Serikali imewasilisha Bungeni mapendekezo ya Mwelekeo wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/17-2020/21, huku ikieleza kwamba vipaumbele vikubwa ni kujenga uchumi wa viwanda na miundombinu.
Wakati mapendekezo hayo yakiwasilishwa, wabunge wa upinzani wamepinga huku wakisema kwanza inatakiwa kuhakikisha mgogoro wa Zanzibar unaisha.
Akiwasilisha mpango huo Bungeni jana, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alisema katika mwaka wa kwanza wa mpango huo, 2016/17, pamoja na miradi mingine, serikali itanunua ndege mbili mpya za abiria za Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Katika ujenzi wa barabara, awamu ya kwanza ya mpango huo, serikali itaendelea na miradi ya ujenzi wa barabara za kupunguza msongamano kwenye miji mikubwa ya Arusha, Mwanza na Dar es Salaam, itapewa kipaumbele.Mpango huo pia unaeleza kuwa katika awamu hiyo ya kwanza, makadirio ya bajeti kwa mwaka 2016/17, fedha kwa ajili ya maendeleo zitakuwa ni Sh. bilioni 6,182.2 ambapo fedha za ndani zitakuwa Sh. bilioni 4,810.1 sawa na asilimia 77.8 na za nje zitakuwa Sh. bilioni 1,372.1.
Mpango huo ulieleza kwamba katika mwaka 2015/16, serikali ilitenga Sh trilioni 5.9 kwa ajili ya miradi ya maendeleo, lakini hadi Desemba, mwaka jana, fedha zilizokuwa zimetolewa ni Sh. trilioni 1.8.
Kwa mujibu wa takwimu zilizo kwenye kitabu cha mopango huo, mpaka Oktoba, mwaka jana, deni la taifa lilifika dola za Marekani milioni 19,221.4 ikiwa tofauti na Oktoba, 2014 ambapo lilikuwa dola za milioni 18,643.8.
Taarifa hiyo inasema katika kipindi hicho akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola milioni 4,034 kiasi ambacho kinaweza kutumika kuagiza bidhaa kwa mienzi minne.
Mbunge wa Hai (Chadema), Freeman Mbowe, alisema ni vigumu mpango huo kutekelezekana ilhali hali ya kisiasa Zanzibar ikiwa si nzuri.
Alisema nchi haiwezi kuwa na uchumi mzuri na kuendesha mipango yake ya maendeleo kama haina utawala bora.
Wakichangia kwenye mjadala, Magdalena Sakaya, Mbunge wa Kaliua (CUF), alisema bila serikali kujenga reli ya kisasa yenye kiwango cha kimataifa na kutegemea barabara ni vigumu nchi kupata maendeleo.
Alisema ni lazima seikali ianze kwenye kilimo cha umwagiliaji na kuachana na kutegemea kilimo cha mvua ambazo hazieleweki.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda, alisema mapendekezo hayo hayajaeleza wazi itaanzisha viwanda vya aina gani na kuhoji kama viwanda hivyo vitaanzishwa na sekta binafsi au na serikali yenyewe.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Innocent Bilakatwe (Kyerwa-CCM), ambaye alihoji takwimu zilizotumiwa na serikali katika kulinganisha mafanikio iliyoyapata katika mpango wa maendeleo uliopita.
“Ukitizama takwimu zilizotumika ni za mwaka 2012 hadi 2013 wakati leo ni mwaka 2016. Mlitumia vigezo gani kusema wananchi wanaopata maji ni asilimia 60 nchi nzima wakati jimboni kwangu Kyerwa na hata huko Dar es Salaam maji hakuna,” alisema.
Mbunge wa Buyungu (Chadema), Kasuku Bilango alisema, ni vyema serikali ikasema kama viwanda vinaanzishwa na serikali au sekta binafsi pekee.
“Umeme hakuna tunataka viwanda? Mtueleze mmejipanga vipi kuhakikisha nchi ina umeme wa uhakika maana tunaelezwa kuna gesi. Je, hii gesi itaenda mikoa yote au itaishia Dar es Salaam?” alihoji.
Alisema ili kutekeleza vyema sera ya viwanda nchi ni lazima iwe na barabara nzuri kuanzia vijijini hadi mijini na reli ya kisasa.
Mbunge wa Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsanzugwako, alisema, “Changamoto za mpango uliopita ni nzito sana. Mmejipanga vipi kuhakikisha hazijitokezi tena. Mikoa kama Kagera, Katavi na Kigoma ina mvua nyingi na kilimo kinakubali lakini serikali haijawekwa katika mpango wa ujenzi wa viwanda. Hatuna reli tutawezaje kuwa na viwanda?”
Margareth Sitta (Urambo- CCM) alisema: “Barabara haziwezi kudumu bila reli. Ni lazima tuwe na reli ya kisasa. Hizi takwimu za asilimia 60 ya wananchi wanapata maji si kweli wananchi bado hawana maji.”
Akijibu hoja za wabunge hao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itayafanyika kazi maoni yote ya wabunge hasa kuhusu takwimu, huku suala la Zanzibar akishauri liachwe litatuliwe na Wazanzibari wenyewe.
Mbunge wa Madaba, Joseph Kizito, alihoji kutumika kwa takwimu za miaka mitatu iliyopita, kuitaka serikali itakapokuja na mpango huo kueleza wananchi wanaopata maji, wanatumia umbali gani kuyapata kwa maelezo kuwa wapo wanaotembea kilomita 10 kusaka maji.
CHANZO: NIPASHE
No comments :
Post a Comment