Dar es Salaam. Kasi ya utendaji wa Rais John Magufuli imezidi kuibua matumaini mapya kwa Watanzania baada ya sehemu kubwa kuridhishwa na utendaji wake katika siku 100 za mwanzo wa uongozi wake.
Ripoti ya utafiti mpya iliyotolewa jana imebainisha kuwa katika siku hizo, takribani watu wanane kati ya 10 wameridhishwa na utendaji wa jumla wa Dk Magufuli na wana matumaini atafanya vizuri siku zijazo.
Katika utafiti huo uliofanya na timu ya watafiti kutoka kampuni mbili za utafiti za Infotrak Reserch & Consulting na Midas Touche’ East Africa, Rais alipata wastani wa asilimia 84.1 ya alama zilizokuwa zinapima utendaji wa ujumla.
Utafiti huo umehusisha sampuli ya watu 1,200 wenye umri wa zaidi ya miaka 18 ikiwa ni uwakilishi wa Watanzania 24.25 milioni wa kundi hilo na kufanyika katika kanda sita nchini ndani ya mikoa 15 ya Tanzania Bara na Zanzibar.
Kanda hizo ni Pwani, Kanda ya Ziwa, Kaskazini, Kusini, Zanzibar na Kati. Ripoti hiyo inabainisha kuwa Rais alipata wastani wa asilimia 81. 9 katika kigezo cha kuheshimu sheria na utawala bora, huku akipata asilimia 78.9 katika usimamizi wa uhuru wa habari na uhuru wa kutoa maoni.
“Katika kigezo cha urafiki kwa vyombo vya habari, Rais Magufuli alipata wastani wa 76.1 ya alama zote wakati katika msisitizo katika masuala ya kimataifa, ikiwamo Jumuiya ya Afrika Mashariki amepata wastani wa asilimia 77.8,” inasema ripoti hiyo.
Kuhusu utafiti
Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) ndiyo iliyoomba kufanyika kwa utafiti huo uliohusisha mahojiano ya ana kwa ana kwa kusaidiwa na mfumo wa kompyuta, ili kupata maoni yenye uwakilishi halisi juu ya utendaji wa Serikali ya awamu ya tano ndani ya siku 100 za mwanzo. MCL inachapisha magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.
Matokeo ya utafiti yanabainisha kuwa Dk Magufuli huenda ndiye rais aliyepata alama za juu za kukubalika zaidi baada ya uchaguzi kutokana na watu tisa kati ya 10 kuonyesha kuridhishwa namna anavyoendesha Serikali.
“Asilimia 9.6 pekee ya waliohojiwa ndiyo waliona kuwa Rais haendeshi vizuri Serikali na sehemu kubwa ya kundi hili ni wale wenye umri wa kati,” inasema ripoti hiyo ya utafiti uliofanyika kati ya Februari Mosi hadi Februari 7 mwaka huu.
Rais Magufuli ameonekana kuaminika zaidi na akina mama ambao asilimia 93.1 waliohojiwa wanaona anaiendesha vizuri Serikali dhidi ya asilimia 88 ya wanaume.
Umaarufu wa Rais unaonekana kushamiri zaidi vijijini ambako asilimia 91.5 ya waliohojiwa kutoka maeneo hayo waliridhishwa na utendaji wake dhidi ya asilimia 88.2 ya wakazi wa mjini.
Mikakati ya awali ya kiuchumi aliyoanza kuitekeleza Dk Magufuli imezidi kumuongezea imani kwa wananchi ambapo watu nane kati ya 10 wanaamini kuwa atabadilisha hali mbaya ya kichumi nchini.
Ikumbukwe kuwa alipoingia tu madarakani Novemba 5, 2015, Rais alianza kutekeleza mikakati migumu ya kubana matumizi ya fedha za Serikali ikiwamo ya kupiga marufuku safari za nje hadi kwa kibali maalum na taasisi za umma kutokodi kumbi za mikutano mahoteli badala yake watumie majengo ya Serikali.
Njia hizo zilimpatia pia umaarufu nje ya mipaka ya nchi kiasi cha mitandao ya kijamii kuibua kiunganishi kilichotamba katika mtandao wa Twitter kwa kiingereza “#WhatWould MagufuliDo (MagufuliaAngefanyaNini) kikihamasisha watu kufikiri kubana matumizi kabla ya uamuzi wa kutumia fedha. Walipoulizwa wananchi katika kigezo hicho cha kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma, utafiti huo unabainisha kuwa watu tisa kati ya 10 wanaridhishwa na utekelezaji wa ahadi hiyo huku asilimia kubwa wakiwa ni wenye umri kati ya miaka 36 hadi 45.
Kwa muda mrefu rushwa na ufisadi vimekuwa jipu sugu serikalini na Rais alianza kushughulikia suala hilo kwa kuwasimamisha kazi au kutengua uteuzi wa vigogo wanaotuhumiwa kwa ufisadi, wakiwamo vigogo wa taasisi nyeti kama Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Takukuru.
Katika swali la wananchi wanazionaje jitihada za kubaini na kupambana na rushwa na matumizi mabaya ya fedha za umma, watu tisa kati ya 10 walionyesha kuridhishwa na mikakati ya Rais katika kutokomeza janga hilo.
“Watu tuliowahoji wanaona kwamba hatua alizochukua Dk Magufuli hivi karibuni za kupambana na rushwa ni salamu kwa watumishi wazembe na wabadhirifu,” inasema ripoti hiyo.
Hotuba ya Rais wakati wa ufunguzi wa Bunge la 11 aliyoitoa Novemba 19 mwaka jana bado inaishi miongoni mwa wananchi licha ya kutolewa zaidi ya miezi mitatu iliyopita kutokana na kukubalika zaidi na wananchi.
Ripoti hiyo inabainisha kuwa asilimia 89.2 ya waliohojiwa walikiri kuwa hotuba hiyo iligusa maeneo muhimu ambayo yamekuwa yakirudisha nyuma maendeleo ya nchi.
Mbali na kupima mtazamo wa wananchi juu ya ahadi mbalimbali za Serikali ya Awamu ya Tano, ripoti hiyo imeanika mtazamo wa wananchi juu ya mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa katika sekta mbalimbali zikiwamo za elimu, afya, uchumi, uzalishaji wa ajira, mapambano dhidi ya rushwa na miundombinu.
Matokeo hayo yanabainisha kuwa hadi sasa Serikali imefanikiwa katika elimu kwa asilimia 47, afya (19.7), vita dhidi ya rushwa (15.6), uchumi (3.3), miundombinu (2.7) na uzalishaji wa ajira asilimia 2.1. Hata hivyo, Dk Magufuli kwa mujibu wa utafiti huo, amefanya vibaya zaidi katika masuala ya utalii, upatikanaji wa maji safi na salama, uwezeshaji wa wanawake, utatuzi wa mgogoro wa Zanzibar, ulinzi na usalama na madini.
Wananchi bado wanaona Rais anatakiwa aweke mkazo zaidi katika masuala ya elimu, afya, ajira, uchumi, kilimo na kupunguza gharama za maisha, kwa mujibu wa utafiti huo.
Katika kupima ubora wa uteuzi wa Baraza la mawaziri, wananchi wamemkubali Rais Magufuli kwa kumteua Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu kwa asilimia 90 huku wakikubali udogo wa baraza la mawaziri.
No comments :
Post a Comment