Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete
Januari 2015. Ilianza na kiporo cha matukio mengi ya 2014, yakiwamo ya uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, mchakato wa Katiba mpya na kashfa ya escrow ambayo yalitikisa nchi na haikuwa ajabu wakati Rais alipotangaza Baraza la Mawaziri lililokuwa na mabadiliko 13 ambayo yaliwaweka nje makada watatu.
Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alitangaza baraza lililokuwa na mabadiliko hayo Januari 25 baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kujadili ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) iliyohusu Akaunti ya Tegeta Escrow ambayo ilifunguliwa kwa pamoja na Shirika la Umeme na kampuni binafsi ya kuzalisha nishati hiyo ya IPTL zilizokuwa zinazozana kuhusu malipo ya gharama za nishati hiyo.
Tanesco ilitakiwa iweke kwenye akaunti hiyo fedha ambazo ingeilipa IPTL kusubiri kumalizika kwa mzozo huo uliokuwa mahakamani, lakini fedha hizo, zaidi ya Sh306 bilioni, zilichotwa kwa njia ambayo ilionekana kuwa ya ‘ujanja’ na kuisababishia Serikali kukosa mapato iliyostahili.
Ufuatiliaji wa mwenendo wa fedha hizo ulibaini kuwa baadhi zilitumbukia mikononi mwa mawaziri, wabunge, majaji, viongozi wa dini na watumishi waandamizi wa Serikali na mabilioni mengine ya fedha taslimu yalichotwa kutoka benki.
Bunge liliazimia wote waliohusika kwa njia moja au nyingine wawajibishwe na mamlaka zinazowahusu.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa wakati huo, Jaji Fredrick Werema alikuwa wa kwanza kujiuzulu na kufuatiwa na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Anna Tibaijuka na wa mwisho akawa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye alijiuzulu siku Rais alipotangaza mabadiliko.
Mawaziri wapya walioingia ni Anne Kilango, aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Charles Mwijage, mbunge wa Muleba Kaskazini ambaye aliteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Watumishi wengine wa umma kutoka Benki Kuu, Mamlaka ya Mapato (TRA), Tanesco na Wizara ya Ardhi walifikishwa mahakamani mwezi Januari kwa kuhusishwa na kashfa hiyo, wakati watumishi wengine waliachishwa ama kusimamishwa kazi, akiwamo mnikulu wa Ikulu.
Taharuki ya Panya Road
Kwa wakazi wa Dar, mwaka 2015 haukuanza vizuri baada ya vijana wanaojulikana kama Panya Road kuvamia maeneo kadhaa ya jiji, hasa mitaa ya Sinza, Kinondoni, Mwananyamala, Mabibo, Magomeni, Manzese, Kagera na Mburahati na kupiga, kupora watu na kuvunja vioo vya magari.
Siku hiyo, Januari 2, vijana hao walikuwa wametoka kumzika mwenzao aliyeuawa kwa tuhuma za wizi na kusambaa mitaani kufanya uhalifu huo uliosababisha jiji zima kupata taharuki. Polisi walieleza baadaye kuwa tukio hilo halikuwa kubwa kama ilivyodhaniwa bali lilikuzwa na teknolojia ya mawasiliano baada ya watu kutumiana ujumbe kutahadharisha kuhusu Panya Road. Baadaye walitangaza kuwakamata zaidi ya vijana 500 kwa tuhuma za kuhusika kwenye tukio hilo.
Profesa Lipumba, wafuasi CUF mbaroni
Katika anga za kisiasa, mwenyekiti wa CUF. Profesa Ibrahim Lipumba, akiwa na wanachama 32 walikamatwa na polisi eneo la Mtoni Mtongani wakidai kufanya maandamano bila ya kibali. Lipumba alikamatwa wakati akielekea Zakhem Mbagala ambako wananchi walikuwa wakimsubiri ahutubie katika siku ya kumbukumbu ya wafuasi wa CUF waliouawa na polisi kutokana na vurugu zilizotokea Zanzibar kupinga matokeo ya urais.
Kukamatwa kwake kulisababisha wabunge wa upinzani kutaka Bunge lijadili suala hilo na Spika Anne Makinda alipojaribu kuwazuia, walisimama wote wakipiga kelele na ndipo lilipoahirishwa hadi jioni wakati walipojadili.
Kituo cha polisi chavamiwa
Mwezi Januari pia ulikumbwa na tukio lisilo la kawaida baada ya watu 15 kuvamia kituo cha polisi cha Ikwiriri wilayani Rufiji na kupora bunduki saba na risas 60. Tukio hilo lilitokea Januari 22 na askari waliouawa katika shambulio hilo ni Edgar Mlinga na askari wa kike aliyejulikana kwa jina la Judith.
Mapacha walioungana wazaliwa
Januari 4. Mkazi wa Kata ya Buhare, Manspaa ya Musoma mkoani Mara, Helena Paulo (20) alijifungua watoto pacha wa jinsi ya kike wakiwa wameungana kifuani na tumboni wakiwa na uzito kilo 4.6 kwa pamoja. Tukio hilo lilivuta hisia za wananchi wengi ambapo walijitokeza kwenye hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara wakitaka kuwashuhudia muujiza huo.
Walioshindwa waapishwa
Januari 6. Utata uliibuka kuhusu matokeo ya uchaguzi wa Serikali za mitaa baada ya wagombea watatu waliotangazwa kushinda Ubungo kuwekwa kando, na badala yake walioshindwa ndiyo waliapishwa. Kitendo hicho kilisababisha vurugu na polisi kulazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya. Vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa CUF na CCM .
Jaji Samatta apanda kizimbani
Jaji Mkuu Mstaafu, Barnabas Samatta alipanda kizimbani Januari 8 kutoa ushahidi katika Mahakama ya Wilaya ya Hai tukio ambalo lilivuta hisia za wananchi wengi kwa kuwa lilikuwa ni la aina yake kuona kiongozi wa juu wa mhimili huo wa dola. Jaji huyo mstaafu alilazimika kufika mahakamani hapo ili kutoa ushahidi dhidi ya
Akutwa na kenge 134 hai JNIA
Katika tukio lililoshangaza wengi Januari 11, raia mmoja wa Kuwait, Hussain Ahmed Ally Mansour (34) alikamatwa na polisi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na kenge 149, kati yao 134 wakiwa hai. Polisi ilidai kuwa alikuwa wakiwasafirisha kwenda nje ya nchi.
Dk Shein afuta michango shuleni
Januari 13. Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein atangaza kufuta michango kwenye shule za msingi na malipo ya gharama ya mitihani kwa wanafunzi wa sekondari kuanzia Julai.
Ukawa wajitenga Kura ya Maoni
Januari 24. Vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa) vilitangaza kutoshiriki na kuhamasisha wananchi wawaunge mkono kugomea kuendelea kwa mchakato wa Kura za Maoni, vikidai kwamba kuna matatizo mengi katika utekelezaji wa jambo hilo muhimu.
Jukwaa la Katiba limejitokeza na kuweka bayana pendekezo lake la kutaka wagombea wa nafasi ya urais kutoka katika vyama mbalimbali vya siasa kupimwa afya zao kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
No comments :
Post a Comment