Wakati Chama cha Mapinduzi kinapinga uamuzi wa Marekani wa kusitisha msaada kwa Tanzania wa tilioni 1.5 kutokana na kufutwa kwa matokeo ya Uchauzio Mkuu wa Zanzibar, Chama cha Wananchi CUF kimeunga mkono uamuzi huo na kutaka mshindi wa urais wa Zanzibar atangazwe na kuapishwa ili kuondoa vikwazo vya kiuchumi.
Msimamo huo ulitolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chama cha Wananchi (CUF), Ismail Jussa Ladhu jana alipokuwa akizungumzia uamuzi wa Marekani kuzuia fedha za MCC hadi muafaka wa uchaguzi utakapopatiwa ufumbuzi pamoja na kuondoa sheria kandamizi ya makossa ya mitandao.
Jussa alisema hakuna njia ya kunusuru Tanzania kuwekewa vikwazo vya kiuchumi ikiwemo kunyimwa misaada zaidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kukubali kukamilisha uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.
Aidha alisema kuwa uamuzi wa Marekani wa kuzuia msaada unatoa fundisho kubwa kwa nchi nyigine kuheshimu mashariti ya kunufaika na fedha za MCC ikiwemo kulinda misingi ya Demokrasia na Utawala bora.
Jussa alisema matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar yalifutwa kwa ubabe na Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi Zanzibar baada ya kuona CCM wapo katika hatari ya kuanguka lakini hakuna kifungu cha Katiba kinachompa uwezo huo.
Alisema msimamo wa CUF utaendelea kubakia palepale pamoja na kufanyika kwa mazungumzo ya kutafuta muafaka wa uchaguzi, ZEC warudi kazini wakamilishe kuhakiki na kutangaza matokeo na mshindi wa uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka huu.
Alisema kuwa kuna kikundi cha watu wachache Zanzibar ndiyo hawataki kuona mabadiliko yakitokea ya kiutawala Zanzibar licha ya CCM kushindwa kufikia malengo ya Uchaguzi Mkuu mwaka huu.
“Kuna kikundi cha watu Zanzibar hakitaki kuona mabadiliko ya kiutawala kwa maslahi yao binafsi licha ya CCM kuanguka katika uchaguzi wa Oktoba 25 Mwaka huu,”alisema Jussa.
Alisema kuwa kadhia ya uchaguzi wa Zanzibar imesababisha madhara makubwa ikiwemo wananchi kuishi katika mazingira ya wasiwasi pamoja na kupanda kwa gharama za maisha visiwani humo.
Jussa alisema hakuna sababu kwa Viongozi wa CCM kuwa na wasiwasi wa kupoteza vyeo wakati marekebisho ya kumi ya Katiba ya Zanzibar yameweka mfumo mzuri wa kuunda serikali ya pamoja na wao kunufaika kama CUF ilivyonufaka baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.
Aidha, alisema CUF haiko tayari kuona Uchaguzi Mkuu unarudiwa Zanzibar kwa malengo ya kuibeba CCM licha ya kuanguka katika uchaguzi wa awali Visiwani humo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai, alisema kuwa haikuwa mwafaka kwa Marekani kuzuia msaada huo wakati Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ilikuwa na hoja za msingi za kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 Mwaka huu.
Alisema kuwa uchagfuzi wa Oktoba 25 Mwaka huu ulipoteza sifa za kuwa uchaguzi huru na wa haki baada ya kutawaliwa na vitendo vya udaganyifu kinyume na misingi ya demokrasia na utawala bora.
Alisema hana wasiwasi na Marekani kuwa hawajapata taarifa na vielelezo vya kuharibika kwa uchaguzi wa Zanzibar na iwapo watapata taarifa hizo watakubaliana na uamuzi wa ZEC wa kufuta matokeo ya uchaguzi huo.
Alisema uchaguzi huo ulitawaliwa na vitendo vya udaganyifu ikiwemo idadi ya wapiga kura kuzidi watu waliosajiliwa katika daftari la wapiga kura wa kudumu pamoja na mawalaka wa vyama kupigwa na kufukuzwa katika vituo vya kazi.
“Ufumbuzi wa migogoro sio kuzuia misaada kwa sababu unawaumiza hadi watu wasiokuwa na hatia, cha muhimu ni kutafuta njia ya mufaka za kuondoa matatizo.”alisema Vuai.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
No comments :
Post a Comment