Wakili Juma Nassoro, akiwa na baadhi ya viongozi wa CUF, nje ya Mahakama Kuu Dar es Salaam, jana akiwaeleza mambo machache wanachama na wafuwasi wa chama hicho kuhusiana na ombi lililopelekwa katika mahakama hiyo la kutaka kuwashtaki Msajili wa Vyama vya Siasa na watu wengine 12, akiwamo Profesa Lipumba.
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekubali maombi yaliyowasilishwa na Bodi ya Wadhamini wa Chama cha Wananchi (CUF) ya kutaka kuwasilisha maombi katika kesi ya msingi ya kufuta uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi wakumtambua Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.Katika kesi hiyo, Bodi ya Wadhamini ambayo iliwakilishwa na Wakili Juma Nassoro, aliitaka mahakama hiyo kuweka zuio maalumu kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuacha kufanya kazi nje ya mipaka yake na kuingilia maswala ya chama hicho kinyume cha taratibu.
Akisoma uamuzi huo jana, Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaama, Ama–Isario Munisi alisema mahakama hiyo imeridhia kuwasilishwa kwa maombi ya kesi ya msingi ndani ya siku 14 ili ianze kusikilizwa.“Mahakama imeridhia hoja ya mleta maombi ya kutaka kuwasilisha maombi ya kesi ya msingi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama wengine 12 waliomo kwenye kesi hii,” alisema Jaji Munisi.
Baada ya uamuzi huo kutolewa, Wakili Nassoro alisema sasa wanakwenda kujipanga ili ndani ya siku saba waweze kuwasilisha maombi hayo.
“Tunashukuru mahakama imekubali maombi yetu, kilichobaki ni kwenda kujipanga ili tuweze kuwasilisha maombi katika kesi ya msingi dhidi ya walalamikiwa wetu,” alisema Wakili Nassoro.
Katika kesi hiyo, Wakili Nassoro alidai mahakamani hapo, kuwa mbali na kuweka zuio hilo kwa msajili, pia kesi hiyo imelenga kuwashtaki waliokuwa wanachama 12 wa chama hicho wakiongozwa na Profesa Lipumba.
Alisema hoja nyingine katika kesi hiyo, ni pamoja na kumtaka msajili kutengua uamuzi wa kumrudisha Profesa Lipumba kwenye nafasi yake kwa madai alishavuliwa uanachama.
Alisema kitendo cha kiongozi huyo kuvamia ofisi za chama hicho na kuikalia kinyume cha sheria pamoja na kuharibu baadhi ya mali za chama hicho hakikubaliki.
Wakati Mahakama Kuu ikikubali maombi hayo, Profesa Lipumba amesema hakukuwa na haja ya kupeleka mahakamani suala hilo kwa kuwa litapoteza muda.
Akizungumza nje ya mahakama, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro alisema kitendo cha msajili kuziandikia barua Benki za NMB na Exim ili Profesa Lipumba aweze kufungua akaunti na kumpa ruzuku kinapaswa kupingwa.
Alisema mwenye mamlaka ya kuandika barua kwenda katika benki hizo, ni bodi ya wadhamini ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kusimamia mali za chama.
Alisema bodi hiyo ambayo imesajiliwa na Wakala wa Ufilisi na Udhamini (RITA) ambayo inawajibika chini ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na sio msajili au mwanachama aliyefukuzwa.
“Tunamshangaa Msajili wa Vyama vya Siasa kuendelea kumwandikia barua Lipumba, huku akijua kufanya hivyo ni kosa, kwa sababu wenye mamlaka ni bodi ya wadhamini,” alisema Mtatiro.
Alisema katika mchakato huo, bodi ya wadhamini kwa kushirikiana na Katibu wa Bodi wanapaswa kuandaa vikao kwa ajili ya kujadili suala hilo kabla ya kufikia uamuzi huo.
Alisema mpaka sasa bodi hiyo imeshangazwa na uamuzi wa Profesa Lipumba wa kufungua akaunti hiyo, huku ikihoji mahala alipozitoa nyaraka muhimu.
“Tunaamini Lipumba ameghushi nyaraka za kufungulia akaunti katika Benki ya Exim, kwa sababu wenye nyaraka hizo ni bodi ya wadhamini na si yeye kwa sababu ndiyo wanaosimamia masuala ya fedha na mali za chama chini ya Katibu Mkuu wa chama, Maalim Seif Sharif Hamad,” alisema Mtatiro.
Alimtaka Msajili kuacha kuingilia mausla ya chama hicho kwa madai kuwa kipindi hiki siyo cha Chama Cha TLP au NCCR-Mageuzi, bali ni zama za CUF ambao wamesimama imara kwa ajili ya kuhakikisha haki inatendeka.
Alisema kutokana na hali hiyo, chama hicho kimejipanga ili kuhakikisha kuwa suala hilo linamalizika kwa haki katika mahakama hiyo.
Hata hivyo, Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa, Sisty Nyahoza alisema barua aliyopewa Profesa Lipumba kwa ajili ya kufungua akaunti ni sawa na barua ya serikali za mitaa.
“Lipumba amepewa barua ya utambulisho kama zilivyo barua za serikali za mitaa kwa sababu kila chama kinapopata mwenyekiti mpya kinapaswa kuwasilisha barua ya kumtambua mwenyekiti huyo ndani ya ofisi hizo,” alisema na kuongeza:
“Lakini mpaka sasa Ofisi ya Msajili haijapokea barua yoyote ya kutomtambua Lipumba kama si mwenyekiti wa chama,” alisema Nyahoza.
Alisema taarifa za kuwapo baadhi ya viongozi wa chama hicho kuonana na msajili hazijafika kwenye ofisi hiyo kwa sababu vikao vyote vinavyofanyika vina utaratibu wake.
Na Patricia Kimelemeta – Mtanzania Digital
Jumanne, Oktoba 11, 2016
Jumanne, Oktoba 11, 2016
No comments :
Post a Comment