Meatu/Singida. Vita ya watumishi hewa inayoendelea nchini imempandisha kizimbani, Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Imani Nyamangaro jana akidaiwa kujilipa mishahara ya wastaafu 57 yenye thamani ya Sh29.4 milioni wakati huko Meatu, mkoani Simiyu mtumishi aliyefariki mwaka 2012 ameendelea kulipwa zaidi ya 21 milioni.
Mbali na matukio hayo, huko Mwanza imebainika kwamba watumishi hao hewa wamekuwa ‘wakikopa’ fedha kwenye taasisi mbalimbali za fedha.
Mhasibu kujilipa mishahara ya wastaafu
Katika shtaka linalomkabili Nyamangaro, mwendesha mashtaka na wakili wa Serikali, Michael Ng’hoboko alidai mbele ya Hakimu wa Mahakama hiyo, Joyce Minde kuwa kati ya Aprili 29, 2013 na Machi 27, 2014 mshtakiwa, kwa makusudi, aliiba mishahara hewa ya zaidi ya Sh29.4 milioni.
Ng’hoboko alidai kuwa mshtakiwa alikuwa akijipatia mishahara hiyo ambayo wahusika walishastaafu kazi muda mrefu, kupitia akaunti yake yenye namba 50802503513 ya Tawi la NMB Mjini Singida.
Nyamangaro alikana kutenda makosa hayo 57 na kesi yake imeahirishwa hadi Aprili 27 itakapotajwa tena.
Hakimu Minde alisema dhamana ya mshtakiwa ilikuwa wazi na kwamba angepashwa kutoa fedha taslimu Sh14,709,321 mahakamani au mali isiyohamishika yenye thamani inayolingana na kiasi hicho cha fedha.
Hadi mwandishi wa habari alipoondoka mahakamani hapo, mshtakiwa alikuwa hajatekeleza masharti ya dhamana.
Marehemu alipwa miaka minne
Katika usaili wa watumishi mkoani Simiyu, imebainika kuwa mtumishi wa zamani wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, aliyefariki miaka minne iliyopita amelipwa Sh21.2 milioni kupitia akaunti yake ya NMB, wilayani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Erasto Sima alisema wamegundua kwamba marehemu huyo ambaye hakumtaja jina amekuwa akilipwa mshahara baada ya kuendelea na kazi ya uhakiki wa watumishi hewa kwa awamu ya pili katika
halmashauri hiyo na wengine 15.
“Baada ya zoezi la awali la kuhakiki watumishi hewa tukaona ni bora zoezi hili likawa endelevu ndani ya wilaya yetu. Tumewabaini watumishi hewa wengine 15 ambao wako katika makundi ya waliofariki, wastaafu na watoro sugu,” alisema.
Alisema kuwa miongoni mwa watumishi hao wastaafu ni sita, watoro wa kudumu wanane na aliyefariki mmoja na wameshachukua hatua za haraka za kuzuia
mishahara hiyo ili isiendelee kulipwa.
Akizungumzia marehemu aliyelipwa kwa miaka minne pasi na kubainika, Sima alisema walibaini baada ya mtu asiyejulikana kutumia kadi ya benki ya kwenye mashine ya ATM na kumezwa.
“Mtu huyo ameshindwa kuichukua lakini hadi muda huo, Oktoba 2015, alikuwa ameshalipwa kiasi hicho cha fedha huku na kwenye akaunti hiyo kulikuwa na Sh1 milioni tu. Tumewasiliana na meneja wa NMB, tawi la Mwanhuzi, Meatu afanye ufuatiliaji ili tuweze kumbaini mtu aliyekuwa akichukua fedha hizo na tukimkamata tunamfikisha katika vyombo vya sheria.” alisema.
Aliwaonya watumishi wote wa Serikali wanaofanya kazi ya kuhakiki watumishi kwamba wale watakaowabaini walio hewa na kuwaacha kwa masilahi yao hawatavumiliwa.
Awali, Wilaya ya Meatu iliwabaini watumishi hewa 19 huku wengi wao wakiwa kutoka idara za elimu na afya.
Watumishi hewa wakopeshwa
Katika hatua nyingine, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imebaini mbinu zinazofanywa na watumishi serikali za kunufaika na mishahara hewa.
Akizungumza jana jijini Mwanza, Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Ernest Makale alisema watumishi hao wamekuwa wakifanya mchazo mchafu wa ‘watumishi hewa kukopa fedha’ kutoka benki mbalimbali kwa kutumia nyaraka za kughushi.
Alisema uchunguzi umebaini kuwa majina ya watumishi yaliyowasilishwa na baadhi ya halmashauri za mkoa huo si kamilifu kwani kuna wengine ambao hawajaorodheshwa.
Makale alisema kutokana hali hiyo Takukuru inaendelea na uchunguzi wa kina kuwabaini watumishi hewa wengine na wale wanaoshirikiana nao.
“Kuna dalili za wazi ambazo zinaonyesha kuna watumishi wasiokuwa waaminifu wa halmashauri ambao wanahusika kufanya vitendo hivi vya udanganyifu, atakayebainika atafikishwa mahakamani,” alisema Makale.
Takwimu za Serikali
Kati ya Sh583 bilioni ambazo Serikali imekuwa ikitumia kila mwezi kwa ajili ya kulipa mishahara, zaidi ya Sh54 bilioni zimekuwa zikipotea kutokana na kulipa watumishi hewa.
No comments :
Post a Comment