NA VERONICA ROMWALD
– DAR ES SALAAM
WODI ya Sewahaji, iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambayo alilazwa mke wa Rais, mama Janeth Magufuli hivi karibuni alipougua, imeharibika moja ya lifti zake kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.
Mama Magufuli alilazwa katika wodi hiyo Novemba 9, mwaka huu, baada ya kufikishwa hospitalini hapo akiwa amepoteza fahamu na kuruhusiwa Novemba 11, mwaka huu.
Jengo hilo lina lifti mbili, iliyoharibika ni ile ya upande wa kushoto na hivyo kubakia ya kulia ambayo nayo inaelezwa kuwa imechoka kutokana na kutumika muda mrefu sasa tangu jengo hilo lilipojengwa.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, mmoja wa wauguzi wanaohudumia katika jengo hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema ingawa wanaitumia hiyo iliyobaki, hata hivyo wana wasiwasi mkubwa.“Wengi wanatumia ngazi kupanda huko juu kwenda wodini, lakini kama mgonjwa yupo mahututi lazima tutumie lifti kumpandisha, binafsi natumia lifti mara nyingi kwa sababu miguu yangu huwa wakati mwingine inauma.
“Lakini kusema ukweli lifti yetu hii iliyobaki nayo imechoka… yaani unaingia humu ndani lakini unaomba Mungu utoke salama, isigome au kuzima,” alisema.
Pamoja na kuharibika kwa lifti hiyo, picha iliyopigwa wakati mama Magufuli akitoka ndani ya wodi hiyo nayo iliibua mjadala mkubwa, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Katika picha hiyo kulionekana kiti chakavu ambacho mara nyingi hutumiwa na walinzi wanaokaa kulinda lango la kuingilia ndani ya jengo hilo.
Aidha, kulionekana bawaba za milango ya jengo hilo zikiwa zimeng’oka kabisa.
Matatizo yaliyoainishwa katika picha hiyo tayari yameonekana kufanyiwa kazi na uongozi wa hospitali hiyo, ambapo juzi gazeti hili lilipita katika wodi hiyo tena na kushuhudia milango hiyo ikiwa tayari imerekebishwa bawaba zake ipasavyo.
Akizungumza na MTANZANIA Jumamosi, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa hospitali hiyo, Aminiel Eligaesha, alikiri kuwa wanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwamo hiyo ya uchakavu wa lifti zake.
“Kweli lifti za baadhi ya majengo yetu ni za muda mrefu, zimechoka na ile ya pale Sewahaji inafikisha mwaka sasa tangu ilipoharibika, hii ni changamoto kubwa kwetu,” alisema.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo, wamepanga kununua lifti nyingine na kubadilisha zile zilizokaa muda mrefu, ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi.
“Katika mwaka huu wa fedha wa 2016/17 tumepanga kununua lifti mbili mpya. Kununua zote mbili gharama yake tunakadiria kuwa ni Sh milioni 700, tutakapofanikisha tutawaita ili muweze kupeleka habari hizo njema kwa jamii,” alisema.
Hivi karibuni, katika ukurasa wake wa mtandao wa ‘Instagram’, Rais Dk John Magufuli aliandika kuwa sasa anaridhishwa na utendaji kazi wa wataalamu wa Muhimbili (MNH).
“Mabadiliko ya hospitali yetu ya Muhimbili yanaridhisha kwa sasa na huduma ziko katika kiwango kizuri, angalau kero zitapungua zaidi tukisimamia utendaji na uwajibikaji,” alisema.
/MTANZANIA
No comments :
Post a Comment