dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Sunday, October 18, 2015

Paroko Dar atoa mazito kifo cha Filikunjombe

Wakati Rais Jakaya Kikwete, jana akiwaongoza viongozi wa serikali wakiwamo mawaziri, wabunge, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na waombolezaji mbalimbali waliojitokeza kuuaga mwili wa aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Ludewa, Deogratias Filikunjombe na wenzake wawili, Paroko wa Kanisa Katoliki Parokia ya Epifania Kijichi, Padri Respis Mzena, amehoji endapo kifo hicho ni mpango wa Mungu kweli ama la. 

Akiongoza ibada ya mwisho ya kuiombea miili ya marehemu hao iliyofanyika nyumbani kwa Filikunjombe Kijichi jijini Dar es Salaam kabla ya kusafirishwa kwenda Ludewa Njombe kwa ajili ya maziko leo, Padri Mzena, alisema marehemu aliishi maisha ya useminari aliyohamia nayo uraiani.

Pia alihoji sababu ya kutokea kwa vifo mfulululizo wakati wa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu na kuwataka Watanzania kumuomba Mungu pamoja na kutenda mema wakati wote ili kujiandaa na safari ya milele.

“Najiuliza kwa nini wakati huu vifo hivi, je ni mpango wa Mungu kweli? Kuna wakati watu walifariki sana kwa ajali.
Pia kuna wakati watu wenye ulemavu wa ngozi waliuliwa kikatili kwa kukatwa na mapanga, kifo kama hicho hatuwezi kusema ni mpango wa Mungu, hivyo tunapaswa kumuomba Mungu na kuajiandaa wakati wote,” alisema Padri Mzena na kuongeza:

“Nilisoma na Filikunjombe, maisha ya seminari ya kujali wenzake na kupenda wengine, alijitoa kwa ajili ya wengine hasa wananchi wa jimbo lake na amekufa na rafiki zake ambao wakati wote aliwapenda,” alisema Padri Mzena.

Alitolea mfano kuwa, endapo CCM ingekuwa na wabunge wachapakazi kama, Filikunjombe ni wazi kuwa serikali kwa maana ya nchi ingepiga hatua kubwa ya maendeleo.

“Kwa sababu wema hawadumu, tunatakiwa kutenda mema bila kuchoka na kuamini kuwa watu wanaokufa katika mema wanaishi milele.

Pia tusifikiri kuwa mtu anayekufa kifo cha mateso kama ndugu zetu hawa wametenda maovu, si kweli, tujiandae kwa kila wakati kutwaliwa,” alisema.

Miili iliyoagwa jana katika viwanja vya Hospitali ya Jeshi Lugalo, kabla ya kusafirishwa kuelekea nyumbani kwao Ludewa mkoani Njombe, ambayo inatarajiwa kuzikwa leo ni Filikunjombe, kaka yake,
Plasdus Haule na rafiki yake, Egid Nkwera, ambao walifariki pamoja katika ajali ya Chopa iliyotokea Oktoba 15, mwaka huu.

Filikunjombe na wenzake wanne, akiwamo Rubani wa helikopta hiyo, Willium Silaa, walipoteza maisha katika ajali hiyo, iliyotokea mbuga ya Selous eneo la Msolwa mkoani Morogoro wakati wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Ludewa, Njombe.

Viongozi wengine waliojitikeza kuiaga miili hiyo ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Spika wa Bunge, Anne Makinda, mgombea wa nafasi ya urais (CCM), Dk. John Magufuli, mawaziri na wabunge mbalimbali wakiwamo wa vyama vya upinzani.

MAKINDA: BUNGE LIMEPATA PENGO
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Bunge, Spika wa Bunge hilo, Makinda, alisema, “Napata uzito kusimama na kusema chochote kwa kuwa kwa kipindi hiki kifupi cha mwezi huu tumepoteza wabunge wanne, hili ni pigo kwetu,” alisema Makinda.

Alisema Filikunjombe alikuwa kijana mdogo ambaye hakutimiza miaka yake mitano ya kutumikia ubunge lakini mambo makubwa aliyofanya yamemfanya ajulikane kwa kasi kubwa.

Makinda alisema Filikunjombe alikuwa mtendaji zaidi kuliko mzungumzaji na rafiki wa vyama vyote vya siasa na kwamba alikuwa na marafiki wengi wabunge wa vyama vyote hivyo ni mfano wa kuigwa. 

Alisema kutokana na ushupavu wake wa kufanya kazi na kuwajali wananchi wake, ilionyesha kuwa atashinda tena kuwa mbunge wa jimbo hilo.

“Filikunjombe mara kadhaa nilikuwa simuoni bungeni, anatoroka kwenda jimboni kwake kushughulika na wananchi wake, tulikuwa tunaona anawatembelea wagonjwa, anachimba mashimo ya kuweka nguzo za umeme.

 Jimbo lake limepakana na langu, kutokana na ubize wangu alikuwa akipita kuwasalimia wananchi wangu na kusikiliza shida zao na kuwasaidia kama mbunge wao, tulimpenda ila Mungu alimpenda zaidi,” alisema Makinda.

Mbali na hilo Makinda, aliwataka Watanzania kuachana na chuki, hila, mifarakano isiyo na tija na badala yake wapendane maana hakuna anayefahamu hatma ya maisha yake.

“Deo alikuwa kipenzi cha watu asiye mbaguzi ndio maana leo kaondoka na rafiki na ndugu zake, hivyo ni vema familia na ndugu zake wakaishi kama ambavyo alitaka familia yake iishi, naamini Filikunjombe ataishi milele pamoja nasi,” alisema.

KAFULILA: ALINISAIDIA KUPAMBANA NA ESCROW
Akizungumza kwa niaba ya Kamati ya Kambi ya Upinzani Bungeni, Mgombea wa ubunge   Jimbo la Kigoma Kusini kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, David Kafulila, alisema, Filikunjombe, alikuwa mbunge wa mfano hususan bungeni akisimamia haki na alichokiamini bila kujali itikadi ya chama chake.

Alisema alikuwa akishirikiana na Filikunjombe, katika mambo mbalimbali hususan katika sakata la Escrow na kuibua hoja ya ufisadi iliyotikisa bunge lililopita.

Alisema: “Tutamuenzi kwa kusimamia uwajibikaji, hivyo wabunge wengine waige mfano wake, alikuwa ni jasiri ambaye hakuogopa kusimamia kile anachokiamini.”

ACT: Tumeumia kuliko CCM
Kwa upande wa Chama cha ACT-Wazalendo, kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa na kutuma salamu za rambirambi kwa familia hiyo, Ofisi ya Bunge, Chama cha Mapinduzi(CCM) na Taifa kwa ujumla kufuatia kifo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Chama hicho, Samson Mwigamba, ilisema kifo cha Filikunjombe kimewaumiza zaidi chama hicho kuliko hata CCM yenyewe.

“Filikunjombe kwetu alikuwa rafiki namba moja wa ACT-Wazalendo, ingawa wengi wanamfahamu kama rafiki wa karibu wa kiongozi wetu, Zitto.

Kwa lugha rahisi zaidi tulimtambua kama mwanachama hai wa ACT-Wazalendo asiye na kadi,” alisema.

Alisema awali walishirikiana naye katika  kushauriana kuhusu kuanzisha chama hicho cha ACT-Wazalendo.

“Kama rafiki wa karibu alitutia moyo sote kwamba tunaweza kuanzisha chama kingine na kikaja kuwa mbadala wa kweli.

Alikuwa mshauri, mchangiaji mawazo na mchangiaji namba moja wa rasilimali katika kuendesha chama chetu,” alisema Mwigamba.
Alisema, historia ya Taifa itamuenzi kama historia ya chama cha ACT-Wazalendo, CCM na Bunge.

 AJALI YAUA ASKARI
Wakati msafara wa viongozi mbalimbali ukiondoka katika viwanja vya Lugalo na miili hiyo kuelekea nyumbani kwa marehemu Kijichi, askari mmoja aliyekuwa akiongoza msafara wa mgombea urais wa CCM, Dk. Magufuli alipata ajali eneo la Ubungo mataa na kupoteza maisha hapo hapo baada ya kupasuka kichwa.

Askari huyo aliyekuwa akiendesha pikipiki ya kuongoza msafara, aligongana uso kwa uso na pikipiki (bodaboda) aina ya boxer iliyokuwa ikitokea Morogoro na kusababisha kifo chake.

Mashuhuda wa ajali hiyo, walilieleza Nipashe kuwa, dereva wa msafara huo, alifariki dunia kutokana na kuangukia kichwa na kusababisha kutokwa na damu nyingi huku dereva wa bodaboda aliyogongana naye akiwa amevunjika mguu.

Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga, alithibitisha kutokea kifo cha askari huyo.

WASIFU
Deogratias Haule Filikunjombe, alizaliwa Machi 4, 1972 na kufariki dunia Oktoba 15, mwaka huu, alikuwa Mbunge wa Ludewa tangu 2010 mpaka 2015.

Alisoma katika shule ya msingi Ludewa mwaka 1986, baada ya elimu ya msingi alijiunga na seminari ya Matola Njombe kwa ajili ya masomo ya awali mwaka 1988 mpaka 1989.

Aidha, alisoma elimu ya sekondari katika seminari ya Kasita inayomilikiwa na Jimbo Katoliki la Mahenge kuanzia mwaka 1989 hadi 1992 na alijiunga na sekondari ya Forest Hill mjini Morogoro kwa masomo ya kidato cha tano na sita mwaka 1994/96.

Baada ya hapo akajiunga na Chuo cha Uhusianao wa Kimataifa cha jijini Dar es Salaam, Tanzania na kisha alijiunga na Chuo cha Polisi Moshi (CCP).

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Makerere Uganda na kusoma Shahada ya Mawasiliano ya Umma mwaka 1996. Aliwahi kuwa mwakilishi wa Radio One na ITV pamoja akitumia jina la Deo Haule na pia mwandishi wa Gazeti la The Guardian.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments :

Post a Comment