Mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama cha AFP, Soud Said Soud, amesema uchaguzi mkuu wa visiwani hivyo haukuwa huru na wa haki kwa sababu kulikuwa na watu waliokuwa wakiingia vituo vya kupiga kura wakiwa na karatasi za kura mfukoni na kupiga zaidi ya kura moja kitendo ambacho kinyume na sheria.
Aidha, mgombea huyo amemtaka Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, aondoke madarakani kwa madai muda wake wa uongozi kikatiba umefikia kikomo Novemba 2, mwaka huu na badala yake iundwe serikali ya mpito itakayoandaa uchaguzi mwingine.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Soud alisema baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) ndiyo chimbuko la kuchafuka kwa uchaguzi wa visiwa hivyo, baada ya kushindwa kusimamia majukumu yao ipasavyo kwa kuweka mbele maslahi ya vyama vyao badala ya taifa.
Alisema uchaguzi huo ulitawaliwa na mizengwe ikiwamo vitendo vya udanganyifu, vitisho na mawakala kupigwa na kuvuliwa nguo wakiwamo wa chama cha Tadea katika mkoa wa Kusini Pemba.Alisema katika kituo cha kupigia kura cha Madungu katika mji wa Chakechake, kura zilizidi idadi ya watu waliokuwa wameandikishwa katika Daftari la Wapigakura ambao ni 180 lakini baada ya kufungua na kuhesabu kura zilifikia 350.
Aidha, alisema Soud alisema baadhi ya mawakala walikamatwa wakiwa na kura mifukoni wakiwa katika hekaheka za kutaka kutumbukiza kura zisizo halali katika masanduku ya kura halali katika kituo cha Chonga, mkoa wa Kusini Pemba.
“Uchaguzi wa Zanzibar ulikuwa uchafuzi siyo uchaguzi, lazima urudiwe kulinda misingi ya kweli ya demokrasia ambayo kila mwanademokrasia wa kweli ataitetea,” alisema.
Alisema katika Jimbo la Wawi mkoa wa Kusini Pemba, taratibu zilivunjwa baada ya masanduku ya kura kuchukuliwa kutoka chumba namba nne na kuhamishiwa namba sita na kazi ya kuhesabu kufanyika bila ya kuwapo mawakala wa vyama vingine.
Vyama vitatu hadi sasa vimetoa msimamo wa kutaka uchaguzi kurudiwa Zanzibar kati ya 14 vilivyokuwa vimesimamisha wagombea kikiwamo CCM, AFP na ADC. Kutokana na mgogoro wa kikatiba ulioibuka, Soud alisema Rais Dk. Shein anatakiwa kuunda serikali ya mpito itakayokaa madarakani kwa muda wa miezi 18 ambayo itaandaa uchaguzi mwingine pamoja na kuiongoza Zanzibar katika kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi huo.
Alisema serikali hiyo lazima ishirikishe vyama vyote vya siasa, watu wanaoheshimika na jumuiya za kiraia ili kumaliza mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.
Alisema Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 28 (2), inaeleza wazi kuwa Rais ataacha madaraka yake baada ya kumaliza miaka mitano kuanzia tarehe alipokula kiapo cha uaminifu pamoja na kiapo cha kuwa Rais wa Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment