wa chelewa kusafisha mazingira, basi kuwepo kwake shuleni tutakuwa tumetoa elimu kwa taifa.
Mtoto huyu, anatoka kwenye nyumba ambayo lishe ni shida, maji hakuna, kipato cha ndani hakitoshelezi kustawisha familia, anafika shuleni analazimika kwenda kutafuta kuni, kuteka maji mtoni ili walimu wapate kuni na maji ya nyumbani kwao, ili chakula cha shuleni kipikwe, anabanwa na haja, choo hakionekani, anakimbilia msituni au choo kimefurika, hana dawati, mwalimu ana matatizo mengi nyumbani, mshahara kacheleweshewa, hivyo kiwango na ubora wake kufundisha wanafunzi ni hafifu.
Kifupi wote (mwalimu na mwanafunzi) wanakutana darasani na shuleni wakiwa na matatizo lukuki yanayofanya kubadilisha kabisa malengo halisi ya kuelimisha, na huishia kuwa na masomo yanayolenga kufaulu, bila kujenga uelewa, nadhari inayokosa vitendo, lugha na vitendea kazi vugumu visivyosaidia kuelimisha mwanafunzi.
Leo tunapokutana na wale ambao walibahatika kusoma bila adha (watoto wa jamii ya kipato cha kati na cha juu) au wageni wa nje (wakenya, makaburu, wazungu) kisha kwa uchache wao wanapewa nafasi za kuajiriwa na kuaminika kufanya kazi na kupewa majukumu, tunashindwa kujielewa hata kuangalia tatizo liko wapi.
Aidha tunashindwa kuainisha kwa umakini kuwa sera ya elimu si fanisi, ina upungufu ambao kwa msingi unatukwamisha kuwa na maendeleo tunayoyataka.
Tunapoangalia uchaguzi huu na hata tukishapata rais, wabunge na madiwani, kazi ya kuhakiki na kupitia sera ya elimu haiishi mpaka miaka mitano ijayo.
Kwa leo nitaishia hapa, makala ijayo nitaendeleza yale mapya tuliyonayo kuhusu uchumi, afya, maji, kilimo, ardhi, viwanda , nishati na pia nafasi ya Tanzania katika kujipambanua kimataifa.
Ukiwekeza kwenye elimu,utafanikiwa katika kilimo, viwanda, afya na mengineyo. Hakuna taifa lililowahi kujengwa duniani bila kuwekeza kwenye elimu. Kwenye mazingira haya ya utandawazi na kama pia tumekubali kuwa sekta binafsi na soko huria ndiyo itakayosukuma maendeleo ya nchi, hatuna budi kubadilika Watanzania na hasa vijana kujielimisha wenyewe kwenye mambo mbalimbali iwe kwenye teknolojia, siasa (watu wengi hufikiri siasa ni ya wanasiasa lakini wakumbuke wote tunaathirika na uamuzi wa kisiasa.
Bado naendelea kusizitiza, Serikali ya Awamu ya Tano itajengwa juu ya misingi ya kiitikadi, kifalsafa na kimaono na kamwe haitajengwa juu ya misingi ya kusakata rumba na “pushups majukwani”. Hicho ni kielelezo cha kukwama kifikra na kufilisika kisera, kifalsafa na kuishiwa maono. Mwenyezi Mungu hakutaka taifa hili liwe masikini bali huu ni mpango wa wanadamu kwa makusudi au kwa kushindwa kutumia vipawa vyao kufikiri zaidi.
Naamini Mwenyezi Mungu analipenda sana taifa hili, kila dalili na tafiti makini za kisomi zimeonyesha kwamba Watanzania wapo tayari kubadilisha utawala Oktoba 2015, kwa haya mapya ambayo wamejaaliwa kuyaona kwa serikali mpya ijayo ya Ukawa.
Mwandishi wa Makala hii Ben-Rabiu Saanane nimkuu wa Idara ya Sera na Utafiti ya Chadema. Anapatikana kwa simu +255768078523
- See more at: http://raiamwema.co.tz/misingi-ya-urais-si-kusakata-rumba-au-pushups-jukwani#sthash.945jzH7e.dpuf
No comments :
Post a Comment