dual citizenship

Pemba Paradise

Zanzibar Diaspora

Mwanakwerekwe shops ad

ZanzibarNiKwetuStoreBanner

ZNK Patreon

Scrolling news

************ KARIBUNI..................Contact us for any breaking news or for any information at: znzkwetu@gmail.com. You can also fax us at: 1.801.289.7713......................KARIBUNI

Monday, January 18, 2016

Serikali yaipa kibano benki Stanbic mabilioni ya Uingereza

Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango.
Kashfa ya benki ya Stanbic Tanzania iliyotokana na mkopo wa Sh. trilioni 1.3 ambao Serikali ya Tanzania ilikopa benki ya Standard ya Uingereza, imeingia kwenye sura mpya baada ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuitoza benki hiyo faini ya Sh. bilioni tatu kutokana na kuvunja taratibu za kibenki.
 
Itakumbukwa kuwa, mwishoni mwa mwaka jana, Mahakama ya London, Uingereza ilibaini ufisadi kwenye mchakato wa  mkopo huo ambao serikali ya Tanzania ilikopa benki ya Standard ya Uingereza kupitia mshirika wake Stanbic Tanzania.
 
Katika hukumu yake, mahakama hiyo iliamuru Serikali ya Tanzania ilipwe dola za Marekani milioni saba (Sh. bilioni 15), ikiwani ni asilimia moja ya riba iliyoongezwa na tozo ya Sh. bilioni moja.
 
Katika mkopo huo, serikali ilitakiwa kulipa asilimia 1.4, lakini benki ya Stanbic Tanzania, ikaingiza kinyamela kampuni ya Kitanzania ya EGMA kama mtu wa kati pamoja na  kuongeza asilimia moja ya mkopo huo kisi cha dola za Marekani milioni sita.Fedha hizo zinadaiwa kuingizwa kwenye akanti ya EGMA na baada ya siku chache kutolewa, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. 
 
FAINI YA SH. BILIONI TATU
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha Dk. Philip Mpango, alisema kwa kuzingatia upungufu  wa miamala iliyohusisha kampuni ya EGMA na Stanbic Tanzania, BoT imeiandikia barua benki ya Stanbic ya kusudio la kuitoza faini ya Sh. bilioni 3.
 
Alisema faini hiyo imetozwa kutokana na kifungu namba 67 cha Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
 
Alisema sheria hiyo inaitaka benki ya Stanbic kutoa utetezi katika kipindi cha siku 20 ambacho kitaisha Januari 30, mwaka huu.
Alisema endapo BoT haitaridhika na utetezi huo, Stanbic italazimika kulipa faini hiyo.
 
Kuhusu kampuni ya EGMA, Dk. Mpango alisema uchunguzi bado unaendelea kufanywa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na utakapokamilika taarifa itawekwa wazi.
 
“Benki Kuu imechukua hatua hizo kama onyo kwa benki ya Stanbic ili iweze kuwa makini katika kuhakikisha shughuli zake zinaendeshwa kwa mujibu wa taratibu za kibenki na kuzingatia sheria,” alisema.
 
JINSI ILIVYOBAINIKA
 Dk. Mpango alisema Julai, 2013 BoT iligundua matatizo yaliyohusiana na hasara itokanayo na mikopo, huku baadhi ya wafanyakazi wake kuacha kazi na wengine  kuondolewa kazini wakiwamo viongozi waandamizi wa benki hivyo, hivyo kuagiza  kufanyika kwa ukaguzi maalum.
 
Alisema ukaguzi huo ulibaini kuwapo kwa miamala ya kutia shaka iliyohusu malipo kwa kampuni ya EGMA iliyohusika katika uwezeshaji wa upatikanaji wa mkopo huo.
 
Alisema malipo hayo kwa kampuni ya EGMA yalikuwa yamefanyika kinyume cha  taratibu za kibenki na yalihusisha uongozi wa benki ya Stanbic.
 
Dk. Mpango alisema taarifa ya ukaguzi huo iliwasilishwa kwa benki ya Stanbic na BoT iliagiza Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo kuchukua hatua stahiki za kurekebisha kasoro zilizoonekana.
 
Alisema pia Stanbic iliagizwa kutoa taarifa kwa Kitengo cha Kupambana na Utakatishaji Fedha ( FIU) kilichopo Wizara ya Fedha na Mipango kuhusiana na miamala hiyo yenye mashaka na Stanbic walitekeleza na kutoa taarifa FIU.
 
Alisema Septemba 29, mwaka jana, BoT ilipokea barua kutoka Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Kughushi na Rushwa ya nchini Uingereza (SFO), ikiiomba BoT ruhusa ya kutumia ripoti yake ya ukaguzi kama ushahidi katika kesi dhidi ya benki ya Standard ambayo ni mshirika wa Stanbic Tanzania.
 
Dk. Mpango alisema katika kesi hiyo benki ya Standard ilikubali makosa na ilitozwa faini ya dola za Marekani milioni 32.20, ambazo kiasi cha dola milioni 7 zinalipwa kwa serikali ya Tanzania, dola milioni 6 zikiwa ni fidia na dola milioni moja zikiwa kama ni riba. 
 
“Faini waliyopewa Stanbic  kwa benki na taasisi za fedha zisijihusishe na makosa ya aina hiyo ambayo ni kinyume cha taratibu za kibenki na uvunjaji wa sheria za nchi,” alisema.
 
BENKI ZAONYWA
Dk. Mpango alionya kuwa, hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa benki au taasisi ya fedha yoyote itakayobainika kwenda kinyume na taratibu za kibenki na sheria ya benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
 
MAELEZO YA STANBIC
Nipashe lilimtafuta msemaji wa benki ya Stanbic, Annette Nkini, kuelezea hatua ya BoT kuindikia barua ya kutakiwa kulipa kiasi hicho cha fedha, alisema hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa kuna wakubwa wake ambao wanapaswa kulizungumzia.
 
Msemaji huyo alipoombwa kulipatia gazeti hili namba ya wahusika ambao wanapaswa kulizungumzia suala hilo, alisema angetuma namba lakini hadi gazeti hili linakwenda mitamboni hakutuma namba hiyo na hata alipopigiwa tena simu yake ya mkononi ilikuwa inaaita bila ya kupokelewa.
CHANZO: NIPASHE

No comments :

Post a Comment