Maisha kabla ya bomoabomoa ni ya hofu na yale baada ya tendo hilo ni hatarishi isiyotoa uhakika kwa waathirika juu ya ‘kesho itakuwaje.’
Hiyo ndio inayoweza kuelezwa, kulingana na hali halisi iliyotawala miongoni mwa walio katika balaa hilo. Majanga mbalimbali yanayowakabila wahusika, baadhi yakiwa na uhusiano wa moja kwa moja na bomoabomoa na nyingine ni yanayoambatana na janga hilo.
Hadi kufikia wishoni mwa wiki iliyopita, zaidi ya wakazi wanaokadiriwa 92,330 walioko katika maeneo hatarishi, hawana makazi ya kuishi, kutokana na nyumba zao kubomolewa, katika eneo la Magomeni Sunnah.
Ni sakata linaliowahusu pia wakazi 1,000 wanaoendelea kusota eneo la Bonde la Kinondoni Mkwajuni, licha ya nyumba zao zimeshabomolewa na wiki hii tingatinga la serikali likifanya kazi ya kusafisha mazingira husika, ili yaweze kupitisha maji kirahisi.
Wakazi hao wanaoishi katika vibanda vilivyoezekwa kwa mabati na miti wameendelea kuishi maisha ya ‘kubangaiza’ kutokana na kukosa mahali pa kwenda.Mwishoni mwa wiki iliyopita, serikali ilitangaza mabadiliko katika msimamo wake dhidi ya bomoaboma, ikisema itaendelea katika bonde la Msimbazi tu, huku kwingineko kukifanyiwa tathmini mpya, miongoni mwake ni kuangalia namna gani wanaostahili fidia, wafanyiwe hivyo.
Hiyo inachangiwa na madai kwamba, baadhi ya waathirika wa bomoabomoa, wamedai kuwa na nyaraka halali za kumiliki viwanja vyenye majengo yao na wamekuwa wakilipa kodi serikalini.
Tayari kuna mchakato mwingine unaoendelea wa kuorodhesha wathirika wasio na uwezo ili wapatiwe msaada, huku kwa upande wa pili kuna wakazi walionenda mahakamani kuzuia hatua hiyo ya serikali, ili madai yao ya msingi ya kukiukwa haki yao isikilizwe.
MAISHA YAO HALISI
Wakazi wa bonde la Kinondoni Mkwajuni, ambao licha ya kuwa wakali na wakorofi pindi wanapohojiwa na waandishi wa habari, katika sura ya pili wamekuwa wakiiomba jamii hiyo kuwafadhili kwa msaada kama vile wa fedha au chakula.
Hali hiyo ni ishara ya kawaida kwamba wanakabiliwa na mazingira magumu na hawana msaada wa kuwasitiri, kutokana na vitu na mali zao wakati wa kubomolewa na wako katika hali ya kuelemewa na matatizo, zaidi ya uwezo wao ulikosimamia.
Ni wakazi wanaioshi katika vibanda vilivyoezekwa kwa mabati yaliyoezuluiwa kutoka kwenye majengo husika, wakipika chakula aina moja, ambayo ni maharage kwa ajili ya milo miwili kwa siku.
“Asilimia kubwa hapa tunaoweza kupika, tunapika maharage ambayo ni rahisi kwetu kula. Kuni za kubandika tunaokota kwenye masalia ya bomoabomoa, suala la kuunga (mboga) ni majaliwa ya Mungu,” anaeleza mkazi anayejitambulisha kuwa, Mama Sharifa, mwenye watoto watatu.
Anatoa sababu za kukimbilia kupika maharage, kwamba haina gharama kubwa ya kuiunga. Anataja mahitaji yake kuwa ni kitunguu na kiasi kidogo cha mafuta kidogo.
“Ukila maharage hayakinaishi! Lakini siyo kama tunapenda, bali tunakula kwa sababu hakuna mboga tunayoweza kuimudu, kwa sababu ya hali mbaya ya maisha tuliyo nayo.
“Kama unavyofahamu, mbona inatakiwa kuungwa vizuri, bora haya maharage ambayo unapika na kula tu,” anasema Mama Sharifa.
SABABU ZA KUBAKI BONDENI
Katika mazungumzo yake na gazeti hili, wakazi hao wameeleza sababu za kushindwa kuondoka eneo hilo, licha ya kufukuzwa tangu Desemba 17 mwaka jana.
Wanabainisha kuwa, ni kutokana na kushtukizwa na dai la kuhama eneo hilo, hali iliyowafanya washindwe kupata mwelekeo wa kujinusuru
Amina Salehe, ni miongoni mwa wakazi hao, anayesema kuwa nyumba yake ya vyumba vinne, iliyojengwa na marehemu mume wake miaka 20 iliyopita, imebomolewa na sasa yuko katika mtihani kushindwa pa kuelekea, baad ya kunomolewa makazi yao.
“Mume wangu alinunua eneo hilo kwa mzee mmoja aliyekuwa akiishi hapa, akajenga hii nyumba na tulifuata taratibu zote za ununuzi wa ardhi, lakini nashangaa nimeambiwa sina hati miliki na ninatakiwa kubomolewa nitaenda wapi,” anasema Amina na kuongeza kuwa;
“Ndio maana nimelazimika kuendelea kulala eneo hili, hadi hapo Mungu atakaponijalia mahali pa kwenda.”
Julius Maisharo (58), ambaye ni mkazi wa Bonde la Kinondoni Mkwajuni, anasema eneo hilo alilirithi kutoka kwa kaka yake miaka 40 iliyopita na kwamba aliliendeleza kwa kujenga nyumba za kupanga.
Maisharo ambaye alijekuwa na jengo la vyumba 10 vya kupangisha, ambavyo kila kimoja alikuwa akitoza kodi ya Sh. 25,000 kwa mwezi. Ilibomolewa Desemba 17 mwaka huu.
“Sikuamini kile kilichotokea, lakini ilibidi nishuhudie. Kwa sasa baada ya kusafirisha ndugu zangu kuelekea mkoani Dodoma kwa wadogo zangu, nimebaki hapa kudai haki yangu,” anasema Julius.
Anaongeza kuwa, serikali ilipaswa kumpatia taarifa mapema kabla ya kumbomolea, ili ajiandae na kuona namna ya kuanzisha maisha mengine.
Kuhusu kama ana mpango wa kuondoka, anasema hatarajii kufanya hivyo, ikizingatiwa kuwa umri wake ni mkubwa na hana shughuli za kufanya zitakazompatia kipato cha kuendesha maisha yake.
WANAOTAKIWA KUBOMOLEWA
Katika kundi lingine ambalo nyumba zao zimewekewa alama ya X kwa maana ya kutarajia kubomolewa, Nipashe iliwashuhudia wakihangaika kuhamisha vitu vyao. kutoka kwenye nyumba walizokuwa wakiishi.
Katika eneo la Kinondoni Hananasif, wakazi wake walianza kuhamisha vitu vyao kuanzia Desemba 30, mwaka jana, ikiwa ni takriban wiki mbili hadi sasa, baada ya kutangaziwa na serikali waondoke hapo kwa hiari kabla ya kukutwa bomoabomoa.
Wakazi hao ambao walikuwa wakionyesha masikitiko yao kwa kile kilichokuwa kikiendelea, walijihami kwa kuhamisha vitu kama madirisha, milango na paa la nyumba.
“Tulivyoona wenzetu wa Mkwajuni wamebomolewa bila ya huruma, ilibidi na sisi tujiandae yasije yakatukuta kama wao, ikabidi tuanze kuhama taratibu,” anasema Maria Mpalila, mkazi wa Hananasif.
Maria anasema kuwa, alinunua eneo hilo kwa bei ya Sh. 50,000 mwaka 1986 na kuhusiana na kuanza kubomoa mapema baada ya agizo la serikali, alifanya hivyo kuhofu kukumbana na matukio ya wizi, ili aokoe mali zake.
“Roho inaniuma nyumba yangu niliyoijenga kwa gharama, leo natakiwa kuibomoa. Watoto wananitegemea, mume wangu amefariki, nitaenda wapi?” anahoji Maria katika hisia ya kulalama.
Maria ambaye ni mama wa watoto watano, kati yao wawili wanamtegemea, anabainisha kuwa, katika orodha hiyo, wawili wanamtegemea na watatu wanajitegemea.
Anasema, gharama za kubomoa nyumba yake alitumia Sh. 150,000 aliyompatia fundi kwa ajili ya kung’oa madirisha, milango na mabati.
“Mafundi wamepandisha bei za kazi, huna 200,000 hakuna anayekubomolea nyumba yako, nimetoa hii hela ili kuokoa vitu vya visiharibiwe,” anasema Maria, anayesema kazi nyinginezo zinahitaji ulinzi ni kuhamisha vitu kuvipeleka kunakotakiwa ambako ndio kwenye hatari zaidi.
“Unakuta umebomoa nyumba kwa fedha kubwa, lakini kama utashindwa kulinda vitu vyako, lazima wezi waviibe, maana wameshamiri sana maeneo haya,” anasema.
Mrai anasema kuwa, ili kuvihamisha vitu vyao ni lazima wawakabidhi kazi hiyo vijana ambao wanafahamu, kuepuka kuibiwa.
“Unakuta unapata hasara juu ya hasara, umeingia gharama lakini vitu vinaishia mikononi mwa wezi,” anasema Maria.
WIZI WASHAMIRI
Vijana mbalimbali walionekana wakirandaranda. katika mitaa ambayo bomoabomoa inaendelea, wakitafuta masalia vyuma, bati na vifaa vinginevyo.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment