Imeahidi kuanzisha mpango maalum ambao kila mwananchi wa Manispaa hiyo atachangia Sh. 40,000 kwa mwaka ili aunganishwe na mpango wa matibabu wa bima ya afya ambao utawawezesha kupata matibabu ya bure katika hospitali mbalimbali.
Mpango huo utaanza kutekelezwa mwezi Juni mwaka huu, huku bajeti ya Manispaa hiyo ikiongezeka kwa asilimia 59 kutokana na kukua kwa mapato ya ndani.
Wazee wa Manispaa hiyo nao wametangaziwa neema ya matibabu bure kwani watapewa kadi maalum zitakazowawezesha kutibiwa hospitali za umma.
Mapato hayo yametokana na ukusanyaji madhubuti katika kodi za majengo, mabango, leseni za biashara, huduma za kuegesha magari, hoteli na ruzuku ya serikali kuu.
Bajeti ya mwaka 2016/2017 katika Manispaa hiyo inafikia Sh. Bilioni 248.47 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka jana ambayo ilikuwa ya Sh. Bilioni 156.24.
Katika bajeti ya mwaka huu kuna ongezeko la Sh. zaidi ya bilioni 92.
Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob aliwasilisha bajeti hiyo jana jijini Dar es Salaam katika kikao cha Baraza la Madiwani.
Baada ya kuwasilisha bajeti hiyo, Madiwani wote wakiwamo wa upinzani na Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliipitisha kwa kauli moja ili ianze kuwahudumia wananchi.
Akisoma bajeti hiyo, Jacob alitaja ukusanyaji wa mapato ya ndani umeingiza Sh. bilioni 64.28 na kwamba imeongezeka kutoka Sh. bilioni 56.6 za mwaka jana.
Licha ya bajeti ya mwaka huu kulenga kugharamia huduma za matibabu, lakini imelenga kujenga shule ya bweni katika Kata ya Goba kwa gharama ya Sh. milioni 250, ujenzi wa matundu ya vyoo katika shule, kujenga vyumba vya madarasa na ununuzi wa madawati 30,000.
Kazi nyingine zitakazofanyika ni pamoja na ujenzi wa Barabara kuelekea kituo cha daladala cha ya Simu 2000 na Barabara ya Akachube ambazo zimetengewa Sh. bilioni 50.
Kuhusu suala la usafi, Meya Jacob alisema kila Kata itakuwa na gari lake la kuzolea takataka na Manipaa imetenga Sh. 2.2b .
Manispaa hiyo ina jumla ya Kata 25 na Sh. bilioni 3.6 zimetengwa kwa ajili ya gharama za kusafirisha takataka.
Aidha, katika bajeti hiyo, Manispaa inatarajia kununua Trekta lenye kijiko kwa ajili ya kutengeneza barabara na zimetengwa Sh. bilioni 1 kwa ajili ya kazi hiyo.
Kazi nyingine za fedha hizo ni kuweka sakafu ngumu katika masoko yote ya manispaa, ili kuondoa adha ya uchafu na matope katika msimu wa mvua na zimetengwa Sh. bilioni 1.65.
Kuhusu vijana na wanawake Manispaa hiyo imetenga Sh. bilioni 4.7 kwa ajili ya kuwakopesha na kila Kata itapata Sh. milioni 200.
No comments :
Post a Comment