Rais John Magufuli
Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah kutokana na kutoridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa hususan kwenye upotevu wa mapato ya Serikali katika Bandari ya Dar es Salaam.
Dk Hoseah ambaye aliingia madarakani mwaka 2006 akichukua nafasi ya Meja Jenerali mstaafu, Anatory Kamazima aliyekuwa kiongozi wa taasisi hiyo tokea 1990-2006, unafanya wakuu wa mashirika ya umma ambao wameondolewa madarakani na Dk Magufuli kufikia sita tangu aingie madarakani Novemba. Wengine ni Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Rished Bade baada kubaini kupitishwa kwa makontena zaidi ya 300 na kusababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh80 bilioni.
Vilevile, Rais alitengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Profesa Joseph Msambichaka, Katibu Mkuu wa iliyokuwa Wizara ya Uchukuzi, Dk Shaaban Mwinjaka na Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadhi Massawe. Kigogo wa kwanza kuonja ‘joto ya jiwe’ alikuwa Kaimu Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Hussein Kidanto na kuvunja Bodi ya hospitali hiyo alipofanya ziara ya kushtukiza katika hospitali hiyo.
Taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Mawasiliano, ilimkariri Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue akisema kuwa kutokana na uamuzi huo, Rais Magufuli amemteua aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola kukaimu nafasi hiyo.
Balozi Sefue amebainisha kuwa, Rais Magufuli amechukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa Takukuru chini ya Dk Hoseah hauwezi kuendana na kazi anayoitaka.
“Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya Serikali ni Bandarini na katika Mamlaka ya Mapato Tanzania, hivyo Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda mrefu lakini kasi ya Takukuru kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka,” alisema Balozi Sefue.
Mbali ya Dk Hoseah, Balozi Sefue alisema, Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi waandamizi wanne wa Takukuru ambao walisafiri nje ya nchi licha ya Rais kupiga marufuku safari hizo kwa watumishi wa umma. Aliwataja watumishi hao kuwa ni Mkurugenzi wa Elimu kwa Umma, Mary Mosha; Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu, Ekwabi Mujungu, Ofisa Uhusiano, Doreen Kapwani na Katibu Muhtasi wa Mkurugenzi Mkuu, Rukia Nikitas ambao walisafiri nje ya nchi licha ya kunyimwa kibali cha safari kutoka kwa Rais au Katibu Mkuu Kiongozi.
Balozi Sefue amewataka watumishi wengine wa umma kutii agizo la Rais na kuonya kuwa atakayekiuka atachukuliwa hatua kali.
Kauli za Dk Hoseah na Mlowola
Akizungumzia uteuzi huo Mlowola alisema: “Ni mapema mno kuzungumzia suala hili maana hata barua bado sijapata... Si unajua tena Serikali inafanya kazi kwa utaratibu.”
Dk Hoseah alipotafutwa kuzungumzia uamuzi huo wa Rais, hakupokea siku na alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) alijibu kuwa ana shughuli nyingi na kutaka apigiwe baadaye.
Wadau wazungumza
Wakizungumzia uamuzi huo, baadhi ya wasomi na wanasiasa walisema kwa jinsi mashirika na taasisi za Serikali zinavyonuka rushwa na ufisadi, Dk Hoseah alipaswa kujiuzulu muda mrefu, badala ya kusubiri kuondolewa na Rais.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Richard Mbunda alisema Takukuru imeshindwa kuzifanya kazi hizo mbili kwa muda mrefu.
“Kwa muda mrefu fedha za umma zinaliwa. Hakuna mtu ambaye angemuacha Dk Hoseah kwa rushwa, wizi na ufisadi ule uliofanyika bandarini na TRA. Alipaswa kujiuzulu siku nyingi kutokana na taasisi aliyokuwa akiisimamia kuonekana wazi kushindwa kufanya kazi yake ipasavyo. Uamuzi wa Dk Magufuli naona ni sahihi kabisa,” alisema Mbunda.
Alisema taasisi hiyo inapaswa kuwa na kiongozi atakayeifanya iwe na meno. “...Na hili linawezekana kama kiongozi mkuu wa Takukuru atahakikisha sheria inaboreshwa ili taasisi iwe na meno zaidi ya kudhibiti na kuzuia rushwa.”
Mhadhiri mwingine wa UDSM, Dk Benson Bana alisema: “Ukiona Rais anatengua uteuzi wa kiongozi mkuu mwandamizi wa Serikali tambua kwamba kuna jambo ambalo si sahihi amelibaini. Tumesikia mengi kuhusu rushwa na mfano mzuri ni lile sakata la makontena pale Bandarini. Inaonekana wazi kulikuwa na kasoro fulani.”
Alisema kutokana na kasoro hizo ni wazi kuwa Dk Magufuli anahitaji mtu mwingine atakayeweza kuifanya kazi hiyo vyema; “hata alipomteua (Mlowola) tulijua tu kuna jambo linataka kufanyika.”
Kaimu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema, “Kuondolewa kwa mtu mmoja hakumaanishi mabadiliko Takukuru maana tatizo la taasisi hiyo ni la kimfumo.”
“Tunapaswa kuwa na Katiba Mpya itakayoeleza majukumu ya Takukuru na kuipa meno ili ifanye kazi zake vyema.”
Mnyika alimtaka Dk Hoseah kujitokeza hadharani na kuzitaja rushwa kubwa alizokuwa akificha kuziweka hadharani kutokana na kuwagusa wakubwa.
“Kama anahisi kaonewa huu ndiyo wakati mzuri kwake kuibuka na kuzitaja rushwa hizo. Lakini pia Dk Magufuli awe anatueleza sababu za kumteua mtu na sababu za kumuondoa mtu ili wananchi wajue tatizo ni nini katika utendaji wa Serikali,” alisema.
DED Kinondoni asimamishwa
Wakati Dk Magufuli akitengua uteuzi wa Dk Hoseah, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Tamisemi), Jumanne Sagini jana alimsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, mhandisi Mussa Natty ambaye hivi karibuni alihamishiwa huko akitokea Manispaa ya Kinondoni.
Sagini alisema Natty anapaswa kurudi katika Manispaa ya Kinondoni na kusubiri uchunguzi zaidi dhidi ya tuhuma zinazomkabili.
Alitaja tuhuma hizo kuwa ni usimamizi mbaya uliosababisha barabara za Manispaa ya Kinondoni kujengwa chini ya kiwango na kutowachukulia hatua watendaji wa manispaa waliokua chini yake, ukosefu wa uadilifu katika ubinafsishaji wa eneo la ufukwe wa Bahari la Coco na malalamiko ya wananchi juu ya viwanja katika eneo la Kinondoni ulioambatana na usimamizi duni wa watumishi hasa wa sekta ya mipango miji na ardhi.
No comments :
Post a Comment