Arusha. Kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na wanachama 63 wa Chadema, akiwamo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe kupinga kushtakiwa kwa kufanya maandamano na mikusanyiko isiyo halali, imepangwa kutajwa Desemba 30 katika Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha.
Katika kesi hiyo, ambayo inatarajiwa kusikilizwa na majaji watatu, wafuasi hao wakiwamo pia aliyekuwa katibu mkuu Chadema, Dk Willibrod Slaa na mbunge aliyemaliza muda wake Arusha Mjini, Godbless Lema wanapinga kuendelea kusikilizwa kwa kesi za kufanya mikusanyiko inayodaiwa si halali.
Akizungumza jana mara baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Lema alisema wanaomba Mahakama Kuu kutamka kwamba Mahakama zinazoendelea kusikiliza kesi hiyo si halali na inakiuka Katiba kwani inazuia uhuru wa chama cha siasa kukutana.
“Tunaomba kesi hizi zifutwe kwani zinakinzana na Katiba na hazina uhalali wa kutendeka kosa la kijinai pale wanasiasa wanapokusanyika katika mkutano halali,” alisema.
Katika mahakama mbalimbali jijini hapa, watuhumiwa hao 63 wanakabiliwa na mashauri mbalimbali yanayohusiana na mikusanyiko isiyo halali, kuanzisha kesi ya Januari 5, 2011 ambao viongozi wakuu wa Chadema walikamatwa kwa maandamano, yaliyokuwa yakipinga uchaguzi wa meya wa Jiji la Arusha.
Katika kesi hiyo, wafuasi hao wa Chadema wanawakilishwa na Wakili Method Kimomogoro.
No comments :
Post a Comment